The House of Favourite Newspapers

Si Nay wa Mitego tu… Hata Hawa ‘Walitumbuliwa’

0

Makala: Andrew Carlos

MWISHONI mwa wiki iliyopita Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) lilitoa tamko rasmi la kuufungia Wimbo wa Shika Adabu Yako ulioimbwa na staa wa Bongo Fleva, Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’ kuwa wimbo huo umekuwa na ukiukwaji mkubwa wa maadili, kashfa, uchochezi, kudhalilisha watu na kuhatarisha amani na utengamano miongoni mwa wasanii na jamii kwa ujumla.

Tukio la Nay kufungiwa ‘kutumbuliwa’ wimbo huo limemuweka katika orodha sawa na wasanii wa Bongo Fleva ambao nao walishatumbuliwa nyimbo zao na kupewa onyo. Wasanii hao ni pamoja na Madee (Tema Mate Tuwachape), Jux (Uzuri Wako), Snura (Nimevurugwa), R.O.M.A (Viva Roma Viva) na wengine wengi.

Mbali na ndani ya Bongo, wapo wasanii wengine kutoka Afrika ambao nao walishatumbuliwa nyimbo zao na katika makala haya yanawaanika.

Wizkid (Show You The Money na In My Bed)

Ayodeji Ibrahim Balogun ama Wizkid kama atambulikavyo kwenye muziki, mwaka jana alitumbuliwa na Shirika la Utangazaji la Nigeria (NBC) nyimbo zake mbili ambazo ni Show You The Money pamoja na In My Bed kupigwa kwenye TV kutokana na kukosa maadili.

Davido ft Meek Mill (Fans Mi)

Fans Mi ni moja kati ya ngoma za kimataifa ambazo alifanya David Adedeji Adeleke ‘Davido’ akishirikiana na rapa kutoka Marekani, Meek Mill. Video na wimbo huu kwa ujumla nao ulitumbuliwa na NBC kupigwa redioni na kwenye TV kutokana na kukosa maadili pia kuleta vishawishi juu ya matumizi ya dawa za kulevya.

Koffi Olomide (Selfie)

Nguli kunako muziki wa Bolingo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Koffi Olomide naye anaingia katika listi ya wasanii waliotumbuliwa nyimbo zao kusikika redioni na kwenye TV.

Hivi karibuni, Tume ya Kudhibiti Maadili Kongo iliitumbua albamu yake mpya ya 13ieme Aporte ambayo ilikuwa na nyimbo takriban 39 ukiwemo wa Selfie kutosikika redioni huku sababu zikiwekwa wazi kuwa neno ‘Ekoti te’ limetumika katika kila wimbo kwenye albamu hiyo ambalo tafsiri yake ni tusi.

Olamide (Bobo na Indomie)

Olamide Adedeji ambaye ni rapa anayebamba kunako gemu la Hip Hop Nigeria naye anaingia katika orodha ya wasanii wa Afrika waliotumbuliwa nyimbo zao.

Olamide alitumbuliwa na NBC nyimbo zake za Bobo na Indomie kutosikika redioni na kwenye TV kutokana na kuwa na lugha ya matusi na pia baadhi ya mashairi yake yanaashiria kuleta uchochezi katika jamii.

Iyanya (Gifts)

Iyanya Onoyom Mbuk naye ni mmoja wa wasanii wa Nigeria walioingia kwenye utumbuliwaji wa nyimbo zao ambapo wimbo wake wa Gifts alioshirikiana na Don Jazzy ulitumbuliwa kutoonekana kwenye TV wala kusikika katika redio yoyote nchini Nigeria kutokana na kukosa maadili.

Leave A Reply