The House of Favourite Newspapers

Simbu Aeleza Alivyovunja Rekodi Yake ya Olimpiki

0
Mwanariadha wa Tanzania, Alphonce Felix Simbu akiwa na tuzo yake baada ya kutua nchini.

MAKALA: IBRAHIMU MUSSA | CHAMPIONI JUMATANO | HABARI

MWANARIADHA wa Tanzania, Alphonce Felix Simbu, wikiendi iliyopita alifanikiwa kushika nafasi ya tano na kutengeneza rekodi mpya katika mbio za London Marathon baada ya kukimbia kwa muda wa saa 02:O9:10.

Muda huo ni tofauti ya 00:02:05 na ule alioutumia katika mashindano ya Olimpiki yaliyofanyika Rio de Janeiro nchini Brazil, mwaka jana ambapo alishika nafasi kama hiyo.

Alphonce Felix Simbu alishika nafasi ya tano katika mashindano ya Virgin Money London Marathon.

Katika Olimpiki alitumia muda wa saa 02:11:15.
Mapema mwaka huu, Simbu alifanikiwa kuibuka mshindi wa mashindano ya Standard Chartered Mumbai Marathon baada ya kutumia saa 02:09:32 ambapo alizawadiwa Dola za Kimarekani 42,000, sawa na Sh milioni 91.
Katika mashindano ya London Marathon, wikiendi iliyopita, nafasi ya kwanza ilichukuliwa na Mkenya Daniel Wanjiru aliyekimbia kwa muda wa saa 02:05:48, ya pili Muethiopia, Kennisa Bekele (02:05:57), huku nafasi ya tatu na ya nne zikienda kwa Wakenya, Bedan Karoki (02:07:41) na Abel Kirui (02:09:10).

Mwanariadha, Alphonce Simbu akimaliza katika mashindano ya  Olimpiki mwaka  jana katika jiji la Rio de Janeiro, Brazil  ambapo alishika nafasi ya tano.

Championi limefanikiwa kufanya mazungumzo maalum na mwanariadha huyo moja kwa moja kutoka London, England, na kufunguka jinsi mashindano hayo yalivyokuwa:
“Kwanza namshukuru Mungu kwa kukimbia na kumaliza salama, unapomaliza salama ni jambo la kumshukuru Mungu kwa sababu siyo wote ambao walimaliza, wengine waliishia njiani.

Alphonce Simbu akifanya yake kwa kushika nafasi ya kwanza Mumbai Marathon 2017, India (katikati).

“Haya ni mashindano makubwa duniani pamoja na Berlin Marathon, Tokyo Marathon, New York Marathon, Boston Marathon ambayo yote yanatambulika kama mashindano makubwa kwani yanakuwa na wakimbiaji waliokimbia muda mrefu halafu wazoefu.

Unazungumziaje rekodi yako mpya?
“Kiukweli kwangu ni kitu kizuri ambacho kinaonyesha namna nilivyofanya kazi kubwa kwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine tofauti na ile rekodi ya kwanza katika mashindano ya Olimpiki kule Brazil.

Kuna taarifa za kupata udhamini kutoka Adidas, unalizungumziaje hilo?
“Ni kweli nimepata mkataba wa udhamini kutoka katika Kampuni ya Adidas na ndani ya mkataba huo nitakuwa napata vifaa vya mazoezi na pesa ambazo bado hatujafikia katika makubaliano mazuri, lakini vifaa nimeshaanza kupata.
“Nadhani mambo mengi yatakuwa wazi yakishakamilika, kwa sasa bado mapema sana ila kitu kizuri ni kwamba kila kitu kitakuwa sawa, ni jambo la kuendelea kuomba Mungu tu.

Unazungumziaje safari yako ya London kutaka kukwama?
“Kiukweli safari ilikuwa ngumu kwa sababu tulihangaika sana Dar es Salaam karibia wiki moja kutafuta ‘visa’ na hili lilitokana na utaratibu wa kuilipia kubadilika kwani malipo yanafanyika kwa njia ya benki.
“Tulijaribu kutuma akaunti namba zetu za benki zikawa zinakataa, tukapewa saa 24 lakini bado ilishindikana pia tukawaambia Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) na wao wakawasiliana na Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo ambao walitusaidia kuandika barua kwa Balozi wa Uingereza.


“Lakini ubalozi ulisema muda umeisha ila wao wakatutumia mawasiliano ya watu wa Afrika Kusini, hata hivyo waandaaji wa mbio hizo nao wakawasiliana na watu wa Afrika Kusini ambapo nikaanza safari tena ya kuelekea huko kukamilisha.
“Kiukweli ilikuwa ngumu na ilibaki kidogo nisije huku lakini nawashukuru wote ikiwemo Serikali ya Tanzania kwa jitihada walizozifanya mpaka nimefika kutokana na changamoto zilizojitokeza.

Umejipanga vipi kwa mbio za mabingwa wa dunia ambazo zitafanyika hapo London?
“Nadhani jukumu kubwa litakuwa ni la shirikisho na maandalizi yanatakiwa yafanywe na wao na wanatakiwa wajipange kwani katika mbio hizi jukumu lilikuwa ni kwangu lakini nawashukuru Multichoice kupitia DSTV kwa sababu waliniwezesha kukaa kambi pamoja na wenzangu kadhaa.


“Kitu kizuri ni kwamba kambi ile imeleta matunda maana kuna mwenzangu juzi alikimbia Humburg, Ujerumani na amefanikiwa kuweka rekodi nzuri ya muda ambao umemuwezesha kwenda kwenye mashindano ya dunia licha ya changamoto za hapa na pale.

Ni kweli umejiunga na jeshi?
“Ndiyo, sasa hivi nipo chini ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), nawashukuru kwamba wamenipa ushirikiano mkubwa sasa kuhakikisha nashiriki mbio hizi, mwaka jana nilipokwenda kufanya usaili niliwaeleza kuhusu haya mashindano ninayoshiriki.
“Sasa hivi nimehamishiwa Mkuyuni kutoka katika Kambi ya JKT Oljoro na hata kuja kwangu huku nimepata ruhusa kutoka kwao ambao wao walipeleka maombi yangu kwenda nje katika ofisi ya rais.

Unawaambia nini Watanzania?
“Kikubwa hata wao wenyewe wanajua mchezo umeshuka lakini kitu kizuri kwetu ni kushirikiana na kuweza kufufua juhudi ambazo zimeendelea kufanyika chini ya viongozi wa riadha.
“Viongozi wamekuwa wakijituma na imani yangu tuna uwezo wa kufanya vizuri kwa mashindano yajayo na kuweza kuchukua medali za dhahabu.

Ushindani wa Wakenya na Waethiopia unauonaje?
“Unajua katika kila jambo kuna watu huwa na uzoefu zaidi kutokana na kulifanya jambo hilo kwa muda mrefu sana, sasa ukiwaangalia wakongwe wa Kenya na Ethiopia ni watu ambao wamekimbia mbio nyingi.
“Wana uzoefu wa kutosha, wanajua mbinu nyingi, kwa hiyo kwa watu kama sisi ambao tunakuja kwenye mashindano haya makubwa ndiyo tunajifunza jinsi gani ya kupambana nao,” anasema Simbu.

Leave A Reply