The House of Favourite Newspapers

Simulizi ya Mrisho Mpoto; Mkewe ajifungua, ashindwa kumpa jina mtoto

0

OLYMPUS DIGITAL CAMERA

MPENZI msomaji wiki iliyopita katika simulizi hii ya Mrisho Mpoto tuliishia pale alipofunga harusi ya ajabu ambapo keki ilikuwa boga na dafu ikawa ndiyo shampeni. Katika harusi hiyo pia MC alikuwa Mrisho mwenyewe na wenzake tisa na pia tulielezea pale mwisho wa harusi hiyo alipomaliza alifunga mlango na kurudisha ufunguo kwa wahusika waliompa ukumbi.

Tambaa nayo mwenyewe…

“Baada ya kuoa, nikakaa fungate kwa siku kadhaa ambapo nilipata mwaliko mwingine wa kwenda tena Marekani sehemu moja inaitwa Maryland. Nikachukuliwa nikapelekwa kama mtoto, maana kama nilivyosimulia hapo nyuma wale Wazungu walikuwa wakiniona kama gifted yaani mtu aliyebarikiwa na kuwa zawadi kutoka kwa Mungu. Wakaanza kunisoma kujua mimi ni mtu wa aina gani.”

Duhh! Ikawaje sasa Mrisho, ulitumia muda gani kuwepo huko?

“Nilitumia muda mrefu, kama miezi tisa hivi lakini nilikuwa naingia kwenye idara tu za mambo ya arts. Kuna siku nilipelekwa eneo jingine huko Washington DC, Marekani linaitwa Black Stage. (Black stage ni sehemu ya watu weusi tu wanaojumuika pamoja na kutoa burudani) kwa kuwa walikuwa wameona kitu ndani yangu, wakanipokea nikawa nafanya shoo zangu huko.”

Anainama kana kwamba ana uchungu wa kitu anachotaka kukizungumza, kisha namuuliza vipi tena Mrisho, ananiangalia na kuendelea…

“Nakumbuka siku moja nikiwa katika shoo huko Washington DC, niliposhuka tu nilikutana na simu kutoka Tanzania ambapo mwalimu wangu wa Kikundi cha Parapanda, Mgunga Mnyenyelwa alikuwa akinipigia, akaniambia kuwa mke wangu amejifungua.

“Nilifarijika sana, kwa kuwa Mnyenyelwa nilikuwa namchukulia kama baba yangu, mwalimu wangu, yeye ndiye aliyempa jina mwanangu wakati nipo Marekani. Alimpa jina la Manju likiwa na maana ya kiongozi.

“Nilirudi nyumbani (Tanzania) nikamuona mwanangu, nikafurahi lakini baada ya kama miezi mitatu tena nikapata safari ya kwenda nchini Uingereza, nikaona kujifungua kwa mke wangu ni kama kumeleta baraka kwangu kwani safari zilikuwa hazikauki, mara nimeenda Zambia, Nairobi na sehemu mbalimbali. Licha ya kutembea nchi zote hizo, bado maisha yetu yalikuwa ya kawaida. Tulikuwa tukiishi palepale tena maisha ya kimaskini tu.”

Ananishtua kidogo, safari nje ya nchi kila mara na nyingine alikuwa akiitwa na Wazungu halafu ananiambia eti alikuwa maskini, anagundua ameniweka katika njia panda, anafafanua…

“Ujue Wamarekani walivyokuwa wakiniita kule na ninakaa nao, naishi nao, nia na madhumuni walikuwa hawataki kabisa kunipa hela, walikuwa wanataka kunijenga niwe na uelewa mkubwa zaidi. Waliamini kabisa kama wangenipa hela nisingeweza kufanya kile wanachokitaka kwa hiyo walikuwa wako tayari kunipa knowledge zaidi. Walinitengeneza hasa kwenye story telling, acting na editing na baada ya hapo nikapata tenda hukohuko ya kubadilishana lugha.

 Hii ilitokana na makubaliano ya serikali ya Tanzania na Uingereza ambapo watoto wa huko walikuwa wanafundishwa na Watanzania na watoto Watanzania wanafundishwa na Waingereza.

“Wakati bado nikiwa nchini Uingereza, mwenzangu kutoka Kundi la Parapanda, Irene Sanga alinipigia simu na kuniambia kuwa ana shairi ambalo angependa nilione na tuimbe naye pamoja. Nikamwambia asubiri nikirudi.

“Niliporudi Irene akanipa hilo shairi, tukashirikiana kuyaweka sawa hivyo tukaimba pamoja ndiyo wimbo ule wa Salamu Zangu na hapo ndipo safari yangu ya muziki ikaanza rasmi jina la Mjomba likaanzia hapo na kuanza kupata shoo kibao, lakini kupata shoo hizo likatokea jambo ambalo siwezi kulisahau maishani mwangu…

JE, unajua ni jambo gani hilo lililompata Mrisho? Endelea kufuatilia simulizi hii kali na ya kusisimua wiki ijayo hapahapa.

Leave A Reply