The House of Favourite Newspapers

Sio Vibaya Tukatumia Kombe La Dunia Kujifunza Mambo Mazuri

TUPO kwenye kipindi cha mapumziko baada ya kumalizika kwa msimu wa 2017/18 ambao ulihitimishwa rasmi Juni 2, mwaka huu pale michuano ya Kombe la FA ilipofikia tamati kwa Mtibwa Sugar kuwa mabingwa.

 

Mtibwa wamekuwa mabingwa wa FA baada ya kuifunga Singida United mabao 3-2 katika mchezo wa fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

 

Kabla ya hapo, Ligi Kuu Bara ilifikia tamati Mei 28, mwaka huu kwa Simba kuwa mabingwa wakilichukua kombe lililokuwa likishikiliwa na Yanga ambayo ilimaliza msimu ikiwa ya tatu.

 

Yanga ndiyo ilikuwa bingwa mtetezi ikiwa imelichukua kwa misimu mitatu mfululizo nyuma, safari hii mambo yalikuwa magumu kwao, wakaishia nafasi ya tatu.

Wakati hapa nyumbani michuano mbalimbali imesimama tukisubiria msimu mpya wa 2018/19, kuna michuano ya Kombe la Dunia imeanza huko Urusi.

 

Juzi Alhamisi, michuano hiyo ilianza kuunguruma ambapo timu 32 zitakuwa zikichuana kumsaka mshindi mmoja.

Mshindi huyo mmoja anatafutwa kuweza kuchukua ubingwa wa michuano hiyo ambao upo mikononi mwa Ujerumani iliouchukua mwaka 2014 wakati michuano hiyo ilipofanyika nchini Brazil.

 

Tumeona wenyeji Urusi wakianza kwa kishindo kwa kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Saud Arabia katika mchezo wa kwanza wa ufunguzi wa michuano hiyo uliopigwa juzi Alhamisi.

 

Watu wengi walikuwa hawaipi nafasi kubwa Urusi kupata ushindi huo, lakini mwisho wa siku wameweza kufanya kile ambacho wengi hawakuwa wakiamini jambo ambalo linadhihirisha kwamba soka si mchezo wa kutabirika hata kidogo ingawa mara chache watu hufanikiwa kutabiri matokeo.

 

Wakati michuano hiyo ikiwa imeanza, hapa kwetu ligi na michuano mbalimbali imesimama ambapo ni wakati mzuri kwa wachezaji wetu kujifunza mambo kutokana na kile kinachoendelea kwenye michuano hiyo.

Kuna vingi vya kujifunza kwa wachezaji wetu ikiwemo namna ya uchezaji na mambo mengine, lakini mbali na wachezaji kujifunza huko, pia hata viongozi wetu wa soka na serikali nao wanaweza kujifunza kitu hapo.

 

Nikukumbushe tu kuwa, mwakani Tanzania itakuwa mwenyeji wa michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa vijana chini ya miaka 17, hivyo kupitia Kombe la Dunia hili tunaweza kujifunza namna ya maandalizi yanavyokuwa.

 

Tuna siku chache kabla ya kuanza kwa michuano hiyo, hivyo maandalizi yanahitajika mapema ili tu tuweze kuwa na michuano yenye kuvutia.

Tukiboronga itakuwa aibu kwetu na pengine Shirikisho la Soka Afrika (Caf) litatunyima siku nyingine kuandaa michuano mikubwa zaidi.

Hivi sasa Caf wametuamini na kutupatia michuano hii ya vijana, hilo tulichukulie kama kipimo chetu, tukifanya vizuri basi kuna uwezekano wa kupata nafasi ya kuandaa ile michuano ya wakubwa kwa siku za mbele.

 

Hivyo serikali inatakiwa ijifunze miundombinu ya wenzetu namna ilivyo ili na sisi tufanye kama walivyofanya wao. Hata kama haitakuwa kwa kiwango cha juu kutokana na tofauti ya uchumi wao na wa kwetu, lakini angalau tusiwakere wageni wetu.

 

Wageni wakija wanatakiwa waishi sehemu zenye hadhi, huko barabarani wanapopita pawe sehemu salama kwao ili tu kuifanya michuano hiyo kuwa na mvuto na izungumzwe vizuri mara itakapomalizika.

 

Hivi karibuni, wakaguzi kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) na wale wa Caf, walikuja kukagua miundombinu kabla ya kuanza kwa michuano hiyo, cha kufurahisha ni kwamba walikubaliana na maandalizi yaliyopo ambapo viwanja vya Azam Complex na Taifa vimepitishwa kutumika kwa michuano hiyo.

 

Kumbuka michuano hiyo itafanyika kwenye ardhi ya Dar es Salaam, lakini awali kulikuwa na ombi ifanyike mikoa mbalimbali ya Tanzania, kutokana na miundombinu kutokuwa rafiki sana kwa mikoa mingine, ndiyo maana ikapangwa kufanyika Dar pekee.

Comments are closed.