Simba Hawaukosi Ubingwa

KWA staili hii Simba inakosaje ubingwa wa Ligi Kuu Bara? Vigogo wa Simba wameibuka na kutangaza ofa mpya kwa wachezaji wa timu hiyo kwamba kila mechi watakayoshinda kila mchezaji atapata fedha ya maana.

 

Simba hadi hivi sasa tayari imefanikiwa kushinda michezo 12 ya ligi kuu kati 17, ikitoka sare michezo mitano huku ikiwa haijapoteza mchezo wowote.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, wachezaji hao wameongezewa morali ya kupata ushindi na kuwawekea motisha ya fedha kwa kila mechi watakayoshinda ya ligi kuu na michuano ya kimataifa Afrika.

 

Simba hivi sasa inawategemea zaidi Emmanuel Okwi na John Bocco katika kupata ushindi. Mtoa taarifa huyo alisema, motisha hiyo ya fedha imegawanywa kwa mafungu, ipo inayowahusisha wachezaji wa kikosi cha kwanza, akiba na wanaokaa ambao wao wanapata sawa.

 

“Kiukweli hivi sasa mabosi na viongozi wa Simba, wamedhamiria kuuchukua ubingwa wa ligi kuu msimu, kwani wameandaa motisha kwa wachezaji kwa kila mechi watakayoshinda pekee.

 

“Kama wakitoka sare au kufungwa, hakuna motisha yoyote ya fedha inayotolewa na kikubwa wao wanataka ushindi pekee ili kuendelea kukaa kileleni na kutowapisha wapinzani wetu.

 

“Fedha hizo za motisha zimegawiwa hivi, wachezaji wa kikosi cha kwanza wenyewe wanapewa shilingi 400, 000 kila mmoja na wale wa akiba na benchi wanapata 200, 000 kila mmoja,” alisema mtoa taarifa huyo. Alipotafutwa kocha msaidizi wa timu hiyo kuzungumzia hilo, alisema:

 

“Hili la motisha ni zuri linaleta hali ya kujituma na kupambana wachezaji wanapokuwa uwanjani na kupata matokeo kwani hilo ndiyo lengo letu kubwa.”

 

Mbali ya motisha hii mpya ambayo itawafanya wachezaji kuvuna mamilioni ya fedha kama wakiendelea kushinda mechi zao hadi mwishoni mwa msimu, wachezaji wa timu hiyo wamekuwa wakigawana Sh milioni 10 kutoka kwa mwekezaji Mohamed Dewji ‘Mo’ kwa kila mechi wanayoshinda.

 

Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Loading...

Stori zinazo husiana na ulizosoma

Toa comment