SIMBA CHUNGA HAWA JUMAMOSI TAIFA

Kikosi cha JS Saoura.

KATIKA kitu ambacho Simba watafurahia wikiendi hii kwenye Uwanja wa Taifa katika mechi dhidi ya JS Saoura ni shangwe nzito za mashabiki wao ambao watakuwa wakiongozwa na msemaji wao Haji Manara ambaye atapiga kambi kuzunguka majukwaa ya kawaida.

 

Lakini tathmini ya kiufundi inaonyesha kwamba wapinzani wao kwenye mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika, watacheza soka la pasi lakini la kujilinda sana huku wakiwategemea watu watano.

 

Video mbalimbali za timu hiyo zinaonyesha kwamba ikiwa ugenini kwenye mechi za ligi inaweka ukuta mzito na kuacha watu wachache mbele lengo likiwa ni kulazimisha sare au suluhu.

 

Hivyo Simba inapaswa kuwabana kwelikweli. Staili hiyo huenda ikawapa nafasi kubwa Simba ambao wamepania kushambulia kwa nguvu kupitia katikati na pembeni jambo ambalo huenda likaibua shangwe kubwa haswa kutokana na staili mpya ya kushangilia iliyopewa jina la ‘Yes We Can’ chini ya Manara.

Waalgeria hao ambao tayari wametanguliza watu Dar, hupenda kupiga pasi fupi ili kumchanganya mwenyeji, hawana uzoefu na michuano ya kimataifa kwani huu ndiyo msimu wao wa kwanza tangu wapande daraja.

 

Katika tathmini zao za mechi mbalimbali za ligi na kimataifa ambazo Spoti Xtra imeziona mpaka kufikia wikiendi iliyopita, inaonyesha kwamba wana wachezaji watano wa kuchungwa lakini Thomas Ulimwengu si miongoni mwao.

 

Wachezaji hao wazoefu ndiyo wamecheza mechi nyingi msimu huu, wamepachika mabao ya timu hiyo pamoja na
kutoa asisti zinazoibeba timu na wasipocheza kocha anatokwa jasho kwenye benchi. Wa kwanza kiungo mshambuliaji, Mohammed Hammia anayevaa jezi namba 26.

Yeye amecheza michezo 13 na ametupia mabao matatu vilevile na amekuwa mhimili mkubwa wa timu hiyo kutokana na ufundi wake na kupaka rangi anavyokuwa kwenye eneo lake. Straika Mohammed Boulaouidet aliyecheza mechi tisa akiwa na mabao matatu pia ni tishio na tegemeo kubwa, yeye anavaa jezi namba 11. Anajua kulitumia umbo lake.

MoustaphaDjallit ndiye mshambuliaji wao wa kati na wanamuaminia sana. Yeye amecheza mechi 11 akatupia mabao matatu lakini uwepo wake uwanjani umekuwa ukitoa faida kwa wenzake kufanya madhara.

 

Ana jezi namba 17 na ndiye nahodha wao. Hamza Zaidi ni winga yao ya kushoto amecheza mechi 16 na kupachika mabao mawili lakini ni bingwa wa asisti, ni miongoni mwa wachezaji waliocheza mechi zote msimu huu na haumii hovyo huku sifa yake kubwa ikiwa ni mbio na mwili wake ni kama Emmanuel Okwi alivyo.

Anava jezi namba 19. Wana beki wao mmoja ambaye ni kazikazi kama ilivyokuwa kwa enzi za Nadir Haroub ‘Cannavaro’ akiwa kwenye fomu Yanga, huyu anaitwa Ibrahim Bekakchi anavaa jezi namba 4 amecheza mechi 12 na ametupia bao moja la kichwa na asisti mbili. Kwa upande wa kocha wa Simba Patrick Aussems amesema Wachezaji wake wana mzuka wa kutosha na mashabiki waje Uwanjani kwa kujiamini.

 

“Tumekuwa na muda mwingi wa kujiandaa kule Zanzibar. Ninafahamu fika umuhimu wa mchezo huo na tayari tumeshaandaa mbinu kali ambazo zitatufanya tupate matokeo mazuri kwenye mechi hiyo.”

 

“Tumejiandaa vya kutosha na uzuri ni kwamba kila mmoja anafikiria mechi hiyo na ameipa uzito wa kutosha, kikubwa watu waache presha kisha waone ni kitu gani ambacho tutakifanya mbele ya Waarabu hao,” alisema Mbelgiji huyo ambaye amecheza mechi nne kwenye klabu Bingwa hadi sasa, ameshinda tatu na kufungwa moja.

 

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Loading...

Toa comment