The House of Favourite Newspapers

Simba yamtengea Omog milioni 350 za usajili

0

Simba-DayWachezaji wa timu ya Simba.

Wilbert Molandi na Sweetbert Lukonge
KAMATI ya Usajili ya Simba, imemtengea kocha wake Mcameroon, Joseph Omog, Sh milioni 350 kwa ajili ya usajili wa wachezaji wapya.
Timu hiyo iliyoweka kambi yake ya pamoja mkoani Morogoro, tayari imewasajili wachezaji watano pekee wazawa ambao ni Shiza Kichuya, Mohamed Ibrahim, Hamad Juma, Mzamiru Yassin, Jamal Mnyate huku ikimchukua Mwadini Ally kwa mkopo kutoka Azam FC.

IMG-20160623-WA0002Kocha Simba Mcameroon, Joseph Omog enzi akiwa Azam FC.

Wakati wakiendelea na maandalizi hayo ya msimu mpya, kocha huyo anaendelea na mchujo wa wachezaji wa kimataifa kabla ya kuwasajili kwenye msimu ujao.
Akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa Simba uliofanyika katika Bwalo la Polisi, Masaki jijini Dar jana Jumapili, Rais wa Simba, Evans Aveva, alisema kikubwa wanataka kuona wanakuwa na kikosi imara kitakachopambana na kuchukua ubingwa wa ligi kuu, hayo ndiyo malengo yao.
Aveva alisema, katika msimu uliopita timu yao ilishindwa kufikia baadhi ya malengo ikiwemo la ubingwa kutokana na usajili mbovu walioufanya kwa kusajili wachezaji wasiokuwa na vigezo vya kuichezea Simba.
Aliongeza kuwa, zoezi hilo la usajili hivi sasa wamemkabidhi Omog kwa kusaidiana na msaidizi wake Mganga, Jackson Mayanja kufanikisha usajili huo.
“Uongozi umetenga bajeti ya shilingi milioni 350 kwa ajili ya kusajili. Na jukumu hilo la usajili tumemuachia kocha wetu Omog kuhakikisha anakuwa na kikosi bora na imara kitakachopambana kutwaa taji la ubingwa.
“Hayo ndiyo malengo tunayotaka kuyatekeleza msimu ujao, ni kupambana kufa au kupona kuhakikisha tunafanikisha malengo yetu,” alisema Aveva.
Katika hatua nyingine, Simba wamepokea nyasi zao bandia ambazo tayari zipo bandarini tayari kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wao uliopo Bunju jijini Dar. Aveva alisema mara baada ya nyasi hizo kufika, uongozi wake upo kwenye hatua ya mwisho kwa ajili ya kuzitoa bandarini hapo.
Aveva alisema, mchakato huo wa ujenzi unatarajia kuanza haraka huku akitaja bajeti nzima ya ujenzi wa uwanja ikiwemo kuweka nyasi bandia kuwa ni Sh milioni 200. Aliongeza kuwa, pia uongozi wao umepanga kutengeneza hostel za wachezaji wao zitakazokuwepo uwanjani hapo kwa thamani ya Sh bilioni 3.4.

Leave A Reply