The House of Favourite Newspapers

Sitasahau Nilivyokumbana na Jini Mwanaume-9

0

ILIPOISHIA IJUMAA:
Nikashtuka nilipoona namba ya yule mzungu, nikajiambia: “Siipokei.” Nikairudisha simu kwenye kimeza.

Simu iliita mpaka ikakakata yenyewe. Baada ya muda kidogo ikaita tena. Nikaishika tena ili kuona kama ilikuwa namba ileile au nyingine. Nikaona ni namba ileile.
Wakati ule naitazama ile simu, simu hiyo ikajipokea yenyewe. Kwa maneno mengine ilijiunganisha yenyewe ikawa hewani. Nikaisikia ile sauti ya mzungu ikiniuliza: “Kwa nini hupokei simu? Sasa nakuja chumbani kwako!”SASA ENDELEA…

Nilipoisikia ile sauti ikiniambia vile, nilishtuka nikaitupa chini kisha nikashuka kitandani na kukimbilia kwenye mlango huku nikipiga kelele.
“Usije! Usije! Usije…!”

Niliufungua mlango nikatoka ukumbuni. Kilichonisitiri ni kuwa nilikuwa nimevaa shumizi ya dada, vinginevyo ningetoka nikiwa mtupu kwani sikukumbuka kuvaa nguo.
Nilipotoka ukumbini nilikimbilia kwenye mlango wa chumba cha dada, nikaanza kuugonga kwa nguvu huku macho yangu yakiwa kwenye mlango wa mbele kwani kama huyo jini angekuja, angetumia mlango huo na ningemuona.

Nikaendelea kuugonga ule mlango huku nikimuita dada.
“Dada! Dada hebu fungua…!”
“Nani… Enjo?” nikaisikia sauti ya dada ikiuliza kutoka chumbani.
“Ndiyo ni mimi dada, nifungulie mlango!”
“Kumetokea nini?” Dada akaniuliza lakini sauti yake ilisikika kwa karibu. Nikajua alikuwa ameshashuka kitandani na yuko karibu na mlango.

Mara mlango ukafunguliwa, dada akatoka.
“Haya kumetokea nini?” Dada akaniuliza akiwa amenitolea macho. Nilikuwa nimemshtua.
Wakati ananiuliza nilikuwa nahema kama niliyekuwa ninafukuzwa. Nikajua ni kwa sababu moyo wangu ulikuwa ukienda kwa kasi kwa sababu ya hofu iliyonipata.

“Yule mzungu si amenipigia simu, sikuipokea. Akapiga tena simu ikajiunganisha yenyewe nikasikia sauti yake ikiniambia: “Kwa nini hupokei simu, ninakuja chumbani kwako!” Ndiyo nikaitupa ile simu nikatoka mle chumbani.” Dada alikunja uso na kuniuliza.

“Unasemaje?”
Nikajua kile kipengele cha simu kujipokea yenyewe ndicho hakukielewa.
Nikamfafanulia.

“Hebu twende huko chumbani kwako,” akaniambia.
Alitangulia yeye kuingia mle chumbani na mimi nikamfuata nyuma.
“Simu hiyo hapo chini,” nikamwambia.

Akainama na kuichukua. Japokuwa niliitupa kioo chake hakikuvunjika na taa yake ilikuwa inawaka ikionesha yule mzungu aliendelea kuwa hewani muda wote niliokimbia.
Bila shaka simu ilikatwa baada ya dada kuichukua pale chini.
“Namba yake ni ipi?” Dada akaniuliza.

Nikamuonesha namba ya yule mzungu. Wakati namuonesha shemeji naye akaingia.
“Kumetokea nini au yule jini amekuja humu chumbani?” akauliza huku akinitazama. Kwa tabia yake kila jambo alitaka kulitilia mzaha.

Mwenzake nilikuwa nimetaharuki na sikumjibu.
Dada ndiye aliyemueleza nilivyopigiwa ile simu na yule mzungu kisha ikajipokea yenyewe.
Shemeji alikuwa anajifanya hajali kitu lakini aliposikia ile habari alishtuka.

“Naona kama anataka kukutisha tu lakini sidhani kama anaweza kuja humu ndani,” akaniambia.
“Kwa nini? Jini ni jini, anaweza kuja. Yeye ameshakusudia kumtesa mdogo wangu,” dada akasema.
“Sasa atalala vipi?”

“Mimi silali tena humu chumbani peke yangu,” nikawaambia.
“Basi lala naye,” shemeji akamwambia dada.
“Kwanza twendeni tukakae sebuleni,” nikawaambia kwa vile wakati ule usingizi ulikuwa umeniruka.
Tukaenda kukaa sebuleni. Muda ule ilikuwa ni saa tisa usiku. Tukazungumza hadi saa kumi. Shemeji akaanza kusinzia. Baadaye nikamuona dada naye yuko kimya. Nikajipa moyo kwamba kutakucha muda si mrefu.

Baadaye na mimi nikapitiwa na usingizi hapohapo, nikalala.
Dada ndiye aliyeniamsha kukiwa kumeshakucha.
“Nenda kalale chumbani,” akaniambia.

Nilipotupa macho, shemeji alikuwa ameshaondoka. Nikainuka na kuingia chumbani. Wakati naingia tu chumbani, simu yangu ikaita. Kwa kweli nilishtuka kwa kudhani kuwa ni yule jini.
Nilipotazama skrini ya simu nikaona jina la Eddy, mpenzi wangu aliyekuwa masomoni Uingereza.

Je, kilifuatia nini? Usikose mwendelezo wake katika Gazeti la Ijumaa siku ya Ijumaa.

Leave A Reply