The House of Favourite Newspapers

SIMULIZI MAMA ALIYEMWAGIWA TINDIKALI INASIKITISHA

AADHIMISHO ya siku kumi na sita za kupinga ukatili wa kijinsia na walemavu mkoani Mbeya yameendelea kwa kuwatembelea na kutoa msaada wa chakula, mavazi na pesa kwa baadhi ya watu waliofanyiwa ukatili mkoani hapa.  

 

Moja ya watu waliofanyiwa ukatili ni mwanamke aliyejulikana kwa jina la Vumilia Sankemwa (32) na mwanaye Loveness Peter (13), wakazi wa Mama John, Kata ya Ilomba jijini Mbeya ambapo mama huyo alisimulia simulizi ya tukio ambayo inasikitisha.

 

Mkuu wa Dawati la Jinsia Mkoa wa Mbeya, Mary Gumbo akiwa na jopo la askari wa Dawati walimtembelea Vumilia na mwanaye na kuwapa faraja ikiwemo kuwapa msaada wa chakula. Licha ya kutoa msaada huo pamoja na ujasiri wao wa kiaskari walishindwa kujizuia baada ya kusimuliwa kadhia iliyoikuta familia hiyo.

 

“Ndugu zangu kwanza nawashukuru kuja kutuona na kutupatia msaada huu, mimi nilimwagiwa tindikali mwaka 2017 nikiwa na wanangu wawili mmoja ni huyu mnayemuona hapa ambapo katika tukio hilo mimi nimepofuka macho yote kama mnavyoniona hapa pia kupata majeraha katika mwili na mwanangu Loveness alipata majeraha pia,” alisema Vumilia huku akibubujikwa na machozi na kuongeza:

“Baada ya kupatiwa matibabu ya awali nilishauriwa kwenda kupata matibabu zaidi Hospitali ya KCMC Moshi ambapo baada ya matibabu nikiwa narejea basi lilipata ajali na kutekeketea kwa moto pamoja na dawa zote nilizopewa Moshi hivyo mpaka sasa nimekwama matibabu na sina pesa za kurudi hospitali.”

 

Kwa upande wa mwanaye Loveness, mama huyo alisema alipata majeraha kichwani lakini anamshukuru Mungu kwa kupona hatimaye kufanikiwa kumaliza elimu ya msingi mwaka huu. Loveness katika matokeo ya shule ya msingi amefaulu kuendelea na masomo ya sekondari lakini hana uhakika wa kutimiza ndoto yake kwani hana mtu wa kumnunulia sare na mahitaji ya shule kama madaftari kwa kuwa baba yake alifariki na mama yake kwa sasa ni kipofu.

 

Familia hiyo imeomba wadau kujitokeza kuwasaidia chakula pia mahitaji ya shule ili mtoto huyo asome aweze kumtunza mama yake ambaye kwa sasa ni kipofu. Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na jeshi la polisi, tukio la mama huyo na mwanaye kumwagiwa tindikali liliwapata wakiwa wanatokea dukani kununua bidhaa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.

Inasemekana wakati wakiwa njiani waliweza kukutana na mama mmoja aliyefahamika kwa jina la Emmy Kyando (40), mkazi wa Sae mkoani humo ambaye inadaiwa kuwa ni mke mwenza wa muhanga wa tukio hilo na mara baada ya kuonana naye aliwamwagia kimiminika hicho katika sehemu mbalimbali katika miili yao na baada ya hapo waliweza kupata msaada toka kwa wasamaria wema kwa kupelekwa Hospitali ya Rufaa Mbeya kwa matibabu.

 

Maadhimisho ya kupinga ukatili wa kijinsia na walemavu yalizinduliwa katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Usharika wa Forest yaliyoratibiwa na Mwenyekiti wa Askari Wanawake Mkoa wa Mbeya, Debora Lukololo. Uzinduzi huo uliambatana na ibada maalumu ya maombi kwa askari wa majeshi yote.

Madee Afunguka Babu Tale Kuwatosa TIP TOP Wasafi Festival

Comments are closed.