The House of Favourite Newspapers

Simulizi ya Filamu ya Titanic-02

0
Baadhi ya vipande vya filamu ya Titanic

ILIPOISHIA

“Zimeni kamera,” alisema Brock huku akionekana kuwa na hasira.

Ilikuwa ni lazima kuangalia karatasi zile zilikuwa na nini.  Wakazipeleka katika vyombo maalum na kuanza kuzisafisha, baadaye wakagundua kwamba karatasi moja ilichorwa picha nzuri ya mwanamke aliyekuwa amelala kwenye kochi huku akiwa uchi wa mnyama, na shingoni alikuwa na mkufu wenye madini ya thamani.

SONGA NAYO

Kila mmoja alishangaa, wakati hu Brock alikuwa akiongea kwa simu, alipoiona picha ile ikabidi aache kuzungumza kwa simu na mtu mwingine na kuikodolea macho picha ile.

“Hebu niione,” alisema Brock huku akisogea kwa karibu.

“Hapa tutakuwa tumepata kitu bosi,” alisema jamaa mmoja aliyekuwa akiisafisha karatasi ile iliyochorwa picha.

Brock akaichukua picha ile na kuaingalia huku akiwa kwenye mshangao mkubwa. Alishangazwa kwani ule mkufu aliyokuwa akiiona kwenye mchoro ule wa mwanamke, kulikuwa na picha iliyopigwa kwa kamera ambayo ilionyesha cheni ileile.

“Ile picha yenye cheni ipo wapi?” aliuliza Brock.

Brock akaichukua picha ile na kuanza kuangalia mkufu ule. Akawa na kazi ya kuangalia mchoro na picha. Ulikuwa mkufu uleule aliouvaa mwanamke yule aliyechorwa. Katika ile picha kwa chini ilichorwa tarehe ya siku iliyochrwa, ilikuwa ni tarehe 14/04/1912, siku moja kabla ya meli hiyo kuzama.

“Inashangaza” alisema Brock huku akiwa haamini alichokuwa akikiangalia.

***

Filamu inahama kutoka katika meli ile na kuhamia upande wa pili. Ni nyumbani, mwanamke mmoja mzee amekaa sehemu akitengeneza chungu chake. Televisheni imewaka, mtangazaji anasikika akimsifia mtu anayeitwa Brock ambaye kipindi cha nyuma aligundua dhahabu ya Hispania. Jamaa amejizolea umaarufu na siku hiyo alikuwa na habari nyingine kabisa.

Bibi yupo bize na chungu chake lakini masikio yake yanafanya kazi ya kusikiliza kilichokuwa kikitangazwa kwenye televisheni. Brock anasema kwamba wamefanikiwa kuifuatilia Titanic iliyokuwa imezama baharini, walikwenda mpaka chini kabisa meli hiyo ilipokuwa.

Bibi anaposikia hivyo, anashtuka, anaacha kazi yake na kwenda kuangalia televisheni ile. Mjukuu wake, Lizzy anashangaa, anamsogelea bibi yake.

“Kuna nini?” aliuliza.

“Hebu ongeza sauti,” alisema bibi huku akiiangalia televisheni ile.

Brock anaelezea jinsi walivyozama chini ya maji kwenye meli ile na kukuta baadhi ya vitu ukiwemo mchoro ule. Bibi anapouona anashtuka mno, ni yeye, alichorwa miaka 84 iliyopita.

***

Kazi inaendelea katika meli ya Brock, anaendelea kufuatilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea. Kuna mashine inatengenezwa tayari kwa kutupwa tena baharini kwani kuna kazi kubwa pia ilitaka kufanyika. Wakati akiwa bize, ghafla mfanyakazi wake, Bobby anamkimbilia pale alipokuwa na kumuita, anageuka, Bobby amemfikia na kuanza kuongea naye.

“Brock, kuna simu yako,” alisema jamaa huyo. Brock anamwangalia usoni, mtazamo ulioonyesha kumuuliza haoni kama kazi aliyokuwa akiifanya ilikuwa muhimu sana.

“Bobby huoni kuna kazi inaendelea ya kulizindua hili nyambizi kwa kuliingiza ndani ya maji?” aliuliza Brock huku akimshangaa Boby.

“Niamini! Hii simu ni muhimu sana kuipokea,” alisema Bobby.

Brock alivyoambiwa hivyo, akaona hakuna jinsi, kama aliambiwa kuwa simu hiyo ilikuwa muhimu sana, akaamua kwenda huko na kuzungumza na huyo mtu aliyempigia simu.

“Ila utabidi kuongea kwa sauti kwa kuwa ni mzee sana,” alisema Bobby.

“Sawa.”

Brock akachukua simu ile na kuanza kuongea, kwanza akajitambulisha na kukata kumfahamu mtu aliyepiga. Hapohapo Bobby akamwambia kwamba jina lake aliitwa Rose Calvert.

“Mrs Calvert..” aliita Brock.

“Nimeshangazwa kuona tayari mmeupata moyo wa bahari, Mr. Lovett,” alisema bibi Rose kwenye simu huku pembeni akiwepo mjukuu wake. Alipoambiwa hivyo, Brock akashtuka, alijua mwanamke huyo alimaanisha nini. Hapohapo akayageuza macho yake na kumwangalia Bobby.

“Nilikwambia kwamba hii simu ni muhimu sana bosi,” alisema Bobby.

“Sawa! Nakusikiliza Rose. Unaweza kutuambia yule mwanamke wa kwenye mchoro ni nani?”

“Ooh! Ndiyo! Mwanamke wa kwenye ule mchoro ni mimi!” alijibu bibi Rose na kuachia tabasamu pana.

***

Brock alizungumza naye na kuhitaji kuonana naye. Ilibidi helkopta itumwe kwenda kumchukua yeye na mjukuu wake kule walipokuwa. Si kila mtu alikuwa akiamini kama kweli bibi Rose alikuwa akizungumza ukweli, wengine walihisi kwamba alikuwa akidanganya kwa ajili ya kupata umaarufu au pesa. Mtu wa kwanza kufikiri hivyo alikuwa Lewis.

“Huyu mwanamke ni muongo. Anatafuta pesa tu na kujulikana. Ni Mungu pekee ndiye anayejua kwa nini! Ni kama yule mwanamke wa Kirusi, Anesthesia” alisema Lewis, alikuwa akizungumza hayo huku akimwangalia Brock.

“Wanakuja,” alisema Booby na kuwaonyeshea helkopta ambayo haikuwa mbali kutoka pale meli yao ilipokuwa.

“Rose Dewitt Bukater alikufa katika meli ya Titanic alipokuwa na miaka 17, si ndiyo?” alisema Lewis na kuuliza.

“Ndiyo!”

“Kwa hiyo kama atakuwa hai bila shaka atakuwa na miaka zaidi ya mia moja,” alisema Lewis.

“Miaka 101 mwezi ujao,” alisema Brock.

“Basi sawa. Tuseme yeye ni bibi muongo,” alisema Lewis na kuongezea:

“Unajua nimekwishafanya uchunguzi kuhusu mwanamke huyu kuhusu maisha yake ya nyuma, alipokuwa na miaka 20 alikuwa muigizaji. Aliitwa kama Rose Dawson ambaye baadaye aliolewa na mtu aliyeitwa Calvert. Wakahamia Cedar Rapids na kupata watoto kadhaa. Baadaye Calvert akafariki na Cedar Rapids kupotea kabisa,” alisema Lewis kwa sauti kubwa kwani helkopta ndiyo ilikuwa ikitua.

“Kila mtu anajua kuhusu almasi, ilitakiwa kupotea lakini huyu atakuwa anajua kila kitu,” alisema Brock.

Helkopta ikatua, watu wengine wakaanza kuteremsha mizigo yake. Bibi Rose akateremshwa akiwa kwenye kiti chake cha magurudumu na Brock kujitambulisha kwa mwanamke huyo. Akamkaribisha Lizzy ambaye ndiye alikuwa mjukuu wa mwanamke huyo.

Akaribishwa, wakapewa chumba na kuanza kupanga vitu vyao chumbani humo zikiwemo picha nyingi alizokuwa amepiga miaka hiyo ya nyuma. Akamtambulisha mjukuu wake aliyeitwa Lizzy, wakazungumza kidogo.

“Naweza kuwasaidia kitu chochote kile?” aliuliza Brock.

“Ndiyo! Ningependa kuuona mchoro wangu,” alisema Bibi Rose.

Akachukuliwa na kupelekwa katika chumba kilichokuwa na mchoro huo ambao ulikuwa ndani ya maji na kuonyeshewa. Alipouangalia, akayafumba macho yake na kuanza kukumbuka mbali, siku ambayo alichorwa picha ile na mpenzi wake.

“Louis wa 16 alivaa cheni ya almasi iliyoitwa Taji la Bluu la Almasi. Ilipotea mwaka 1792. Katika kipindi hichohicho Louis alipoteza kila kitu. Kumbukumbu zinasema kwamba hata hii almasi ilichongwa na kujulikana kama Moyo wa Bahari. Leo ina thamani hata zaidi ya almasi maarufu iitwayo Tumaini,” alisema Brock.

“Hicho kilikuwa kitu cha thamani na pekee nilichovaa shingoni mwangu. Niliivaa mara moja tu,” alisema Bibi Rose.

“Unahisi huyu ni wewe bibi?” aliuliza Lizzy.

“Ndiyo! Ni mimi! Unahisi sikuwa mtanashati?”

“Nina furaha kukutana na mtu ambaye anaweza kutuambia kila kitu kilichotokea. Unaweza kutuambia hii ilikuwa ni ya nani?” aliuliza Brock.

“Naweza kumkisia mtu mmoja aliyeitwa kwa jina la Hockley!”

“Nathan Hockley! Ni sawa, alikuwa akiishi jiji Pittsburgh. Inajulikana kwamba hii cheni ya almasi alimnunulia mtoto wake, Caledon wiki moja kabla ya kusafiri na Titanic kwa ajili ya mchumba wake, wewe. Meli ilizama, ilimaanisha kwamba hata meli hii cheni nayo ilizama pamoja na meli. Unaona tarehe?” aliuliza Brock na kuwaonyeshea tarehe iliyoandikwa katika mchoro ule.

“14/04/1912,” alisema Lizzy.

“Hii inamaanisha kwamba kama bibi yako anasema kuwa mwanamke yule ni yeye basi atakuwa ameivaa ile cheni siku ambayo Titanic ilizama,” alisema Lewis.

“Na hiyo inakufanya wewe kuwa rafiki wangu wa karibu,” alisema Brock huku akimwangalia Bibi Rose. Hapohapo akaanza kumuonyeshea vitu vingi ambavyo walivichukua kutoka katika chumba alichokuwemo ndani ya meli ile.

“Hivi ni baadhi ya vitu tulivyovikuta ndani ya chumba chako.”

“Hiki kilikuwa changu, ni kitu cha thamani. Kinaonekana kama vile kilivyokuwa siku ya mwisho nilipokiona,” alisema Bibi Rose na kujiangalia.

“Taswira yangu imebadilika sana,” alisema Bi Rose baada ya kujiangalia jinsi alivyozeeka.

“Upo tayari kurudi katika meli ya Titanic?’ aliuliza Brock, Bibi Rose akakubali kwa kutingisha kichwa.

Lewis akaanza kumwambia jinsi meli ilivyogonga mwamba wa barafu na baadaye kuanza kuzama. Bibi Rose alikuwa kimya akimsikiliza, alipomaliza akamwambia kwamba pamoja na maelezo yake, lakini kulikuwa na utofauti.

“Unaweza kutuambia,” alisema Brock huku akimwangalia Bibi Rose.

Bibi Rose akasimama na kuanza kuelekea katika televisheni moja ambayo ilichukua picha kutoka katika meli ile iliyokuwa baharini na kuanza kuangalia mazingira ndani ya meli hiyo. Sura yake ilikuwa na huzuni nzito, alikuwa akiangalia huku watu wengine waliokuwa mahali pale wakimwangalia kwa makini kabisa. Ghafla akaanza kulia kwani kumbukumbu ya kile kilichotokea nyuma kilionekana kumuumiza mno. Hapohapo Lizzy akamfuata.

“Naomba nimpeleke akapumzike,” alisema Lizzy.

“Hapana!” alisema Bibi Rose.

“Unahitaji kupumzika!”

“Hapana!” alisema Bibi Rose na kukaa chini. Hapohapo Brock akaomba kiredio cha kurekodia sauti tayari kwa kuanza kazi ya kumrekodi mwanamke huyo.

“Tuambie Rose!” alisema Brock.

“Ni miaka 84 imepita.”

“Haina shida. Jaribu kukumbuka kitu chochote kile.”

“Kweli unahitaji kusikia hili au hutaki Mr. Lovett?” alimuuliza Brock ambaye akaitikia kwa kutingisha kichwa.

“Ni miaka 84 imepita lakini bado ninaweza kusikia harufu ya mchoro ule. Titanic iliitwa Meli ya Ndoto, na kweli ilikuwa hivyo,” alisema Bibi Rose.

 

Je, nini kiliendelea?
Tukutane Alhamisi hapahapa.

Usipitwe na Matukio, Install App Yako ya Kijanja na Namba Moja Tanzania ya Global Publishers

Android Bofya ===> Google Play

iOS Bofya ===>Apple Store

Leave A Reply