The House of Favourite Newspapers

Shishi: Ukitaka Kujua Moto Wangu, Mguse Mume Wangu

0

Amezaliwa Igunga mkoani Tabora  mwaka 1987. Jina lake halisi ni Zuwena Yusuph Mohammed. Ila wengi wanamtambua kwa jina lake la kisanii la Shilole au Shishi Baby.

 

Kwa mujibu wake, baba yake alimkimbia mama yake akiwa mtoto mdogo anayetambaa.

Alisoma Shule ya Msingi ya Igunga na akafaulu kwenda Sekondari ya Igunga, lakini aliishia kidato cha pili baada ya kubakwa na kubeba mimba akiwa na umri wa miaka 14 pekee.

 

Anaeleza kuwa, mtu aliyemfanyia kitendo hicho cha kinyama alikutana naye wakati akiwa anakwenda kuteka maji kisimani.

 

Mungu ni mwema; Shilole anasema baada ya miezi kadhaa kupita alijifungua mtoto mrembo wa kike aitwaye Joyce.

 

Baada ya hapo akaanza kutafuta riziki kwa kufanya biashara ndogondogo hadi alipokutana na staa wa Bongo Movies, Vincent Kigosi ‘Ray’ ambaye alimfungulia njia kwenye sanaa ya uigizaji.

Mungu si Athumani; mwaka 2010, alipata umaarufu mkubwa baada ya kuigiza Filamu ya Fair Decision ambayo ndani yake yumo Ray, Irene Uwoya, Johari, JB na mastaa wengine wengi wakubwa.

 

Filamu nyingine alizoshiriki ni Don’t Play, Chungu ya Nafsi, Curse of Marriage, Zawadi ya Birthday, Talaka Yangu na nyinginezo.

Hata hivyo, Shilole hakukaa sana kwenye tasnia ya Bongo Movies kwani aliamua kuingia rasmi kwenye gemu la muziki wa Bongo Fleva ambapo ametamba na anatamba na ngoma zake kama Lawama, Paka la Baa, Nakomaa na Jiji, Malele, My Photo, Pindua Meza na nyingine kibwena.

 

Pia Shilole ni msanii pekee wa Bongo Fleva na filamu, ambaye haoni aibu wala hajisikii vibaya kwa kutojua kwake Kingereza. Amekuwa mwepesi mno kutaka kujua Kiingereza na wala haoni aibu juu ya suala hilo; vicheko na kebehi vyote havijawahi kumkatisha tamaa.

 

Mbali na mambo yote hayo, kwa sasa mwanamama huyu ameamua kujikita zaidi kwenye ujasiriamali wa mama ntilie ambapo ana mgahawa wake unaoitwa Shishi Food na anakuambia anaweza kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja kwa sababu anajua jinsi ya kupangilia muda wake na kila kitu kinakwenda sawa.

 

Kwa kutambua mchango wake kwenye gemu la muziki, IJUMAA SHOWBIZ imemtafuta na kufanya naye mahojiano maalum (exclusive interview) ambapo anafunguka mambo mengi kuhusu maisha yake ya sasa na ana jambo gani la kuwasihi vijana ambao wanatamani kuwa kama yeye siku moja;

 

IJUMAA SHOWBIZ: Mambo vipi Shishi?

SHILOLE: Poa tu karibu.

Ijumaa: Asante, hongera naona biashara ya Shishi Food inazidi kukua

 

Shilole: Asante sana, juhudi, nidhamu na usafi ndio nguzo ya biashara yangu.

Ijumaa: Ooh safi sana, vipi lakini unayaonaje maisha ya ndoa kwa mara nyingine tena?

 

Shilole: Maisha ya ndoa ni mazuri sana, nisiwe muongo nae-njoy kupita kiasi.

Ijumaa: Watu wanasema kuwa uonaoleolewa sana, una lipi la kuwaambia?

 

Shilole: (Anacheka) Mimi huwa nasema kila siku kwamba kama kuolewaolewa ni rahisi kama wanavosema, basi na wao wafanye hivyo halafu tuone, jamani kuolewa ni bahati na mimi tayari nina hiyo bahati, waniache.

Ijumaa: Kitu gani ambacho hupendi kuona mume wako anafanyiwa?

 

Shilole: Kitu ambacho sipendi kuona mume wangu anafanyiwa ni kuonewa, au kutukanwa bila sababu, jamani hapo tutaonana wabaya, kwanza kwanini umtukane mume wangu? Sipendi hayo mambo mimi na nipo tayari kupambana na yoyote yule atakayemvunjia heshima mwanaume wangu.

 

Ijumaa: Wewe ni msanii ambaye umepitia changamoto nyingi wakati wa makuzi yako, ebu tuambie mara nyingi ukikutana na wasichana wadogo ambao wana danga huwa unawashauri nini?

 

Ijumaa: Kwanza huwa naumia sana, kama mama natamani mabinti wadogo wapate elimu ya kutosha kwa sababu huyo ndio mkombozi wao wa hapo baadae, lakini kuna wasichana wengine huwa nakutana nao tayari wameshaacha kusoma hivyo huwa nawashauri ni bora waanzishe biashara ndogondogo ambazo zitaweza kuwasaidia hapo baadae na sio kudangia wanaume hovyo, kwa sababu wakiendelea kufanya hivyo kuna uwezekano wakuja kupata magonjwa makubwa hapo baadae.

 

Ijumaa: Ni kweli kwamba kwa sasa unaratarajia kuitwa mama kwa mara nyingine?

Shilole: Jamani watu hawaishi maneno huko mitandaoni, mimi sina mimba lakini hata kama nitakuwa nayo kweli kuna shida gani? Mimi ni mke wa mtu hivyo lolote linaweza kutokea.

 

Ijumaa: Umewahi kutembea na mume wa mtu?

Shilole: Hapana na haitakuja itokee

 

Ijumaa: Mbona inasemekana kwamba hata Uchebe na huyu mume wako wa sasa wote uliwatoa kwa wake zao?

Shilole: Sio kweli, hakuna mwanaume ambaye nimewahi kumtoa kwa mke wake, mara nyingi nikianza kuwa nao kwenye uhusiano wa kimapenzi wanakuwa tayari wameshaachana na wanawake zao, sasa hapo huwezi kusema kuwa nimewachukua toka kwa wake zao.

 

Ijumaa: Umekuwa ukijishughulisha na mambo mengi kama vile muziki, filamu, ujasiriamali na vitu vingine vingi kwa wakati mmoja, tuambie unaweza vipi kupangilia muda wako?

 

Shilole: Kila kitu katika maisha huwa kinaenda kwa mipango, mimi nina ratiba zangu katika kazi, yaani najua sasa hivi nifanye nini na nini, ndio maana unaona kila kitu changu kinakwenda sawa na katika ubora uleule unaotakiwa.

STORI: Sifael Paul

Leave A Reply