The House of Favourite Newspapers

SIMULIZI YA KUSISIMUA: THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 16

0


MTUNZI: Hashim Aziz (Hashpower)
0719401968
ILIPOISHIA:
“Hakikisha huyo malaika wa Mungu anafikishwa kwenye mikono salama! Tumia akili yako kujua utafanya nini, lakini nataka awe salama lakini asiache alama yoyote inayoweza kumuunganisha na sisi,” alisema Bosi Mute, nikainamisha kichwa kwa adabu kuonesha kukubali, kisha nikachukua lile burungutu la fedha na kuliweka mfukoni.

SASA ENDELEA…
Bonta naye aliinama kwa adabu kama ishara ya utii kwa Bosi Mute kisha akatangulia yeye kutoka, nikawa namfuata kwa nyumanyuma. Tulishuka mpaka chini, Bonta akanigeukia na kuniambia kwamba mtihani niliopewa natakiwa kuufanya bila msaada wa mtu yeyote.

“Sasa nifanyeje?”
“Unaweza kwenda kumuacha kwenye maeneo ambayo watu wenye roho nzuri watamchukua na kwenda kumlea, unaweza kwenda kumuacha kanisani, msikitini, kwenye vituo vya watoto yatima na kadhalika, lakini hutakiwi kuonekana kama wewe ndiye uliyemuacha,” aliniambia Bonta, kidogo nikashusha pumzi kwa sababu angalau nilipata mwanga wa nini cha kufanya.

‘Nini kilitokea pale? Mbona mlikuwa mnanipigia makofi?”
“Ulipewa bastola isiyo na risasi kwa lengo la kukupima kama una ujasiri wa kuua! Ulipovuta ‘trigger’, ulionesha kwamba kama kungekuwa na risasi, ulikuwa tayari kumuua huyu mtoto, hicho ni kipimo cha juu kabisa katika hizi kazi zetu!” alisema Bonta, sasa nikapata picha ya kilichotokea.

Kumbe walikuwa wanataka kunipima kama nina roho ya kuua! Na kweli kwa hali ilivyokuwa, nilikuwa nimeshamuomba msamaha Mungu wangu kabla hata ya kufanya dhambi kwa sababu kwa sababu ni kweli kama kungekuwa na risasi, ningemuua mtoto wa watu.

Ujue wakati mwingine tunawalaumu tu majambazi au magaidi kuwa wana roho mbaya sana lakini kuna mitihani wanapitia wanajikuta tu tayari roho zao simeshabadilika na kuwa kama wanyama.

Na wasichokijua watu wengi, damu ya mtu ni nzito sana! Unapoanza kumwaga damu ya mtu wa kwanza, akili zako zinakuwa ni kama zimekufa ganzi na kamwe hazitaweza kurudi na kuwa sawa mpaka na wewe ufe! Ni rahisi sana kwa mtu ambaye ameshawahi kuua, kuendelea kuua tena na tena mpaka na yeye atakapouawa kinyama.

Huwezi kuyakatisha maisha ya binadamu mwenzako halafu ukabaki kuwa salama, yaani hata kama hakuna mtu yeyote anayejua, damu ya mtu ni nzito, itakufuata tu na lazima na wewe utaishia kufa kifo cha ajabu ajabu.

Kama huamini, hebu fuatilia historia za watu wote ambao unajua walishawahi kufanya mauaji uangalie mwisho wao ulikuwaje! Bahati mbaya kwangu, ni kwamba nilikuja kuujua ukweli huu tayari ikiwa ni ‘too late!’

Laiti kama ningeujua kabla mambo hayajaharibika, ningekuwa tayari hata nife mimi kuliko kuyakatisha maisha ya mtu mwingine, narudia tena kusisitiza hakuna kosa kubwa kama mauaji na hata kama utaweza kuikwepa mikono ya sheria, bado kuna hukumu fulani ya asili ambayo itakutafuna popote ulipo mpaka na wewe utakapokufa.

Nitakuja kukuelezea vizuri hapo baadaye jinsi nilivyoteseka kwa sababu ya uzito wa damu za watu waliopoteza maisha kwenye mikono yangu! Hakika mimi ni mwenye dhambi.

Basi nilitoka na yule mtoto mpaka nje, sikuwa najua kuendesha pikipiki wala gari kwa hiyo njia salama ilikuwa ni kutembea kwa miguu kisha nikatafute usafiri nikiwa nje.

Kabla sijatoka, akili ilinituma kurudi kwanza kwenye lile gari, nikapekuapekua na kukuta kuna kadi ya kliniki ya mtoto pamoja na ‘chuchu’ ya bandia ambayo mtoto huyo alikuwa akiinyonya, nikaisafisha kisha nikamuwekea mdomoni, akawa ananyonya huku akinitazama sana usoni.

Baada ya kutoka nje, nilianza kutembea harakaharaka huku nikiwa nimemkumbatia mtoto huyo kifuani, mkono mmoja nikiwa na bahasha iliyokuwa na kadi yake ya kliniki. Mbele kidogo, nilisimamisha ‘bodaboda’, nikamuelekeza dereva kunipeleka Mombasa.

Nilitaka nikifika pale ndiyo nijue naelekea upande gani kwa sababu bado sikuwa naujua mji na nilikuwa na mtoto wa watu ambaye mama yake ameuawa. Kama mtu angenishtukia na kunikamata, maana yake angehisi kwamba pengine mimi ndiye niliyemuua mama yake au najua wahusika ni akina nani, jambo ambalo lilikuwa la hatari kwelikweli.

Nilitakiwa kuwa makini na hilo nililitambua, basi alinipeleka mpaka Mombasa, pale nikakodi Bajaj na kumuelekeza dereva kwamba anipeleke mjini. Ilikuwa ngumu kidogo kuelewana naye kwa sababu alitaka kujua ni mjini ipi ninayoenda mimi, mwisho tukakubaliana kwamba anisogeze mpaka Buguruni kisha nitajua mwenyewe nini cha kufanya.

Kwa bahati nzuri, yule mtoto alilala muda mfupi baadaye, kwa hiyo njia nzima yeye alikuwa akikoroma tu. Tulienda mpaka Buguruni, nikatoa noti mbili za shilingi elfu kumikumi na kumpa, wala hata sikuulizia chenji, nikateremka na kuvuka barabara. Mbele kidogo nilisimamisha teksi iliyokuwa ikipita bila abiria.
“Unaelekea wapi bosi!”

“Mjini.”
“Posta au Kariakoo!”
“Kariakoo!” nilijibu bila kufikiria kwa sababu ukweli ni kwamba sikuwa nakujua Kariakoo wala Posta zaidi ya kuwa nasikia tu kwenye bomba.

“Huyo mtoto wa nani, mbona kama namjua!” alisema yule dereva, mapigo ya moyo yakanilipuka paah!
“Kwani we..we ni mwenyeji wa Mku..ranga?”
“Hapana! Mi naishi hapahapa Dar.”

“Basi utakuwa umemfananisha, huyu ni mtoto wa aunt yangu Suzy wa Mkuranga, wamekuja kututembelea.”
“Amefanana na mtoto wa dada mmoja anafanya kazi airport, huwa nawabeba mara kwa mara kama gari lake likiwa na matatizo,” alisema yule dereva teksi, mapigo ya moyo yakazidi kunienda mbio.

Kwa ilivyoonesha hakuwa amekosea, mtoto aliyekuwa akimzungumzia ndiyo huyohuyo kwa sababu hata mle ndani ya gari wakati nafanya usafi niliona nyaraka zilizoonesha zinahusu Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere.

Ilibidi nibadilishe mada haraka kwani kama tungeendelea kuzungumza, pengine angepata nafasi ya kumtazama vizuri na pengine kupata uthibitisho kwamba alichokuwa anakihisi ndiyo ukweli.

“Siku hizi Dar foleni imepungua kidogo eeh!”
“Imepungua wapi wakati ndiyo inazidi kuongezeka, yaani zamani mimi nilikuwa naweza kuiga tripu kibao lakini siku hizi, mpaka hesabu ya bosi nashindwa kukamilisha, hakuna kabisa kazi kwa sababu ya foleni,” alisema yule dereva huku gari likiendelea kuchanja mbuga.

Safari iliendelea mpaka tulipofika Kariakoo. Katika kumbukumbu zangu, niliwahi kufika Kariakoo si zaidi ya mara tatu na nakumbuka tulikuwa tukienda kununuliwa nguo za sikukuu na baba kabla hajaanza kuumwa. Kwa hiyo sikuwa naijua vizuri Kariakoo lakini niliamini lazima nitapata majibu.

“Nikushushie sehemu gani?”
“Sehemu yoyote ambayo haina msongamano wa watu wengi, si unajua nina mtoto.”
“Kwani mtoto unampeleka wapi?”

“Nampeleka kwa mama yake, kuna sehemu anatusubiri nikishuka nitampigia simu anielekeze sehemu ya kukutana naye.”
“Sasa kwa nini usipige tu ukiwa bado ndani ya gari? Unajua kutembea na mtoto Kariakoo ni hatari, si unaona watu walivyo wengi.”

“Simu yangu haina vocha, mpaka niteremke nikanunue,” nilimjibu dereva huku nikitoa noti mbili za shilingi elgu kumikumi na kumpa. Niliona nikiendelea kushangaashangaa anaweza kunishtukia, kabla hata hajanijibu vizuri tayari nilishafungua mlango, nikashuka harakaharaka nikiwa nimembeba vizuri yule mtoto.

Hapo tulikuwa kwenye Mataa ya Shule ya Uhuru, nadhani alinishtukia kwa sababu hata nilipoteremka, hakuondoa gari, akawa anaendelea kunitazama naelekea wapi, harakaharaka nikajichanganya kwenye watu wengi na kumuacha kwenye mataa.

Nilikuwa natetemeka mno maana kama ningeshtukiwa sijui nini kingetokea, lazima ningekamatwa na katika kuutafuta ukweli, ingeweza kubainika kwamba mama wa mtoto huyo ameuawa na pengine huo ndiyo ungekuwa mwisho wangu wa kukaa uraiani.

Nilipofika mbali kidogo, niligeuka na kuitazama ile teksi, bado yule dereva alikuwa amesimama palepale kwenye mataa, nikazidi kuongeza mwendo na kutokomea ndanindani kabisa kwenye mitaa ya Kariakoo.

Nilizunguka sana nikiwa hata sielewi naelekea wapi, tukio la yule dereva teksi lilikuwa limenichanganya kabisa kichwa changu. Wanawake wengi niliokuwa napishana nao, walikuwa wakinishangaa kwa nini natembea na mtoto kwenye jua na kwenye maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu, hali iliyonipa wakati mgumu sana.

Mara nilipata wazo, nikasogea kwenye duka moja la vipodozi ambalo wauzaji wake wengi walikuwa ni wanawake.
“Shikamoo mama,” nilimwamkia mwanamke mmoja aliyekuwa kama na asili ya ushombeshombe hivi, akaniitikia kwa uchangamfu.

“Samahani, eti hapa kuna choo cha kulipia jirani?” nilimuuliza kimitego.
Bila kujua malengo yangu, alinielekeza mahali kulipokuwa na choo cha kulipia, nikamuomba anishikie mtoto mara moja kwa sababu nisingeweza kwenda naye.

“Mlete tu, haina shida! Mama yake yuko wapi?”
“Yupo pale dukani anachaguachagua nguo,” nilimdanganya, akanipokea mtoto kwa uchangamfu na kuanza kumrusharusha juu, nikaona hiyo ndiyo chansi niliyokuwa naisubiri. Nilitoka na kujifanya nafuata maelekezo ya kule alikonielekeza kwamba ndiyo kuna choo.

Nilitembea harakaharaka, nilipofika eneo hilo nililoelekezwa, niligeuka nyuma kuangalia kama alikuwa akinitazama, wala hakuwa na habari na mimi, akawa anaendelea kucheza na yule mtoto. Nikajichanganya kwenye watu wengi na kuongeza mwendo, nikapotelea kwenye mitaa ya ndanindani.

Nilikatiza mitaa kwa kasi na baadaye nikatokea barabarani, harakaharaka nikasimamisha bodaboda.
“Nipeleke kwenye kituo cha daladala.”

“Unataka kupanda magari ya kwenda wapi?”
“Gongo la Mboto.”
“Una hela kamili hapo?”
“Nina noti ya shilingi elfu kumi,” nilimjibu yule dereva wa bodaboda, akawa ni kama anasitasita, akaniambia bodaboda haziruhusiwi Kariakoo kwa hiyo anaweza kukamatwa wakati akinishusha na kuanza kutafuta chenji.

“Au nikupeleke mpaka Buguruni, utanipa buku tatu,” aliniambia, nikakubaliana na wazo hilo, nikapanda na muda mfupi baadaye, tukawa tunaelekea Buguruni. Mara kwa mara nilikuwa nageuka nyuma kutazama kama hakuna mtu yeyote anayetufuatilia, bodaboda ikazidi kupasua lami huku nikimsisitiza dereva kuongeza kasi.

Hatimaye tulifika Buguruni, akanishusha na kunirudishia chenji, harakaharaka nikajichanganya kwenye kundi la watu huku nikiwa bado natetemeka sana. Sikujua nini itakuwa hatma ya yule mtoto lakini niliamini tayari yupo kwenye mikono salama kwa sababu wanawake huwa wana huruma sana kwa watoto, tofauti na wanaume.

Niliulizia mahali pa kupata magari ya Gongo la Mboto, msamaria mmoja akanielekeza, basi harakaharaka nikaelekea kituoni, nikapanda kwenye gari na safari ikaanza. Nilienda kushukia Mombasa, nikachukua bodaboda na safari ya kurudi kambini ikaanza.

Hata sikuwa napajua panaitwaje lakini nilimuelekeza dereva kwamba twende nikifika ninapokwenda nitamwambia. Kweli tuliondoka kwa kasi na baada ya kama dakika thelathini, tukawa tumekaribia. Kwa kuwa sikutaka ushahidi, nilimwambia asimame, nikamlipa fedha zake kisha nikaanza kutembea kwa miguu kuelekea pale kambini.

Kwa kuwa tayari nilikuwa najua kwamba ukisogelea tu eneo hilo unaonekana na kamera zilizokuwa zimefungwa kitaalamu kiasi kwamba ni vigumu kwa mtu asiyehusika kujua kwamba kuna kamera, nilikuwa makini na kila kitu nilichokuwa nakifanya.

Nilipofika tu getini, kabla hata sijagonga, mlango mdogo wa pembeni ulifunguka, mlinzi mwenye silaha, aliyevalia sare maalum alinikaribisha kwa kunionesha tu ishara kwamba niingie, nilipoingia geti lilijifunga, nikashusha pumzi ndefu wakati nikitembea harakaharaka kuelekea kule ndani.

 

Je, nini kitafuatia? Usikose kesho hapahapa! Unaweza pia kusoma au kusikiliza hadithi nyingine kwa kuingia:

www.simulizizamajonzi7113.blogspot.com , Facebook: Simulizi za Majonzi au Youtube: Hashpower Online.

 

Usisahau kulike, share na ku-subscribe.

Leave A Reply