The House of Favourite Newspapers

Simba Yamteka Beki Mpya Wa Yanga SC

0

NI umafia juu ya umafia! Baada ya Yanga kuwazidi kete Simba kwa kumsajili Bakari Mwamnyeto, Wekundu hao wa Msimbazi wamejibu mapigo kwa kumteka beki kisiki, Ibrahim Ame ‘Varane’ na kumpa mkataba.

 

Mwamnyeto ambaye alikuwa nahodha wa Coastal Union, inaelezwa kuwa tangu mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara ulivyoanza msimu huu, alikuwa kwenye rada za Simba, lakini mwisho wa siku Simba wakamleta Dar, Yanga wakamchukua na akasaini miaka miwili.Baada ya kuona hivyo, Simba nao wamemnyakua Ame ambaye alikuwa pacha wa Mwamnyeto ndani ya Coastal Union.

Inaelezwa kuwa, Ame alikuwa kwenye hatua za mwisho kujiunga na Yanga ili akaimarisha ukuta wa timu hiyo sambamba na Mwamnyeto kama ilivyokuwa Coastal Union, lakini Simba wakaamua kulipiza kisasi.

 

Habari kutoka kwa mtu wa karibu na Ame zinaeleza kuwa, viongozi wa Yanga walimtumia nauli Jumapili beki huyo ili atue Dar asaini mkataba, lakini ghafla akapokewa na watu wa Simba, akashangaaa, wakaenda kumpa mkataba.

 

“Ame alikuwa kwenye rada za Yanga, akatumiwa kabisa nauli ili aje Dar kusaini mkataba ili aungane na Mwamnyeto, lakini Simba wakawazidi ujanja, wakamuwahi juu kwa juu na kumchukua wao.

 

“Nimezungumza na mwenyewe anasema baada ya kutua Dar, alishangaa kupokewa na watu tofauti na alioelezwa na meneja wake, akapelekwa Posta kwenye ofisi moja na kupewa mkataba wa miaka miwili akagoma kusaini hadi waongee na meneja wake.

 

“Kwanza alikuwa mwenyewe tu bila meneja wake, ikawa rahisi kwa Simba kumshawishi yeye, kisha wakamshawishi na meneja wake, dili likatiki,” alisema mtoa taarifa huyo.Spoti Xtra, lilimtafuta Ame ambaye anaichezea Timu ya Taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes ambapo alisema: “Ligi ilipomalizika nilikuwa nyumbani kwa mapumziko, Jumatatu nikaja Dar kwa ajili ya kumalizana na Simba ambao wananihitaji.

 

“Hivyo kwa sasa tupo kwenye mazungumzo na tumefikia sehemu nzuri, muda wowote kuanzia sasa tunaweza kumalizana.”Taarifa zinasema kuwa mchezaji huyo alikuwa atambulishwe na Yanga juzi Jumanne usiku, lakini ghafla wakapata taarifa kuwa ameshamalizana na Simba wakaachana naye.

Leave A Reply