Simba Yatinga Raundi Pili, Kuwavaa Fc Platinum

LICHA ya kubanwa mbavu nyumbani, lakini imekuwa faida kubwa kwa Simba na kusonga hatua ya kwanza ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

 

Jana Desemba 5, Simba ikiwa Uwanja wa Mkapa jijini Dar, ilishindwa kufungana na Plateau United ukiwa ni mchezo wa marudiano wa michuano hiyo na kuifanya Simba kusonga hatua inayofuata kwa faida ya bao la ugenini.

Kusonga mbele kwa Simba, kumewaibua mashabiki wa timu hiyo wakiwaambia wapinzani wao, Yanga kwamba: “Si mliwaleta Plateau, mkawapokea vizuri pale uwanja wa ndege, sasa waleteni wengine, sisi tumesonga mbele.”

Katika mchezo wa kwanza uliochezwa wikiendi iliyopita nchini Nigeria, Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Clatous Chama ambapo bao hilo limekuwa na faida kubwa kwao baada ya jana kupata matokeo ya  0-0.

Kwenye mchezo wa jana,Simba inabidi wajilaumu wenyewe kwa kushindwa kupata mabao kwa kuwa walitengeneza kona 12 ambazo hazikuweza kuleta matunda.

 

Kiungo wa Simba, Luis Miquissone, alifanya jaribio moja kali ndani ya 18 dakika ya 74 likiwa ni jaribio la pili ambapo la kwanza lilipigwa na Hassan Dilunga dakika ya 60 liliokolewa na kipa wa Plateau United, Adam Abulari.

 

Mara ya mwisho Simba kufungwa nyumbani katika michuano ya CAF ilikuwa mwaka 2013 katika Ligi ya Mabingwa Afrika walipocheza dhidi ya Recreativo do Libolo ya Msumbiji, wakifungwa 1-0.

STORI na SAID ALLY

 


Msimu wa 2018, Simba ilishiriki Kombe la Shirikisho Afrika, ikiwa ni baada ya kukosekana kwenye michuano ya kimataifa kwa takribani misimu minne.

Simba walianzia hatua ya awali kwa kukutana na Gendarmerie Nationale ya Djibouti, nyumbani ikashinda
4-0, ugenini ikashinda 1-0.

Hatua ya pili ikakutana na timu ya Al Masry kutoka nchini Misri hapa nyumbani ilikuwa 2-2. Ugenini wakatoka 0-0. Bao la ugenini likaihukumu.

 

Simba hatua ya kwanza inakwenda kukutana na FC Platinum ya Zimbabwe anayocheza Mtanzania, Elius Maguri, timu hiyo iliiondosha Costa do Sol ya Msumbiji kwa jumla ya mabao 4-1.

Toa comment