The House of Favourite Newspapers

SIKU CHACHE KABLA YA KUOLEWA, MREMBO ANYONGWA GESTI

Kibua Adamu.

 

NI tukio la kutisha! Wakati akiwa kwenye mipango kabambe ya kuolewa siku chache zijazo, mrembo aliyetajwa kwa jina la Kibua Adamu, anadaiwa kunyongwa na mchumba’ke, Mwita Marwa (30), ndani ya nyumba ya kulala wageni (gesti), Uwazi lina simulizi ya kukutoa machozi.

Kibua ambaye ni mkazi wa Mazimbu mjini hapa, alikutwa na tukio hilo la kutisha wiki iliyopita kwenye gesti hiyo maarufu ijulikanayo kwa jina la Luta iliyopo Mtaa wa Nguzo katika Kata ya Mazimbu, jirani na Hosteli za SUA mjini hapa.

 

NI DENTI WA SUA

Habari zilizopatikana kutoka kwa chanzo ndani ya gesti hiyo zilidai kwamba, Kibua alinyongwa na mchumba’ke huyo ambaye alidaiwa kuwa ni Mwanafunzi wa Mwaka wa Tatu wa Chuo Kikuu Cha Kilimo Cha Sokoine (SUA) cha Morogoro wakati mrembo huyo akiwa ni mfanyakazi kwenye gesti hiyo, upande wa baa.

Chanzo hicho kilieleza kuwa, baada ya kujiri kwa tukio hilo baya na taarifa kusambaa majira ya saa 4:00 asubuhi, Afisa Mtendaji wa Kata ya Mazimbu, Alatutisha Sanga ndiye aliyetoa taarifa polisi na kwa mwandishi wetu.

Uwazi, likiwa eneo la tukio, lilifanya mahojiano na mlinzi wa gesti hiyo, Abdallah Eliferiti juu ya ni nini kilitokea ambapo alisimulia:

 

MLINZI ASIMULIA

“Inauma sana. Unajua tulikuwa tunafanya kazi na Kibua. Yeye alikuwa upande wa baa. Ni kweli alikuwa na mchumba am­baye kimsingi tunamfahamu na jana (siku ya tukio) yeye na huyo mchumba’ke walikuwa wamekaa hapa baa na wal­ionekana kama wanagombana maana yule jamaa alikuwa anamtuhumu Kibua mambo f’lanif’lani.

 

 

Mwili ukiwa kwenye defenda la polisi.

 

WIVU WA KIMAPENZI

Kinachoonekana kulikuwa na ishu ya wivu wa kimapenzi. Walikaa kwa muda mrefu sana hadi tulipofunga baa usiku.

“Baada ya baa kufungwa Kibua na mchumba’ke wali­chukua chumba, wakaingia kulala.

“Cha ajabu kulipokucha leo, majira ya saa 4:00 asubuhi, kaka zake Kibua walifika hapa na kuniuliza Kibua yuko wapi?

“Niliwaambia kuwa kuwa yupo chjumbani na mtu wake, wakaniambia nisome meseji kwenye simu waliyokuwa nayo.

“Nilipoisoma meseji hiyo ili­kuwa ya vitisho (haviandikiki gazetini) kiasi kwamba hata mimi iliniogopesha sana.

 

Mhudumu akionyesha damu eneo la tukio.

 

“Baada ya hapo niliwaongoza hadi kwenye chumba wali­chokodi, tulipogonga hakuku­wa na mwitikio wowote hivyo tulijaribu kufungua, lakini ulikuwa umefungwa.

“Tulipochungulia dirishani tulimshuhudia Kibua akiwa kitandani na alionekana kabisa kuwa alishafariki dunia huku huku shuka likiwa na damu kibao hizi hapa (ana­muonesha mwandishi wetu shuka lenye damu.” Mlinzi huyo alipotakiwa kueleza vit­isho vya meseji hiyo alisema:

“Kama nilivyokuambia Kibua na huyo mtu wake walikuwa wachumba hadi nyumbani kwa akina Kibua jamaa huyo alikuwa anafahamika kwani malengo yao yalikuwa ni kufunga ndoa mwaka huu baada ya mwanaume huyo kumaliza chuo.

“Sasa jamaa huyo aliwatumia meseji shemeji zake, yaani wadogo zake Kibua ambayo ilisomeka; ‘Sina sababu ya kuendelea na maisha, nime­shamuua Kibua na mimi nina­jiua…mkifika gesti mtakuta maiti mbili’.

 

AFISA MTENDAJI WA KATA

”Basi baada ya kuuona mwili huo kupitia dirishani, tulitoa taarifa kwa Afisa Mtendaji wa Kata ya Mazimbu, Alatutisha Sanga ambaye naye alitoa taarifa polisi ambao walifika kisha wakafunja mlango na kuushuhudia mwili wa Kibua ukiwa umenyongwa na kuu­chukua kwa ajili ya uchunguzi na kwenda kuuhifadhi kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.

“Kiukweli ni tukio ambalo limewasikitisha sana ndugu, jamaa, marafiki na wakazi wa maeneo haya ndiyo maana umati mkubwa ulikusanyika na kufunga mitaa. Unajua Kibua alikuwa maarufu sana mitaa hii kutokana na ucheshi na mvuto aliokuwa nao.”

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa Kata ya Maz­imbu, Alatutisha Sanga alisema kuwa, tukio hilo ni la kulaaniwa vikali na ku­waomba wapenzi kumaliza tofauti zao kabla ya kusaba­bisha maafa kama hayo.

 

MTUHUMIWA ATIMKA

Ilidaiwa kuwa, baada ya kufanya mauaji hayo, mtuhumiwa huyo alikwenda hosteli na kuchuchukua kilicho chake na kutimkia kusikojulikana, lakini kukiwa na taarifa kwamba huenda amerudi nyumbani kwao mkoani Mara. Kwa upande wake, mwenyekiti wa seri­kali ya mtaa huo, Velisiani Katabaro alilithibitishia Uwazi kutokea kwa tukio hilo kwenye mtaa wake.

 

 

Mashuhuda.

 

KAMANDA MATEI

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, ACP Ulrich Matei alithibitisha kunyongwa kwa Kibua huku akiahidi polisi kufanya kazi yake ya uchun­guzi ili kumkamata mtuhu­miwa huyo na kumfikisha kwenye vyombo vya sheria.

“Ni kweli tukio hilo limetokea, lakini ngojeni polisi wafanye kazi yao ya uchunguzi ili mtuhumiwa akamatwe na ku­fikishwa mahakamani kujibu tuhuma za mauaji,” alisema Kamanda Matei.

Kibua ambaye hakuacha mtoto, alizikwa Jumamosi iliyopita na umati mkubwa kwenye Makaburi ya Kola mjini hapa huku mtuhumiwa akidaiwa kutuma meseji kwa ndugu wa mrembo huyo akieleza kuwa alitamani mno kushiriki maziko ya mwandani wake huyo.

 

MTAALAM WA SAIKOLOJIA

Akizungumza na Uwazi juu ya kwa nini siku hizi kumekuwa na mauaji ya wapenzi, Mha­dhiri wa Saikolojia wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Chriss Mauki alisema kuwa, hali hiyo inatokana na wapen­zi wengi kukosa uaminifu na upendo wa dhati kupoa hivyo ni lazima wapenzi wanapogo­mbana watafute suluhu na siyo kujichukulia hatua kwa hasira.

“Tupo kwenye kipindi kibaya cha watu wengi kupoteza upendo ule wa mwanzo, ku­chokana na kusalitiana hivyo hapa panahitaji uangalifu sana hasa kwa wale wapenzi ambao bado hawajafunga ndoa. Ni vyema kutafuta ushauri wa kitaalam na siyo mpenzi kujichukulia tu hatua na kumuua mwenza wake,” alisema Mauki.

 

 

MCHUNGAJI ATIA NENO

Kwa upande wake, Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Jeru­salem lililopo Kitunda, James Nyakia alisema kuwa, hali kama hiyo imekuwa ikitokea kutokana na watu kukosa hofu ya Mungu na kutaka kujifanyia mambo yao bila kumshikisha Mungu katika kila wanalolifanya.

“Wengi hawana hofu ya Mun­gu kwa sababu wamemuacha Mungu. Vijana wa sasa hawana mwamko na masuala ya kumtumikia Mungu ndiyo maana unakuta wanaadhibi­wa kwa vifo vingi vya ujanani. Nawashauri wamrudie Mungu kwani mchumba aliyetoka kwa Mungu hawezi kumuua mwenza wake kwani ndani yake kuna uungu,” alisema mchungaji huyo.

 Stori: DUNSTAN SHEKIDELE, Moro

Comments are closed.