The House of Favourite Newspapers

Simulizi ya AY: Aeleza alivyowaunganisha Vivian na Complex

0

Ambwene-Yesaya-21Wiki iliyopita tuliishia pale AY alipoamua kuukubali ukweli juu ya kifo cha baba na mama yake na kuamua kuendelea na maisha ya kawaida huku akiendelea kuwaombea wazazi wake huko waliko.

Leo AY mbali na kuwakumbuka wazazi wake, anajaribu pia kuwakumbuka rafiki zake ambao walitangulia mbele za haki, ingawa wiki iliyopita aliwazungumzia kwa ufupi, hawa ni marehemu Saimon Sayi ‘Complex’ aliyekuwa mtayarishaji wa muziki katika Studio za Aigies baadaye kuhamia Studio za Backyard pamoja na Mtangazaji wa Radio Clouds FM, Vivian Tillya.

Songa naye…

“Kiukweli urafiki wangu na marehemu Complex ulikuwa mkubwa sana na mara baada ya kufahamiana na kufanya remix ya wimbo wangu wa Raha Tu basi ukaongezeka maradufu.

“Naweza kusema kuwa urafiki wangu na Vivian pamoja na Complex ndiyo uliosababisha kuzaliwa kwa penzi la wawili hao, kwani mimi nilianza kufahamiana na marehemu Vivian kabla ya Complex, wakati huo Vivian alikuwa anasoma Shule ya Sekondari Mkwawa mimi nikiwa nasoma  Shule ya Sekondari ya Ufundi ya Ifunda huko ndipo tulipoanza kufahamiana na baadaye nilikutana naye jijini Arusha maeneo ya Njiro mwanzoni mwa mwaka 2000.

“Kwa muonekano wake na vile alivyokuwa nilimshawishi aingie redioni kama mtangazaji na kwa kuwa nilikuwa karibu na mtangazaji nguli kipindi hicho, Gardner G Habash basi nikafanya jitihada za kuwakutanisha pamoja na hatimaye Vivian alifanikiwa kujiunga na Clouds Media kama mtangazaji.

“Baada ya kuwa nao kama marafiki ndipo wakajikuta wakianzisha uhusiano ambao baadaye ulizaa penzi zito kwa wao na ikafika sehemu ikawa wazi kila mtu anafahamu. Mwenyezi Mungu awalaze mahali pema peponi rafiki zangu, niliwapenda ila Mungu aliwapenda zaidi.

“Nakumbuka pia kutokana na urafiki wangu na marehemu Complex kuna kipindi niliwahi kutolewa kwenye gazeti moja (jina kapuni),  kuwa nina uhusiano na Vivian, nina amini walikuwa wamedhamiria kumuandika Complex wakanichanganya naye.

“Tukio ambalo nalo siwezi kulisahau maishani mwangu lilikuwa ni la Agosti, 2005 ambapo Vivian na Complex walipata ajali na kufariki kwa pamoja, ajali hiyo ilitokea maeneo ya Mbwewe wakati huo wakitokea mkoani Morogoro kwenye Fiesta iliyokuwa inajulikana kama ‘Moto Zaidi’  wakielekea jijini Arusha kwenye sherehe ya miaka 25 ya ndoa ya wazazi wake Vivian wakati huo pia Complex alikuwa anaenda kumtambulisha Vivian.

“Ni pigo moja kubwa sana kwenye tasnia kwani walikuwa ni watu waliopendwa sana na wasikilizaji wao ila Mungu aliwapenda zaidi. Kwa kuwa Mungu alituumba kusahau maumivu, nikasahau ila moyoni nawakumbuka sana na nitaendelea kuwakumbuka daima. “Mwaka 2005 nilifanikiwa kutoa albamu yangu ya pili iliyoitwa Hisia Zangu na moja ya wimbo uliobamba zaidi ni Yule ambao ulishika chati mbalimbali katika vituo vya redio na televisheni vya Afrika Mashariki.

“Kwenye albamu hiyo nilifanikiwa kushirikiana na wasanii wakubwa wa Afrika Mashariki akiwemo Prezzo, Deux Vultures (Kenya), Maurice Kirya (Uganda) na wimbo huo kunitambulisha vema Afrika Mashariki. Kwani baada ya wimbo wa Yule niliachia mwingine wa pili wa Binadamu nikiwa nimemshirikisha Maurice Kirya toka Uganda na wimbo huo ulikuwa ni hit kubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki kiasi cha kuteuliwa kushiriki katika Tuzo za Kora, kwa mara ya kwanza nikiwa ni msanii wa kiume kushirikia tuzo hizo kutoka Tanzania.”

Usikose wiki ijayo kujua nini kilifuatia baada ya yeye kuchaguliwa na kuwa msanii pekee wa kiume kushiriki tuzo hizo.

Leave A Reply