The House of Favourite Newspapers

Sitasahau Nilivyokumbana na Jini Mwanaume-8

0

ILIPOISHIA WIKIENDA
“Dereva rudi nyuma ulifuate lile gari,” nikamwambia dereva wa teksi huku nikijisikia ahueni kuliona gari hilo.
Dereva wa teksi akapunguza mwendo na kukata kona. Akalifuata gari hilo la shemeji lililokuwa limesimama.
Ile teksi iliyokuwa nyuma yetu ilipita moja kwa moja na kwenda kusimama mbele.
SASA ENDELEA…

Kabla ya teksi kusimama sawasawa nilishafungua mlango. Teksi ilisimama ubavuni mwa gari la shemeji. Nikashuka na kufungua mlango wa nyuma wa gari la shemeji nikajipakia harakaharaka.
Nikampungia mkono dereva wa teksi aende zake. Ile teksi ikaondoka.
Ndani ya gari la shemeji kulikuwa na shemeji pamoja na dada.
“Iko wapi hiyo teksi yenye huyo jini anayekufuata?” Shemeji akaniuliza.
“Si ile pale.”
Nikawaonesha teksi hiyo iliyokuwa imesimama barabarani umbali wa hatua kadhaa kutoka pale tuliposimama sisi. Wakati nawaonesha ile teksi, teksi hiyo ikaondoka na kuendelea na safari yake.
“Niifuate?” Shemeji akauliza.
“Uifuate ya nini?” Dada naye akamuuliza shemeji kisha akaongeza:
“Umeshaambiwa ni jini, tuna kazi naye gani sisi!”
Dada aliponiona ninavyotetemeka alishuka kule mbele alikokuwa amekaa na shemeji akafungua mlango wa nyuma na kuketi na mimi. Shemeji akaliondoa gari.
“Kwani ilikuwaje?” Dada akaniuliza huku akinitazama kwa macho ya kunihurumia.
Nikamueleza vile ilivyokuwa.
“Yesu wangu! Sasa kama ni jini anakutaka wewe kwa kazi gani?”
“Sijui sasa,” nikamwambia huku nikibetua mabega yangu.
“Siku hizi kumekuwa na matukio mengi ya majini kutongoza binadamu, inatakiwa tahadhari sana,” shemeji akadakia.
“Sasa utamjuaje kuwa huyu ni jini na huyu ni binadamu wakati wanajigeuza kama binadamu?” Dada akamuuliza.
“Ndiyo hivyo, mwanaume akikutongoza mchunguze kwanza hasa ukiona mtu anakupa pesa nyingi, huyo ndiye umtilie mashaka sana.”
“Kweli dunia imekwisha. Zamani matukio ya aina hii hayakuwepo!” Dada akasema.

“Sasa sijui atanifuata tena au ataona nimeshamjua atanipotezea,” nikajisemea.
“Sidhani kama atashughulika na wewe tena, kwa vile umeshamgundua hawezi kukufuata,” dada akaniambia.
“Yaani kama nisingemfuma kule bafuni na kumuona vile alivyo, naona angenifyonza damu leo!”
“Nilivyosikia hawakufyonzi damu bali anakufanya uwe mwanamke wake,” dada akasema.
Nikatazama nyuma ya kioo kuiangalia ile teksi. Sikuiona tena.
“Ashindwe!” nikalaani.
Shemeji akanicheka.
“Lakini umeyataka mwenyewe shemu yangu.”
“Nimeyataka yapi?”
“Hayo yaliyokukuta.”
“Kwani mimi nilijua kama ni jini?”
“Si umechukua pesa zake.”
“Si amenipa mwenyewe?”
“Sasa mbona unamkimbia?”
“We shemeji nawe usinizingue…kwani aliponipa zile pesa nilijua kama ni jini. Au nilimwambia anipe, si alinipa mwenyewe? Tena ashindwe alegee!”
Shemeji akabaki kucheka.
“Sasa nikupeleke nyumbani kwako au…?” akaniuliza.
“Hapana. Leo sirudi nyumbani. Anaweza kunifuata.”
Dakika chache baadaye shemeji akalisimamisha gari mbele ya nyumba waliyokuwa wanaishi.
Tukashuka. Kule kutetemeka sasa kulikuwa kumeisha lakini ile hofu bado nilikuwa nayo ingawa ilipungua kidogo.
Tulipoingia ndani niligundua kuwa wenyewe walikuwa wakijiandaa kula nilipowapigia simu. Wakaacha chakula na kunifuata. Hivyo tulipoingia ndani wakafikia mezani.
“Enjo njoo tule,” dada akaniambia.

Nilikuwa sitaki kula kwa sababu ya ile hofu niliyokuwanayo lakini nikajikaza na kwenda mezani.
Wakati tunakula tulikuwa tukiendelea kuzungumza ile habari ya yule jini huku shemeji akiingiza utani wake ambao sikuupenda.
Baada ya chakula nilikwenda kupumzika kidogo kisha nikaenda kuoga. Mwili wangu ulikuwa umetota kwa jasho.
Saa nne usiku nikaingia katika chumba ambacho ningelala usiku huo. Hata hivyo, nilihisi nisingeweza kupata usingizi kutokana na mawazo ya hofu niliyokuwanayo. Nilijaribu sana kusali, kuomba Mungu ili hofu iniondoke na niweze kupata usingizi.

Kweli nilipata usingizi lakini sikulala sana, nikaamka. Nilipoamka usingizi wote ukaniruka. Sikujua ilikuwa saa ngapi lakini nilihisi ulikuwa usiku mwingi. Nikawa nimelala nikiwa macho. Nilikaa hivyo kwa muda mrefu nikiwaza.
Ghafla mlio wa simu yangu niliyokuwa nimeiweka kwenye kimeza cha mchagoni mwa kitanda ikaanza kuita. Nikaitazama ile simu kabla ya kuiinua na kutazama namba iliyokuwa inapiga. Nikashituka nilipoona namba ya yule mzungu, nikajiambia “Siipokei.” Nikairudisha simu kwenye kimeza.
Simu iliita mpaka ikakakata yenyewe. Baada ya muda kidogo ikaita tena. Nikaishika tena ile simu ili kuona kama ilikuwa namba ileile au nyingine. Nikaona ni namba ileile.
Wakati ule naitazama ile simu, simu hiyo ikajipokea yenyewe. Kwa maneno mengine ni kwamba ilijiunganisha yenyewe ikawa hewani. Nikaisikia ile sauti ya mzungu ikiniuliza. “Kwa nini hupokei simu? Sasa nakuja chumbani kwako!”
Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda siku ya Jumatatu.

Leave A Reply