The House of Favourite Newspapers

Shigongo Aanika Jinsi Ubadhirifu Mkubwa Unavyofanyika Mfuko wa Bima ya Afya

0

Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo ameainisha matatizo makubwa matatu yanayoukabili Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), ikiwemo mifumo kati ya hospitali moja na nyingine kutosomana jambo linalosababisha wagonjwa wawe wanafanya kipimo kimoja zaidi ya mara moja wanapohama hospitali pamoja na ubadhirifu mkubwa kwenye mfuko huo.

Akizungumza bungeni wakati wa kuchangia Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote, Shigongo amesema mifumo inayotumika hivi sasa, ni Electronic Medical Record (EMR) ambao unakuwa na uwezo wa kusoma taarifa ndani ya hospitali au kituo kimoja cha afya.

Ameongeza kuwa ili mifumo isomane, inatakiwa kuunganishwa kwa pamoja kwa kutumia mfumo mkubwa wa Electronic Health Record System ambao utakuwa na uwezo wa kuunganisha hospitali zote nchini ili mgonjwa akipimwa kwenye hospitali moja, majibu ya vipimo yaweze kusomeka kwenye hospitali nyingine atakapopewa rufaa.

Tatizo la pili, Shigongo amesema ni ubadhirifu unaofanywa na watu wasio waaminifu ambao wanajitajirisha kupitia mfumo huo kwa kujaza taarifa za uongo za matibabu, kwa kutumia kadi za bima za afya.

Pia, Shigongo amesema tatizo linguine, ni mfuko huo kutokuwa na fungu maalum la kutoa elimu kwa wananchi ili kuzuia magonjwa yasitokee na badala yake, kusubiri watu waumwe ndipo waende kutibiwa. Shigongo amesema mfuko utenge asilimia chache za mapato yake kwa ajili yakutoa elimu hasa kuhusu mfumo wa maisha ambao ndiyo unaosababisha watu waugue magonjwa kama kisukari.

Leave A Reply