The House of Favourite Newspapers

SIRI WACHUNGUZI WA NJE KUGOMEWA BONGO YATAJWA

Mohamed Dewji ‘Mo’

SERIKALI iwaite wachunguzi wa Kimataifa.” Baadhi ya wananchi wamekuwa wakitoa kauli hizo baada ya kuwepo kwa tukio la Mbunge wa Singida Kaskazini, Tundu Lissu kupigwa risasi mwaka jana na hivi karibuni kutekwa kwa mfanyabiashara bilionea nchini, Mohamed Dewji ‘Mo’ na watu wasiojulikana bila wahusika kutiwa mbaroni.  

Kauli hizo za wananchi ambazo zimekuwa zikitolewa hasa kupitia mitandao ya kijamii, zimekuwa zikiambatana na swali la: “Kwa nini Serikali inasita kufikia uamuzi wa kuwaita wachunguzi wa ng’ambo kuja kuwafanya hao waliomshambulia Lissu na kumteka Mo wajulikane?”

 

Kufuatia mara kadhaa Serikali kusisitiza kuwa haioni sababu ya kufanya hivyo, Ijumaa lilimtafuta ofisa wa ngazi za juu wa usalama wa taifa aliyestaafu hivi karibuni ili kujua kinachoizuia Serikali kuomba msaada wa kiuchunguzi kwa lengo la kuwapata wahalifu ambapo siri nzito zilitajwa na ofisa huyo.

 

“Nitakujibu kwa sababu ya ukaribu wetu, lakini sikutakiwa kufanya hivyo kwa sababu mimi si msemaji wa idara ya usalama wa taifa.

“Lakini kwa kukusaidia na kuwasaidia wengine ni kwamba si kila tukio linahitaji msaada wa wachunguzi wa nje, maana siku hizi jambo kidogo tu utasikia watu wanataka vyombo vya uchunguzi kutoka nje vije.

 

“Unataka kuniambia Uingereza hakuna matukio ya kihalifu yanafanywa na vyombo vyao vya usalama tunavyoviamini vinashindwa kuwabaini wahusika na haviombi msaada vya nje?

“Waliomuua Princess Diana nani anajua A-Z yake? Lakini wana chombo imara kabisa cha kiuchunguzi kinaitwa Scotland Yard, mambo yamekwenda mwisho tukaambiwa hayo ni mambo yao ya ndani na mchezo ukaishia hapo,” alisema ofisa huyo.

Image result for mo dewji

Aliongeza kuwa pamoja na kuwepo kwa faida za kuita vyombo vya uchunguzi vya nje lakini vina hasara kwa usalama ambapo ni pamoja na hatari ya siri nyeti kuweza kudukuliwa na hao wanaoitwa kufanya uchunguzi.

Katika dunia ya leo, kumuita mtu aje akusaidie kuondoa shida zako si ajabu akakuletea shida nyingine; we unguliwa nyumba yako uone wanaokuja kukusaidia kuzima moto ndiyo haohao wanakuiba fenicha zako.

 

“Wanaweza kuja kusaidia kuchunguza tukio moja lakini wakachunguza na mambo mengine mia mbili yanayohusu usalama wako, siri zako na mipango yako ya ulinzi wa nchi baada ya siku unaweza kujikuta vitu vyako vingine vimevuja.

“Mbali na hilo kuita wasaidizi katika kila tukio ni kuondoa imani ya wananchi kuhusu uimara wa vyombo vya usalama wa nchi, jambo ambalo ni hatari, huwezi kuwa na taifa ambalo wananchi wake hawawaamini wanajeshi wake,” alisema ofisa huo.

 

Matukio ya Lissu kushambuliwa kwa risasi na wasiojulikana, Mo kutekwa, mwandishi wa habari Azory Gwanda, Ben Saanane kutekwa na kutoonekana yamekuwa yakitumiwa na wengi kama sababu za kuifanya Serikali ione imuhimu wa kuita vikosi vya uchunguzi vya kimataifa, jambo ambalo afisa huyo alipinga na kuwaomba wananchi kuwa na imani na vyombo vyao vya usalama huku akiomba mamlaka husika kuongeza kasi za kuhakikisha amani na utulivu unakuwa imara.

 

STORI: Richad Manyota, Ijumaa

Comments are closed.