The House of Favourite Newspapers

Simba waomba ubingwa Azam

Said Ally | CHAMPIONI|  Dar es Salaam

BENCHI la ufundi la Simba chini ya kocha wake mkuu, Joseph Omog, raia wa Cameroon, limeweka wazi kwamba sasa wanaelekeza maombi yao yote kwa timu ya Azam kuweza kuwafunga wapinzani wao Yanga ili wawasafishie njia ya wao kutwaa ubingwa msimu huu.

Simba itakuwa na faida ya matokeo ya mchezo huo kati ya Yanga na Azam ambao ulipangwa kuchezwa wikiendi hii lakini utapangiwa tarehe nyingine kutokana na timu zote mbili kuwa na majukumu ya kimataifa. Katika mchezo wa awali msimu huu, timu hizo hazikufungana.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja, alisema wanaamini kwamba Azam watakuwa kizuizi kizuri kwa Yanga kuchukua pointi kwao ambapo kama wakifungwa mchezo huo, itakuwa faida kwao.

“Tunategemea kwamba Yanga watakwama watakapokutana na Azam kwa kupata matokeo mabaya ambayo kwetu itakuwa faida kwa sababu njia ya ubingwa itazidi kusafishika na hilo litakuwa jambo zuri kwetu.

“Japo hatufikirii sana matokeo ya wapinzani wetu kwa sababu tunacheza mechi zetu na lengo ni kushinda na siyo jambo lingine na tunaamini kama tutafanya vizuri kwenye mechi hizo, basi kila kitu kitakuwa kizuri kwetu,” alisema Mayanja.

Comments are closed.