The House of Favourite Newspapers

Sitta Achaguliwa Meya Kinondoni

bensitta2

DIWANI wa Kata ya Msasani katika Manispaa ya Kinondoni, Benjamin Sitta amechaguliwa kuwa Meya mpya wa manispaa hiyo katika uchaguzi wa vuta nikuvute, uliofanyika kwenye Ukumbi wa Manispaa hiyo, Magomeni jijini Dar es Salaam jana. Uchaguzi wa Meya mpya wa Manispaa hiyo, umekuja baada ya wilaya hiyo kugawanywa na kuwa na wilaya mbili za Kinondoni na Ubungo.

Awali, Meya wa Kinondoni alikuwa akitokea Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambaye ni Diwani wa Ubungo, Boniface Jacob. Sitta ambaye aligombea nafasi hiyo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) alishinda kiti hicho baada ya kuwashinda wapinzani wake, Mustafa Muro wa Chadema na Jumanne Mbunju wa CUF kwa jumla ya kura zote 18 za wajumbe wa CCM.

Nafasi ya Naibu Meya ilikwenda kwa Diwani wa Kata ya Kigogo, George Manyama pia wa CCM, baada na yeye kupata kura zote 18 zilizopigwa na wajumbe hao.

Hata hivyo, uchaguzi huo ulikuwa wa vuta nikuvute baada ya wajumbe wa vyama viwili vya upinzani, Chadema na CUF kuususa baada ya kutaka wajumbe wao wawili, ambao hawakuwa wakazi wa manispaa hiyo kutaka kupiga kura ambao ni Salma Mwasa na Suzane Lyimo, wote wa Kimara.

Akitangaza matokeo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Kinondoni, Aron Kagoromjuli alisema Sitta na Manyama wameshinda kihalali baada ya kupigiwa kura na wajumbe katika uchaguzi halali, licha ya wajumbe wengine kususia uchaguzi huo na kuwapa tahadhari ya kuwafuta kwenye nafasi zao endapo hawataingia kwenye vikao vitatu vya baraza na kutangaza uchaguzi tena katika kata zao.

“Sasa namtangaza Ndugu Benjamin Sitta kuwa mshindi wa nafasi ya Meya baada ya kushinda kwa kura zote 18 kati ya kura 18 zilizopigwa na hakuna kura iliyoharibika. Pia namtangaza Ndugu George Manyama kuwa Naibu Meya mpya wa Manispaa hii baada ya kushinda kwa kura 18 kati ya kura zote zilizopigwa,” alisema Kagoromjuli.

“Nitoe tu tahadhari kwa wajumbe hawa waliosusa uchaguzi huu kuwa endapo hawatahudhuria vikao vitatu vya baraza tutawafuta na tutaitisha uchaguzi tena kwenye kata zao.”

Uchaguzi huo ulihudhuriwa na wajumbe mbalimbali mashuhuri wakiwemo Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako.

Wengine ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki. Baada ya kususa mkutano huo wa uchaguzi, Chadema walisema kwamba leo watafungua mashtaka kulalamikia uchaguzi huo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu Mkuu wa Chadema, Vincent Mashinji alisema Chadema inaenda mahakamani kupinga uchaguzi huo pamoja na mchakato wake mzima kwani haukufuata sheria na kanuni zinazoongoza uchaguzi wa viongozi wa halmashauri.

“Hatukwenda kwenye uchaguzi kudai kushinda, lakini tunapigania haki kufuatwa, sheria na kanuni zinazolinda chombo kile hazikufuatwa, tutakutana mahakamani,” alisema Mashinji.

Alieleza kuwa wanakusanya ushahidi ilionao wote na kwenda nao mahakamani na kwamba kuanzia sasa chama hicho, hakitakuwa chama cha kulalamika tena.

Mashinji alisema barua za taarifa za kikao hicho, ambacho kilifanya uchaguzi huo ziliwafikia wajumbe Oktoba 21, mwaka huu saa tatu usiku; hata hivyo juzi wajumbe wa upande wa Chadema, walimuandikia Mkurugenzi wa Kinondoni kulalamikia kitendo hicho na kuomba iahirishwe.

“Mkurugenzi alikataa kupokea barua hiyo akidai kuwa siku hiyo ilikuwa Jumamosi siku ambayo siyo ya kazi wakati yeye barua za mwaliko alisambaza usiku wa Ijumaa ambao pia haukuwa muda wa kazi, na ni siku moja na nusu kabla ya uchaguzi,” alisema Mashinji.

Alisema uchaguzi huo uliofanyika na kuwapata Meya na Naibu wake ni batili, kwani Chadema haiutambui kwa sababu baadhi ya wajumbe waliofanya uchaguzi wengi wao hawakustahili kwa sababu siyo wakazi wa Kinondoni.

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee alisema uchaguzi uliofanywa ni batili na kwamba wamejifurahisha tu kufanya uchaguzi. Alisema “wamejifurahisha tu, uchaguzi mzima walioufanya ni batili… sisi tunakwenda mahakamani na tunaamini mahakama itatenda haki.”

Alisema sheria za Serikali ya Mtaa zinasema idadi ya wajumbe, aina ya wajumbe wanaostahili kushiriki kupiga kura, lakini havikufuatwa, badala yake alidai CCM imeongeza wajumbe wake wanne batili, ambao ni pamoja na Profesa Ndalichako na Dk Tulia ambao siyo wakazi wa Kinondoni na wajumbe halali wa Chadema kuondolewa.

Wakati huo huo, uchaguzi wa kumpata Meya na Naibu Meya wa Manispaa ya Ubungo, umeahirishwa baada ya madiwani wa Chadema kususa uchaguzi huo kwa madai hawakupewa taarifa mapema.

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alisema uchaguzi huo unatakiwa kutolewa taarifa ya siku saba kabla. Alisema Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo, John Kayombo alipaswa kutoa taarifa mapema na siyo siku mbili kabla, kama alivyofanya.

“Uchaguzi hautafanyika, tumekataa na hii tunataka Rais ajue mambo haya wanayotaka kufanya katika uchaguzi huu, ingawa tayari tumeshashinda,” alidai Mnyika.

Mgombea umeya wa upande wa Chadema kwa nafasi ya Meya ni Boniface Jacob, ambaye ni diwani wa Ubungo. Imeandikwa na Fadhili Akida na Regina Kumba.

Comments are closed.