The House of Favourite Newspapers

Mchungaji afumaniwa, apigwa faini Sh. 400,000

0

MWANZA: Mchungaji wa kanisa moja la kiroho lililopo Igoma jijini Mwanza aliyejulikana kwa jina moja la Michael (36), amelipa faini ya ugoni baada ya kudaiwa kufumaniwa na mke wa mtu kwenye nyumba ya kulala wageni iliyopo  wilayani Misungwi jijini hapa.

 James Daudi (30), mkazi wa Kijiji cha Mbela wilayani Misungwi ambaye ndiye mwenye mke, alisema, Februari 11, mwaka huu alilipwa na mchungaji huyo kiasi cha Sh. 400,000, fedha aliyojihukumu yeye mwenyewe baada ya kumkuta chumbani na mke wake.

 “Ilikuwa Januari 20, majira ya mchana, nilipewa taarifa na msamaria mwema kuwa kuna jamaa yupo na mke wangu gesti (jina lipo) chumba namba 103. Nilikwenda nikiwa na rafiki yangu, mhudumu akatuzuia kuingia na kufunga mageti akitaka tutafute uongozi,” alisema  James.

 Akaendelea: “Nilitoka kwenda kumtafuta Afisa Mtendaji wa Kata ya  Misungwi, alipofika tayari mhudumu alikuwa amefungua mageti, tukamuona mchungaji akitoka katika chumba hicho na kupitia mlango wa nyuma ambako aliacha gari lake.

“Tukiwa na mtendaji na watu wengine, tuliingia kwenye kile chumba na kumkuta mke wangu yumo chumbani akishangaashangaa. Wakati tunajadiliana, tulielezwa kuwa kumetokea ajali gari limeangukia mtaroni, tulipotoka nje tulimkuta mchungaji ameingiza gari hilo mtaroni ndipo alikiri kuwa alikuwa na mke wangu. Akaahidi kulipa faini ambapo kwenye kulipa, alikuja na mkewe kama shahidi.”

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Misungwi, Emaculata Renana alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kueleza kuwa Mchungaji Michael akiwa na mkewe kama shahidi, alilipa Sh. 400,000 za faini ya ugoni.

 Mwandishi wa habari hizi alimtafuta kwa simu mchungaji huyo ambapo aliomba apigiwe saa 1:00 usiku kwa madai kuwa muda huo alikuwa akiendesha gari. Ilipofika muda huo, hakupatikana hewani.

 “Niko Sengerema nilikuwa msibani, hivi sasa niko barabarani nakuja Mwanza kwa gari, naomba unipigie saa 1:00 usiku nitakuwa nimefika,” alisema mchungaji huyo.

 Jumatatu ya Februari 15, mwaka huu, mwandishi wetu alimpigia simu tena na kuomba apigiwe baada ya nusu saa. Alipopatikana muda huo na kuulizwa juu ya fumanizi hilo, alijibu kwa mkato: “Silijui jambo hilo,” kisha akakata simu.

Leave A Reply