The House of Favourite Newspapers

SIMBA YASHIKILIA REKODI ZA USAJILI BONGO

SIMBA imeshikilia rekodi za usajili kwa wachezaji walioingia na kutoka kwenye Ligi Kuu Bara, pamoja na usajili wote kwa ujumla.

Kwa utafiti uliofanywa na Championi Jumatatu, imeonyesha kuwa Simba ndiyo timu iliyo na rekodi ya kusajili wachezaji kwa bei ghali zaidi na kuuza kwa bei ghali pia. Sasa ikiwa chini ya mwekezaji Mohamed Dewji ‘Mo’, timu hiyo inatarajiwa kufanya makubwa zaidi katika usajili kuanzia msimu ujao huku ikijinasibu kuwa inaweza kusajili mchezaji yeyote Afrika.

Pamoja na hivyo, ukiangalia timu zote za Bongo, Simba pia imefunika kwa kutoa wachezaji wengi zaidi waliocheza katika mataifa makubwa kisoka Afrika Kaskazini, Afrika Magharibi na Ulaya.

YASHIKILIA REKODI ZA USAJILI BONGO

Championi limejiridhisha kuwa, hakuna timu nyingine ya Bongo iliyotoa wachezaji wengi zaidi kucheza Ulaya kuliko Simba. Simba ndiyo inayoongoza.

Baadhi ya wachezaji waliotoka Simba na kucheza soka Ulaya na kwingine kwenye soka la kulipwa ni Selemani Matola (Super Sport-Afrika Kusini), Haruna Moshi ‘Boban’ (Gefle IF-Sweden), Athuman Machupa (Sweden), Renatus Njohole (Yverdon Sports- Uswisi), Shekhan Rashid (Sweden) na Mohamed Mwameja (Marekani).

Ukiachana na hao, katika rekodi za usajili, Simba imeibuka kidedea ikitoa fedha nyingi kununua, pia ikipokea fedha nyingi kuuza.

Hii ni orodha wa wachezaji waliovunja rekodi ya usajili Ligi Kuu Bara.

EMMANUEL OKWI –SH MILIONI 600

Huyu ndiye anayeshikilia rekodi ya usajili Bongo, baada ya kuuzwa na Simba katika Klabu ya Etoile du Sahel ya nchini Misri msimu wa 2015/2016 kwa dola 300,000 (zaidi ya shilingi milioni 600). Huyu ni mchezaji ghali zaidi aliyewahi kucheza ligi kuu.

Msimu huu pia aliweka rekodi baada ya Simba kumwaga Sh milioni 115 na kumchukua kutokea SC Villa ya Uganda.

MBWANA SAMATTA- SH MIL 340

Hivi sasa anakipiga katika Klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji, anafuatia akiwa ameiingizia Simba dola 150,000 ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 340, ilipomuuza katika Klabu ya TP Mazembe ya DR Congo mwaka 2011.

SIMON MSUVA – SH MIL 340

Aliuzwa kutoka Yanga kwenda Difaa El Jadida ya Morocco kwa dola 150,000 (zaidi ya shilingi milioni 340) msimu wa 2016/2017. Alijiunga na Jadida bila kufanya majaribio tofauti na kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Ramadhani Singano ‘Messi’ ambaye alikwenda kwenye majaribio lakini hakufanikiwa kufuzu.

OBREY CHIRWA –SH MILIONI 200

Hivi sasa anaomba kurejea kwenye klabu yake ya zamani ya Yanga, yeye alitua Jangwani kwa shilingi milioni 200 akitokea FC Platinum ya Zimbabwe mwaka 2016 kama mchezaji huru.

DONALD NGOMA –SH MILIONI 200

Donald Ngoma ni kati ya washambuliaji waliotengeza mkwanja mrefu mwaka 2017 baada ya Yanga kumuongezea mkataba wake wa miaka miwili uliomalizika kwa kitita cha Sh milioni 200.

Mwaka 2016, mshambuliaji huyo alisajiliwa kwa Sh milioni 100 akitokea FC Platinum ya Zimbabwe na kujiunga na Yanga.

MRISHO NGASSA – SH MILIONI 160

Alijiunga na Free State ya Afrika Kusini mwaka 2016 kwa dau la Sh milioni 160 kama mchezaji huru baada ya mkataba wake kumalizika Yanga.

SHOMARY KAPOMBE – SH MILIONI 150

Simba iliingiza kitita cha Sh milioni 150 baada ya kumuuza Kapombe AS Cranes ya Ufaransa mwaka 2013 kabla ya kurejea nchini na kujiunga na Azam FC. Hivi sasa yupo Simba.

MEDDIE KAGERE – SH MILIONI 120

Ni mchezaji aliyevunja rekodi ya usajili kwenye msimu huu wa ligi 2018/2019 akitokea Gor Mahia ya Kenya na kuja Simba.

HARUNA NIYONZIMA – SH MILIONI 115

Anamalizia mkataba wake wa mwaka mmoja. Haruna Niyonzima alijiunga na Simba msimu uliopita akitokea Yanga kwa dau la shilingi milioni 115.

KIPRE TCHETCHE NA PASCAL WAWA – SH MILIONI 100

Tchetche alikunja dola 50,000 (zaidi ya Sh milioni 100) akitokea nyumbani kwao alipokuwa anacheza soka. Ni kati ya usajili bora uliowahi kufanywa na Azam. Ilikuwa ni msimu wa 2011/2012. Dau hilo, pia alipewa beki wa kati Pascal Wawa katika usajili wa msimu huo akitokea El Merreikh ya Sudan.

Waliokunja mkwanja wa chini ya Sh milioni 100 ni Thabani Kamusoko Sh milioni 90 kutoka FC Platinum kwenda Yanga (2015), Jonas Mkude aliyeongeza mkataba kwa Sh milioni 80 Simba msimu huu, Kelvin Yondani aliongeza mkataba Yanga Sh milioni 70 msimu huu.

Wengine ni Clatous Chama zaidi ya Sh milioni 70 kutoka Power Dynamo ya Zambia kwenda Simba (2018), Tafazwa Kutinyu shilingi milioni 70 kutoka Singida United kwenda Azam (2018) na Frank Domayo alichota Sh milioni 70 kutokea Yanga kwenda Azam (2014).

Wilbert Molandi na Sweetbert Lukonge

Comments are closed.