The House of Favourite Newspapers

Simba Day Ni Balaaa Uwanja wa Taifa

SIMBA leo Jumatano, itavaana na timu ya Asante Kotoko ya kutoka Ghana ukiwa ni mchezo maalum wa Simba Day.

 

Simba Day ni mfululizo wa wiki ya Simba ambayo imekuwa ikifanyika kila mwaka na kilele chake kinakuwa tarehe 8, Agosti ambayo ni leo.

 

Siku hii Simba huitumia kwa kwa ajili ya kutambulisha wachezaji wapya ambao wamesajiliwa na Simba kuelekea msimu mpya siku ambayo inafahamika kama Simba Day.


Mchezo huo na sherehe hiyo kwa ujumla itafanyika katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, huku mgeni rasmi akiwa ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Kassim.

 

Simba Day itaadhimishwa leo ikiwa ni mara ya kumi tangu kuanzishwa kwake mwaka 2009, ambapo imekuwa ikifanyika kila mwaka.

Simba hutumia siku hiyo pia kuwatambulisha wachezaji wake wote ambao itawatumia kwenye msimu mzima na benchi la ufundi.

 

Lakini baada ya hapo itafuatia mchezo wa kirafiki ambao kwa mwaka huu utakuwa dhidi ya Asante Kotoko ya Ghana.  Maandalizi  ya sherehe za Simba Day mwaka huu  yamekuwa tofauti na  nyuma kutokana na uwepo wa hamasa kubwa hasa katika shughuli za kijamii ambazo zilifanyika nyuma kabla ya kufika siku ya leo Jumatano.

 

Watakaotambulishwa rasmi

Wachezaji ambao wamesajiliwa na Simba safari hii ni pamoja na, Meddie Kagere, Pascal Wawa, Deogratius Munishi, Adam Salamba, Mohamed Rashid, Hassan Dilunga, Chama Claytous na Marcel Kaheza.

 

 Shughuli za kijamii

Kuelekea siku hiyo maalum viongozi wa Simba pamoja na mashabiki na wadau wa soka waliweza kujitokeza katika zoezi la uchangiaji damu kwa watu wenye mahitaji ambapo zoezi hilo lilifanyika Jumapili katika eneo la Ilala Boma jijini Dar.  Haikuishia hapo mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo waliweza kufanya usafi katika Fukwe za Hospitali ya Aga Khan siku ya Jumapili.

Pia wachezaji wa Simba walitembelea kituo cha watoto yatima Kawe.

 

Mastaa kibao kunogesha Simba Day

Mastaa kibao wa muziki pamoja na filamu ambao ni mashabiki wa Simba wataongoza kwa kutoa burudani ya muziki wakiongozwa na bendi ya Africans Stars Twanga Pepeta, Mwasiti, Tundaman, Msaga Sumu huku waigizaji kama Jacob Steven ‘JB’, Monalisa, Idriss Sultan na wengine kibao watapamba siku hiyo.

Hata hivyo, ikumbukwe Simba Day ina historia katika nchini hii tangu kuanzishwa kwake mwaka 2009.

 

 Watambulisha jezi zao mpya

Simba ilizindua jezi zake rasmi orijino juzi kuelekea msimu mpya huku ikipata udhamini wa mil 250 kutoka Mo Energy.

 

SC Villa yaweka rekodi

Ndiyo timu ambayo imeweka rekodi kwa kuwa timu ambayo imecheza na Simba mara nyingi zaidi katika Simba Day ambapo imekutana na timu hiyo mara tatu .

Simba Day ya kwanza SC Villa ilicheza na Simba na kufungwa bao1 -0, huku mwaka 2013, ilifungwa tena na Simba mabao 4-1 na mara ya mwisho walikutana mwaka 2015, Simba ilishinda 1-0.

Lakini Simba iliwahi kukutana na timu kama Express ya Uganda na kutoa sare ya bila kufunga hiyo mwaka 2010, mwaka ulifuata walicheza na Victors Simba ilipigwa bao  1-0 mwaka uliofuata wa 2012 ikaambulia kipigo tena cha mabao3-1 toka kwa Nairobi City, Zesco ya Zambia na ikawapa kichapo cha mabao 3-0 ilikuwa mwaka 2014.

 

Mwaka 2016, Simba iliweza kutoa dozi kwa AFC Leopard ya Kenya kipigo cha mabao 4-0 huku mwaka jana wakiichapa Rayon Sports ya Rwanda kwa bao 1-0.

 

Rekodi pekee

Tangu Simba Day kuanzishwa na leo ikiadhimisha miaka kumi  siku hiyo imewahi kufanyika nje ya Dar es Salaam mara moja tu katika jiji la Arusha na ilikuwa ni mwaka  2011, ambapo Simba  ilicheza mchezo wake dhidi ya  Victoria na ilipoteza mchezo huo.

 

 

 

Comments are closed.