The House of Favourite Newspapers

Simba Watua Kwa Tchetche

0

KLABU ya Simba imeanza harakati za kukisuka upya kikosi cha timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao wa 2020/21.

 

Uongozi wa klabu hiyo unataka kikosi chao kiwe moto wa kuotea mbali msimu ujao na tayari umeshafanya mazungumzo na nusu ya wachezaji wake inaowahitaji ambao mikataba yao ndani ya klabu hiyo inafikia tamati mwishoni mwa msimu huu.

 

Lakini pia uongozi huo unadaiwa kuwa tayari umeshafanya mazungumzo na baadhi ya wachezaji wa kimataifa kwa ajili ya kuwasajili na mmoja kati ya wachezaji hao ni aliyekuwa mshambuliaji wa Azam FC raia wa Ivory Coast, Kipre Tchetche.

 

Tchetche aliyeichezea Azam kuanzia 2011 hadi 2016 ambaye kwa sasa anaitumikia Kedah inayoshiriki Ligi Kuu ya Malaysia, anatakiwa Simba kwa ajili ya kusaidiana na Meddie Kagere na John Bocco.

 

Bocco na Tchetche wanafahamiana vizuri kwani wote walipokuwa Azam, walifanya mambo makubwa kwa kuipa timu hiyo ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2013/14 wakimaliza bila ya kupoteza mechi.

 

Habari za kuaminika ambazo Spoti Xtra limezipata kutoka ndani ya Simba zimedai kuwa, mazungumzo kati ya Tchetche ambaye alikuwa mfungaji wa kutumainiwa wa Azam na uongozi huo yameshakamilika ila kikwazo kikubwa kipo katika dau la mshahara.

 

Mmoja wa viongozi wa Kamati ya Utendaji ya Simba ambaye aliomba kutotajwa jina lake gazetini, alisema Tchetche anataka mshahara wa dola 8,000 kwa mwezi (sawa na Sh 18,320,400).

 

“Kwa hiyo, hapo ndiyo bado kuna tatizo kwani hata katika dirisha dogo la usajili lililofungwa Januari, mwaka huu alikuwa aje lakini dau hilo lilikuwa kikwazo. “Hivi sasa pia bado anahitaji kiasi hicho, kwa hiyo ngoja tusubiri tuone itakuwaje,” kilisema chanzo hicho cha habari.

 

Alipotafutwa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa ili aweze kulizungumzia hilo, hakuwa tayari kusema chochote zaidi ya kudai kuwa muda wa usajili ukifika kila kitu kitawekwa wazi.

 

Katika msimu wa 2012/13, Tchetche aliibuka mfungaji bora Bongo akifunga mabao 17 na msimu wa 2013/14, alitwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu Bara.

Leave A Reply