The House of Favourite Newspapers

Shule ya Viziwi Buguruni Wapewa Vifaa na Kampuni ya AMC

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya magari ya AMC (Nissan) Tanzania, Christophe Henning,  akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusiana na msaada waliotoa katika shule ya Viziwi Buguruni ikiwa ni sehemu ya kurudisha faida kwa jamii kutokana na biashara wanayoifanya hapa nchini wakati wa hafla fupi iliyofanyika shuleni hapo  jijini Dar es Salaam.

KAMPUNI ya magari ya AMC Tanzania imepeleka furaha shule ya Viziwi Buguruni baada ya kukabidhi kwa uongozi wa shule bidhaa mbalimbali kwa ajili ya wanafunzi 237 wanaosoma katika shule hiyo.

Kampuni ya AMC Tanzania ndiyo wauzaji pekee wa magari aina ya Nissan nchini.

Akikabidhi vifaa hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya hiyo, Christophe Henning,  amesema kwamba wamejisikia fahari kuwasaidia wenye mahitaji.

Mwalimu Mkuu wa shule ya Viziwi Buguruni, Kulwa Milembe,  akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu furaha yao kwa ujio wa kampuni ya magari ya AMC (Nissan) Tanzania shuleni hapo wakati wa hafla fupi ya kukabidhi msaada wa mabegi na kompasi iliyofanyika shuleni hapo jijini Dar es Salaam.

Aidha alisema kwamba kampuni yake itakaa katika meza tena na uongozi wa shule hiyo kuona namna ya kuisaidia shule hiyo.

Kampuni hiyo ambayo kwa sasa inatimiza miaka mitano tangu kufunguliwa nchini imesema  inafanya hisani hiyo kurejesha faida kwa wananchi.

“Kama sehemu ya wajibu wetu wa kurejesha faida kwa wananchi,  tumeona tujikite kusaidia wenye mahitaji hasa watoto ili waweze kupata elimu katika mazingira bora kwani tunaamini vitu viwili (watoto na elimu),  hivyo ni muhimu katika maendeleo ya nchi,” alisema Henning.

Miongoni mwa bidhaa walizopewa wanafunzi ni mabegi na kompasi.

Alisema kwamba kampuni ya Nissan ambayo inatengeneza  mitambo mbalimbali,  inajivunia kaulimbiu yake ya ubunifu ambao umewafanya kuwa moja ya makampuni ya kutumainiwa duniani na yanayofanya biashara vyema.

Alisema kutokana na bishara zake,  wanapata nafasi ya kurejesha faida kwa jamii kwa kuwekeza zaidi kwa watoto wenye mahitaji na elimu yao.

Nissan ambao kwa sasa wapo Plot No. 6, Vingunguti Area, Nyerere Road na matawi katika miji mikuu ya kibiashara nchini kama Arusha, Dodoma, Zanzibar, Mwanza, Mbeya na Morogoro.

Katika hotuba yake mtendaji huyo aliahidi Nissan Tanzania kuendeleza ushirikiano na shule ya Buguruni kwa manufaa ya pande zote mbili ili kuleta ustawi katika jamii.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Kulwa Milembe akishukuru kwa zawadi hizo,  alisema kwamba wanafunzi wake wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo vifaa vya kubebea vitu kwa wanafunzi ambao wengine wametoka nje ya Dar es Salaam na familia zao ni maskini.

Alisema wanafunzi wengi wamekuwa hawana vibebeo vya madaftari, kwa hiyo msaada wa mabegi ni tunu kubwa kwao na kwamba pamoja na msaada huo aliiomba kampuni hiyo kuendelea kuwasaidia wanafunzi wake ili waweze kusonga mbele katika elimu.

Shule hiyo yenye wavulana 110 na wasichana 127 na kufanya jumla yao kuwa 237,  ina vitengo vya msingi, ufundi, awali na wasioona.

SHANGWE La YANGA Walivyofika HOTELINI Magomeni, MAKAMBO Atajwa!

Comments are closed.