The House of Favourite Newspapers

Simba Izuie Mechi za ligi kama Inataka Usalama

Wachezaji wa timu ya Simba.

SIMBA, kesho Jumamosi itakuwa tena uwanjani kutafuta pointi tatu muhimu nchini DR Congo itakapokuwa ikivaana na AS Vita Club. Kumbuka kuwa Simba ndiyo inaongoza kundi lake ambalo lina timu za Al Ahily, JS Saoura na AS Vita.

 

Kulikuwa na maneno mengi sana baada ya Simba kushinda mchezo wake dhidi ya JS Saoura kwa mabao 3-0, kuwa hakikuwa kipimo sahihi kwao kwa kuwa AS Vita na Al Ahily ndiyo timu kubwa zaidi kwenye kundi lao. Kesho ndiyo Simba wanatakiwa kuwaonyesha mashabiki wao kuwa hawakubahatisha kwenye mchezo ule uliopita, bali walikuwa na uwezo.

 

Kila mmoja ambaye aliutazama mchezo wa AS Vita na Al Ahly, alisema kuwa zile ndiyo timu kubwa kwenye kundi lao na nafikiri kuwa Simba sasa wana nafasi ya kuwaonyesha kuwa wao ni bora zaidi. Ushindi au sare ndiyo jambo pekee ambalo linaweza kuibeba timu hiyo leo na kuonyesha kuwa wanaweza kutimiza lengo lao la kufika robo fainali ya michuano hiyo mikubwa Afrika.

Nikiachana na hilo, nigeukie kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo kwa sasa Yanga wamecheza michezo mitano mbele ya Simba. Hii ni hali ya tofauti na sijawahi kuona ligi ambayo inakwenda ‘msombemsombe’ kama hii ya Tanzania Bara.

Ukijaribu kuangalia ligi zote, zile zilizoendelea na zinazochipukia utagundua hakuna timu yoyote ambayo imezidiwa michezo mitatu. Timu nyingi hata zile ambazo zinacheza na Simba kwenye michuano hii ya kimataifa michezo iliyozidi ni miwili au mmoja.

 

Sijui Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lina mpango gani, lakini ukitazama vizuri kuna mambo mawili yanaweza kutokea, kwanza ligi itamaliza mvuto mapema, au Simba wanaweza kuja kushtuka kuna timu imeshakuwa bingwa.

Hii ni kwa sababu kama Yanga wakishinda mchezo wao wa wikiendi hii dhidi ya Stand ina maana kuwa watakuwa wameizidi Simba kwa michezo sita na watakuwa wamewaacha kwa pointi 23.

 

Ukitazama kwenye msimamo wa ligi hiyo kuna timu tano au nne zimeshacheza michezo 20 na hazijaweza kufikia pointi hizo, kuonyesha kuwa siyo kidogo kama ambavyo Simba wanafikiri kuwa wanaweza kuzifikia kwa kuwa wana viporo.

Nafahamu kuwa wikiendi inayofuata au kabla ya wikiendi Yanga watacheza tena na hii inaweza kuwafanya Simba kuja kushtuka kwenye ligi wakiwa wameachwa pointi 30 ambazo zitakuwa hatari sana kufikiwa. Kitakachofuata wakati Simba wanapata nafasi ya kucheza ligi itakuwa ni michezo ya mfululizo, watacheza Jumatano, Jumamosi, Jumanne na Alhamisi kwa kuwa watatakiwa kumaliza msimu na wenzao.

 

Hii itawafanya wachezaji wake wachoke na hawataweza kushinda michezo yao inayofuata na mwisho itakuwa nafasi kubwa sana kwa timu nyingine mabingwa msimu huu. Jambo pekee ambalo Simba wanaweza kufanya ni kujaribu kuwaomba TFF kuwa makini na ratiba ya mechi nyingine na ikiwezekana wazuie baadhi ya michezo iliyopo kwenye ratiba, vinginevyo kuna timu itachukua ubingwa, Simba wakiwa na michezo mitano mkononi ya kucheza.

Comments are closed.