The House of Favourite Newspapers

Yanga Dhidi ya Ruvu,Inasakwa Rekodi

0

KATIKA Dimba la Mkapa kuanzia saa 1:00 usiku leo Jumapili, kuna mechi ya Ligi Kuu Bara kati ya Yanga na Ruvu Shooting ambapo mechi hiyo kuna rekodi inasakwa.

 

Ikiwa nafasi ya kwanza na pointi 31, Yanga inakutana na Ruvu Shooting yenye pointi 23 zote zimecheza mechi 13.
Tangu msimu wa 2010/11,timu hizo zimekutana mara 18, Yanga imeshinda 13 na Ruvu Shooting ikishinda moja, huku
zikipatikana sare nne.

 

Akizungumza na Spoti Xtra, Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli, alisema kuwa kila kitu kipo sawa ni jambo la
kusubiri wakati “Mwalimu amekiandaa kikosi chake na kipo sawasawa kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya Ruvu Shooting,  tunaamini kwamba utakuwa na ushindani mkubwa na wachezaji wote,wapo tayari kwa ajili ya mchezo
wetu.

 

“Kikubwa mashabiki wajitokeze kwa wingi uwanjani kuipa sapoti timu yao kwani lengo letu ni kuona kwamba tunafikia malengo ambayo tumejiwekea ya kutwaa ubingwa,” alisema.

 

Naye Ofisa Habari wa Ruvu Shooting, Masau Bwire, amesema kuwa kitakachowaponza Yanga kwenye mchezo wao wa leo ni uwepo wa Kocha Charles Boniface Mkwasa kwenye benchi la timu yao ambaye anaijua vizuri Yanga.

 

“Yaani hao Yanga hata sijui wanaponea wapi? Kwa sababu ukiachilia mbali soka letu kubwa na la kutisha tunalocheza, tunaye kocha Mkwasa Master, ambaye yule ile Yanga yote ipo kwenye mkono mwake, anaijua vizuri sana, sasa najaribu tu kuwaza watatokaje.

 

REKODI INAYOSAKWA Unaambiwa kama Yanga wakiibuka na ushindi wowote leo, timu hiyo itakuwa inazidi kuweka rekodi za aina yake, ushindi kwa Yanga  utawafanya kuweka rekodi ya kucheza michezo 27 bila kupoteza.

 

 

Yanga kwa sasa imefikisha idadi ya michezo 26 mfululizo bila kupoteza kuanzia Machi 15, 2020, Yanga bado inaifukuzia rekodi ya Simba ambayo waliiweka ya kucheza mechi 33 bila kupoteza kutoka Aprili 10, 2017 hadi Mei 12, 2018.

WAANDISHI: SAID ALLY, ISSA LIPONDA NA
MARCO MZUMBE

 

Leave A Reply