The House of Favourite Newspapers

Sheria ya mtandao inamfilisi 50

0

Mwanamuziki wa Hip Hop kutoka nchini Marekani, 50 Cent.

WALE wanaopenda muziki wa Hip Hop au wanaofuatilia showbiz ya kimataifa wanafahamu vizuri jinsi 50 Cent alivyo na ‘sinema’ nyingi katika maisha yake.

Moja kati ya mijengo anayomiliki 50 Cent.

50 Cent ambaye alikulia katika maisha ya kifukara kabla ya kupata utajiri mkubwa, amekuwa ni mtu wa kutawala katika vyombo vya habari kwa mambo tofauti, ikiwemo bifu, kutambia utajiri, lakini yote kwa yote anajua jinsi ya kupambana kuzitafuta fedha.

Awali ilijulikana 50 Cent ambaye jina lake kamili ni Curtis Jackson ana utajiri mkubwa, ghafla akatangaza kuwa amefilisika na anauza vitu vyake vingi vya thamani.Wakati akitangaza hivyo, siku chache baadaye akaonekana akionyesha nyumba kubwa ya kifahari aliyodai ni yake na anaijenga katika Bara la Afrika, pia alionekana sehemu tofauti za starehe akijiachia na kutumia fedha nyingi.

Kitendo cha kujitangaza kuwa amefilisika ilionekana ni ujanja wa kutaka kukwepa adhabu ya mahakama ambayo ilimtaka amlipe mwanamama Lastonia Leviston dola milioni 5 (Sh bilioni 10) kutokana na kuvujisha video yake ya ngono kwenye mitandao.

Leviston, 36, ambaye ni mzazi mwenza wa Rick Ross alishinda kesi na hivyo kutakiwa kulipwa fedha hizo, ukumbuke kuwa Rick Ross na 50 Cent hawana uhusiano mzuri.Wakati ikionekana anafanya maigizo, sasa 50 Cent ambaye aliingiza fedha nyingi zaidi mara baada ya kutoa albamu yake ya Get Rich Or Die Tryin mwaka 2003 ametangaza kuiuza nyumba yake yenye thamani kubwa.

50 aliinunua nyumba hiyo kwa bondia wa zamani, Mike Tyson, kwa dola milioni 4.1 (Sh bilioni 8.2) mwaka 2003, baada ya hapo akatumia dola milioni 6 (Sh bilioni 12) kuiboresha na kuifanya iwe ya kisasa. Mchakato wa kuiuza awali ulikuwa ni dola milioni 18.5 (Sh bilioni 37).

Nyumba hiyo yenye vyumba vya kulala 21 na mabafu 25, haikupata mteja kwa bei hiyo, imeingizwa sokoni tena kwa dola milioni 8.5 (Sh bilioni 17). Mwanasheria wa 50 Cent amedai mteja wake anataka kuiuza ili apate fedha za kulipa deni analodaiwa.

Mwanasheria huyo amesema sababu nyingine ya kuweka sokoni mjengo huo ambao umo ndani ya eneo analomiliki lenye ukubwa wa eka 17, ni gharama zake za kawaida kumshinda 50 Cent, anadai kuifanya nyumba hiyo iwe katika ubora wake gharama zake ni dola 72,000 (Sh milioni 144) kwa mwezi na pia kutunza bustani zote ni dola 5,000 (Sh milioni 10) kwa mwezi.

Ndani ya nyumba hiyo kuna ukumbi, casino, gym, jumla kuna vyumba 52, majiko tisa na ukumbi wa sinema. Bado haieleweki vizuri kama madai hayo ni ya kufilisika ni ya kweli.

Ikumbukwe kuwa Tyson aliiuza nyumba hiyo baada ya kuporomoka kiuchumi.
Wakati huohuo, mwanasheria huyo amesema kuwa Benki ya Sun Trust inamdai 50 Cent, 40, dola milioni 4 (Sh bilioni 8) ambazo alikopa kwa ajili ya kampuni yake ya kupromoti mchezo wa ndondi.

Sheria ya mtandao ya kuwashitaki wanaovuruga mambo katika mitandao, ndiyo imeanza kutumika Tanzania, hivi karibuni, mkasa huu unaweza kuwa darasa kwao. Kwani 50 Cent aliona ufahari kusambaza video hiyo ambayo imemtokea puani.

Leave A Reply