The House of Favourite Newspapers

SIRI TATU VITA YA MONDI,KIBA

MAMBO bado ni moto! Ile vita kati ya mafahari wawili wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba ‘Alikiba’ na Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ imezidi kuchukua sura mpya ambapo siri tatu zinazotajwa kuwa sababu ya ugomvi wao zimetajwa, Risasi Jumamosi limezinasa kutoka vyanzo mbalimbali.

CHANZO CHASHUSHA UBUYU

Chanzo kilicho karibu na familia ya Kiba kilieleza mambo ambayo yanapewa asilimia kubwa kuwa sababu ya ugomvi huo yaliyomfanya Kiba atoe kauli nzito kwa Mondi Oktoba 30, mwaka huu katika ukurasa wake wa Instagram.

Kiba aliandika; “Usiniletee mambo ya darasa la pili unaniibia penseli halafu unanisaidia kutafuta (UNIKOME). Mwanaume huwa anaongeaga mara moja tu sasa ukitaka nikuweke uchi watu wajue unayonifanyia hata kwenye hilo tamasha hatokuja mtu sasa tuishie hapo nakutakia tamasha njema (jema).

Kiba alitoa kauli hiyo baada ya Mondi kusema ametuma salamu kwa uongozi wa Kiba, kumuomba ashiriki kwenye Tamasha la Wasafi linalotarajia kufanyika Novemba 9, mwaka huu katika Viwanja vya Posta jijini Dar.

Tafakuri nzito ni juu ya kauli ‘mambo unayonifanyia’ ambayo Kiba akiyasema Mondi atakuwa amevuka nguo ni yepi?

TURUDI KWA CHANZO CHETU

Chanzo hicho kilisema, kauli aliyoitoa Kiba ilimaanisha jinsi gani wawili hao wana bifu zito ambalo linahusisha masuala ya kukwamishana maendeleo ya kimuziki.

“Unajua kabla ya jana (Oktoba 30) watu walikuwa hawajui yaliyo nyuma ya pazia, walijua bifu la wawili hao limepoa lakini Mondi alipochokoza ndipo Kiba alipouwasha na kimsingi bifu hili ni zito sana si la kuisha leo wala kesho.”

SIRI YA KWANZA

Chanzo hicho kilidai kuwa, siri ya kwanza ambayo inaaminika kwa kiasi kikubwa inaweza kuwa sababu ya kuwepo kwa vita hiyo ni masuala ya ushirikina yanayohusisha pande hizo mbili.

“Nafikiri utakuwa unafahamu uwepo wa tuhuma za masuala ya uchawi, mambo haya yamewahusu sana Mondi na Kiba.

“Unakumbuka kwenye shoo ya Tigo katika Viwanja vya Leaders Kinondoni jijini Dar (Mondi na Kiba walifanya shoo) iliyofanyika 2015, mambo yalivyokuwa, imani za kishirikina zilikuwa wazi, Kiba hakuingilia mlango aliopita Mondi,” chanzo kilidai.

Mbali na madai hayo ya chanzo, habari kutoka kwenye mitandao ya kijamii hasa kutoka kwa timu inayomsapoti Kiba zilisambazwa kwa wingi kumtuhumu Mondi kuwa amekuwa akimkwamisha hasimu wake huyo kimuziki.

Mondi hakupatikana kufafanua tuhuma hizo, lakini mara kadhaa zilipokuwa zikizushwa tuhuma hizo viongozi wanaosimamia kazi zake akiwemo Said Fella wamekuwa wakijitokeza na kuzikanusha.

SIRI YA PILI

Siri ya pili ambayo Risasi Jumamosi liliinyaka iliyoshibisha bifu la wawili hao ni suala ‘fitna za kuhonga fedha kwenye baadhi ya vyombo vya habari hususan radio na televisheni ili kuzuia nyimbo za hasimu zisichezwe.

Vituo ambavyo vimekuwa vikitajwa kutopiga nyimbo za Mondi ni Clouds Radio na TV huku Wasafi TV na Radio zikigomea kucheza nyimbo za Kiba.

Aidha kumekuwepo na malalamiko kutoka pande hizo mbili kuwa kuna baadhi ya waandishi wa habari na vyombo vyao wamekuwa wakitumika kimkakati kukwamisha kazi na umaarufu wa mahasimu hao.

“Hili ni tatizo kubwa, wanazungukana kwenye vyombo vya habari, unakuta mmoja anaenda kwenye kituo fulani kumchezea rafu mwenzake na mwingine anakwenda kuharibu kwenye kituo kingine, jambo hili limekuwa likijenga chuki isiyoisha kati yao.

“Mtu anapozuia nyimbo zako zisichezwe maana yake anataka usisikike na usiposikika maana yake huwezi hata kupata shoo za ndani na nje ya nchi hivyo utajikuta badala ya kwenda mbele unarudi nyuma,” kilisema chanzo kilicho karibu na mmoja kati ya mahasimu hao wa kimuziki nchini.

SIRI YA TATU

Chanzo kingine kilimwaga data kuwa, siri nyingine inayoweza kuwa kichocheo cha bifu la wanamuziki hawa mastaa ni pamoja na fitna za waandaaji wa shoo za nje ambao hutumika kama mawakala katika kutafuta wasanii wa Bongo.

“Huu ni sawa na uuaji, kuna kamchezo wanachezeana katika shoo za nje ambapo uongozi unazungumza na mawakala wakubwa wa muziki hivyo kila wakihitaji msanii kutoka Bongo, wanamshawishi amchukue yule wanaomtaka wao huku wakimponda yule mpinzani.

Takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa Mondi amekuwa mtamu kwa shoo za nje kuliko Kiba pengine inaweza kujenga hisia za kile kinachoelezwa na chanzo kuwa ‘anafitiwa’.

Ingawa Kiba mwenyewe hajazungumza wazi kuhusu hilo la kutengenezewa fitna za kutopata mialiko ya ng’ambo, lakini kauli yake ya kusema akianika anayofanyiwa na Mondi atamvua nguo yametafsiriwa kimtazamo kuwa huwenda yanamaanisha hicho kinachotajwa kwenye siri ya tatu na chanzo chetu.

 

DUDE ATOA MAONI

Msanii wa sinema za Kibongo, Kulwa Kikumba ‘Dude’ alipozungumza na gazeti hili kuhusu mtazamo wake kama mdau wa sanaa Bongo, alisema kikubwa kinachowasumbua vijana hao ni ufalme wa muziki ambao husababisha wafikie hatua ya kushutumiana ushirikina na mambo mengine mabaya.

“Kila mmoja anataka kuwa namba moja, mmoja akiona mwenzake yupo juu anajua kabisa si bure, lazima kuna kitu kafanyiwa na mwenzake na hapo ndipo imani inapowapeleka kwenye ushirikina.

“Wanashindwa kutambua ushirikina hauwezi kukuweka juu milele, utaanguka tu. Hivyo ninavyoamini mimi, juhudi na maarifa katika kazi ndizo zinazoweza kukufanya ufike mahali unapopataka,” alisema Dude.

BABA MONDI NAYE ATIA NENO

Akizungumza na Risasi Jumamosi kuhusiana na suala hilo, baba mzazi wa Mondi, Abdul Juma ‘Baba D’ aliwataka vijana hao kuachana na imani potofu na kama kuna mahali walikoseana hawana budi kusameheana ili waweze kwenda mbele.

“Mimi siamini sana kwenye ushirikina hivyo niwasihi tu wanangu hawa wakae chini na kuzungumza wapi walikoseana? Nilisikia Kiba amesema kuna mambo Mondi anamfanyia ambayo akiyasema yanaweza hata kumharibia shoo yake, kama hayo yapo basi wazee wapo aje ayaweke wazi yatafutiwe suluhu kuliko kukaa nayo moyoni,” alisema baba Mondi.

Walipotafutwa Kiba na Mondi ili kusikia wanazungumziaje kuhusu siri zilizotajwa kama sababu ya kutoelewana kwao, simu zao ziliita bila kupokelewa.

TUJIKUMBUSHE

Kwa muda mrefu, Kiba na Mondi wamekuwa hawapikiki chungu kimoja ambapo awali chanzo cha msingi kilitajwa kuwa ni Wimbo wa Lala Salama ambao ilielezwa kuwa Mondi alifuta mashairi ya Kiba katika wimbo huo jambo ambalo lilimkasirisha vibaya mwenzake kiasi cha kumfanya anune.

Hata hivyo, baada ya jambo hilo kupita Mondi amekuwa akionesha kuwa tayari kutaka kukaa meza moja na mwenzake huyo lakini Kiba amekuwa hataki hata kusikia.

 

STORI: ERICK EVARIST

Comments are closed.