The House of Favourite Newspapers

Sikinde OG Kumenoga, Yampa Mkataba Skassy Kasambula Na Waimbaji Wengine Wawili

0
Skassy Kasambula akizungumza na vyombo vya habari baada ya kuingia mkataba na Sikinde OG.

Skassy Kasambula, nyota wa nyimbo pendwa kama “Christina Moshi” , “Kipipa Ayubu”, “Ajali ya Aminani”, “Salmada” na “Onyo” amejiunga na bendi ya Sikinde OG. Mwimbaji huyo mwenye sauti tamu, ametambulishwa leo mchana Magomeni, jijini Dar es Salaam kwenye mazoezi ya bendi hiyo.

Meneja wa Sikinde OG, Juma Mbizo amewaaambia waandishi wa habari kuwa kuanzia sasa Skassy Kasambula ni msanii wao mpya na ataanza kuonekana jukwaani wiki ijayo. Skassy Kasambula ambaye alihamishia makazi yake nchini Kenya tangu mwaka 1997, amewataka mashabiki wa muziki wa dansi watarajie makubwa kutoka kwake.

Meneja wa Sikinde OG, Juma Mbizo.

Mwimbaji huyo akasema: “Nina hazina ya nyimbo nyingi mpya, nzuri kuliko zile nilizowahi kurekodi miaka ya nyuma. Nitatanguliza mbili “Nifungulie Mlango” na “Aisha. Nimechagua kujiunga na OG kwa kuwa ina wasanii wengi ambao nimewahi kufanya nao kazi akiwemo Fresh Jumbe, Ally Yahaya na Omar Seseme, hii itanipa urahisi wa kufanyia kazi nyimbo zangu mpya na za zamani,” amesema Skassy Kasambula.

Kihistoria, Skassy alizitumikia bendi za Super Matimila, Toma Toma, OSS ya Dukuduku na Ndekule, Sambulumaa na Ngorongoro Heroes kabla hajahamia Kenya. Ametunga zaidi ya nyimbo 70 ukiwemo Christina Moshi ambao ni moja ya nyimbo kubwa sana kwenye soko la muziki wa dansi.

Wimbo huo uliorekediwa na OSS (Ndekule) mwaka 1986, ulipelekea albam yake iliyobeba nyimbo sita iuze zaidi ya nakala ya kanda 200,000 kupitia kampuni ya JO Traders. Mbali na Skassy Kasambula, OG pia imeongeza waimbaji wengine wawili akiwemo nyota wa zamani wa Mwenge Jazz, Hussein Matamile na Awadh Mbulu kutoka Bongo Beats.

Juma Mbizo amesema bado bendi yao inaendelea kuimarishwa na wana maombi ya wasanii wengi wanaotaka kujiunga nao.

“Usajili unaendelea, OG lengo letu ni kupiga wimbo wowote ule (wa bendi yetu au bendi nyingine) kwa ubora ule ule kama ulivyorekodiwa na hii ndio sababu kubwa ya sisi kujiita original'” alifafanua Juma Mbizo na kusema sasa ni watu wataipata “Christina Moshi” halisi.

Leave A Reply