The House of Favourite Newspapers

Sifa za Mwenza Mzuri Maishani

0

HAKIKA Mungu ni mwema na anaendelea kutupigania kwenye kipindi hiki kigumu cha gonjwa hili la COVID-19. Anatukinga na anatulinda, hivyo ni vyema tumshukuru. Kwa wale ambao kwa namna moja au nyingine wamepata maambukizi ya Virusi vya Corona, wasihofu.

 

Kupata ugonjwa huu siyo mwisho wa maisha. Wapo wengi wamepata na wamepona, hivyo amini kwamba Mungu atakuponya na utaendelea na maisha yako kama kawaida. Muhimu zaidi kwa ambao hawajaambukizwa ni kuchukua tahadhari zinazotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Afya.

 

 

Tukirudi kwenye mada yetu ya leo, kwa hakika hakuna ambaye hataki kuwa na mwenza mzuri maishani mwake. Mtu ambaye atakuwa furaha kwenye maisha yake. Hili ni jambo ambalo linamgusa kila mmoja wetu. Hakuna anayependa karaha kwenye maisha ya uhusiano.

 

 

Ndiyo maana watu hufurahia sana pale wanapowaona wapendanao fulani wanaishi vizuri. Kama yeye uhusiano wake unakwenda ndivyo sivyo, siku zote anajisikia vibaya. Anatamani yale maisha ya wenzao ndiyo yangekuwa ya kwake.

 

 

Leo nataka tujifunze tabia ambazo ni nzuri kwa wapendanao. Ndugu zangu, muunganiko wa mwanamke na mwanaume huwa una maana kubwa sana kama tu mtakuwa watu wa kusikilizana. Watu ambao mnazungumza lugha moja kwenye safari yenu.

 

 

Hatukatai, safari ya uhusiano haikosi milima na mabonde, lakini jambo la muhimu la kuangalia ni kutokuwa kwenye safari yenye milima tupu. Yaani ninyi hamna tambarare wala mteremko hata siku moja. Kila siku mpo kwenye vita ya uhusiano.

 

 

Hili ndilo jambo ambalo mara kwa mara nimekuwa nikilizungumza kwenye mada zangu mbalimbali hapa na kwingineko. Maisha ya mwanadamu yanapambana na ‘stresi’ nyingi sana.

Kuna stresi za kiuchumi, kukosa kazi au biashara kwenda vibaya na mambo mengine mengi.

 

 

Mtu unaweza kukuta hukupanga kabisa kwenda kugombana na mtu, lakini unajikuta tu mtu ameingia kwenye anga zako na kuanza kukukwaza. Hujamkosea wala nini, lakini ameamua tu kukuletea jambo ambalo litakusumbua nafsi yako.

 

 

Sasa unapokutana na stresi nyingi za aina hiyo, furaha pekee ambayo itakufariji ni ya kutoka kwa mwenza wako. Yeye ndiye kimbilio lako la kujifariji. Atakutia moyo. Atakutoa kwenye mawazo au msongo ambao pengine ulikuwa nao siku nzima.

Hivyo basi, endapo ukiwa na mwenza sahihi, atalichukua jukumu hilo ipasavyo. Hatakuwa sehemu ya kukuongezea karaha. Sanasana atakutia moyo na nguvu mpya. Kinyume na hapo ni yule mtu wa kukuongezea karaha, itakuwa ni mzigo mara mbili kwako.

 

 

Japo ni ngumu kumpata mwenza ambaye atakuwa msikivu asilimia mia moja, mstaarabu na mwenye kusikiliza zaidi kuliko kutenda, lakini jitahidi sana kumtafuta mtu wa aina hiyo. Usikubali kuingia kwenye uhusiano na mtu ambaye unamuona kabisa ni tatizo kwako.

 

 

Mtu ambaye kelele na fujo ni sehemu ya maisha yake, huyo hafai. Mtu muda wote ana jazba na hana jema, wa nini?

Ni vigumu sana kumtambua kutokana na baadhi ya watu kuficha tabia zao mwanzoni, lakini kadiri mtu unavyomweka karibu, utamjua tu ni mtu wa aina gani.

 

 

Ukijiridhisha kwa muda mrefu kwamba ni msumbufu na umejaribu kufanya kila linalotakiwa kufanya kumuweka sawa, lakini habadiliki, ni bora kuahirisha safari naye. Subiri utampata mwingine ambaye atakuwa furaha kwenye maisha yako.

Asanteni kwa kunisoma.

 

 

Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri. Mnaweza kunifuata kwenye mitandao yangu ya kijamii. Instagram&Facebook: Erick Evarist, Twitter: ENangale.

 

Leave A Reply