The House of Favourite Newspapers

Shikalo Atamba Kupiga Kazi ya Maana Yanga Sc

Faruk Shikalo

KIPA mpya wa Yanga, raia wa Kenya, Faruk Shikalo, amesema amekuja nchini kufanya kazi na kwa kuanza, ataanza na Kariobang Shark. Kauli hiyo ameitoa kipa huyo mara baada ya kutua kambini mkoani Morogoro ambako wameweka kujiandaa na msimu ujao.

 

Yanga wanatarajiwa kucheza na Kariobang katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa utakaopigwa Agosti 4, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Taifa, Dar katika kilele cha Wiki ya Mwananchi yenye kauli mbiu Funga Kazi, Kusanya Kijiji.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Shikalo alianza kwa kuwashukuru mashabiki wa Yanga kwa mapokezi makubwa aliyoyapata mara baada ya kutua nchini na kujiunga na timu hiyo.

 

Shikalo alisema kuwa, anataka kuona timu hiyo ikipata mafanikio ndani ya misimu miwili aliyosaini kuichezea Yanga kwa kuhakikisha anapambana golini ili kuchukua mataji yote watakayoshiriki likiwemo la ligi, linaloshikiliwa na Simba.

 

Aliongeza kuwa, hakuna litakaloshindikana kwake na kikubwa anaomba ushirikiano kutoka kwa wachezaji wenzake, benchi la ufundi, viongozi na mashabiki kwa ujumla ili kufanikisha hayo yote.

 

“Nimetoka Bandari na kuja Yanga kwa ajili ya kufanya kazi na siyo kitu kingine na kikubwa ni kuhakikisha ninaweka rekodi ya kuchukua makombe nikiwa na timu yangu mpya.

 

“Kwa kuanza, nimepanga kuonyesha uwezo wangu katika mchezo wetu wa kirafiki wa kimataifa tutakaocheza na Kariobang na baada ya hapo itafuata michezo mingine.

 

“Nikiwa na Yanga ninaamini nitafanikisha malengo yangu niliyojiwekea ikiwemo kuchukua makombe yote tutakayoshiriki, pia kufika katika hatua nzuri ya michuano ya kimataifa Afrika,” alisema Shikalo.

Comments are closed.