The House of Favourite Newspapers

SKENDO MAFUTA YA UPAKO

0

MWANGWI wa mafuta ya upako bado unavuma kila uchwao, skendo za kila aina zinazungumzwa, Uwazi linakuhabarisha.  Uchunguzi unaonesha kuwa wapo baadhi ya watu wakiwemo wachungaji wa makanisa mbalimbali wametaja mafuta hayo kuwa na nguvu za kichawi, jambo ambalo watumishi wengine wa Mungu wamekuwa wakipinga vikali. Mtazamo huo tofauti wa wachungaji, sasa umefika mbali kiasi cha kuleta majibizano yanayoambatana na lugha za matusi.

KISIKIE CHANZO CHETU

Chanzo makini ambacho ni mmoja wa manabii hao ambaye aliomba hifadhi ya jina, aliliambia UWAZI kuwa sasa hivi kuna vita nzito kati ya manabii na mitume kuhusiana na mambo ya kiroho na nafasi zao za kichungaji.

“Kuna ugomvi mzito kati ya Mtume Bethania Saimon ‘Jiwe la Yesu’ ambaye ni mchungaji wa Kanisa la Neema ya Kitume (AMG) lililopo Mbezi- Luis jijini Dar, Mtume na Nabii Peter Nyaga kutoka Kanisa la RGC Miracle Center Dar, Mtume wa Kanisa la Rehoboth International Ministry, Martin Bashando Shaboka na Joackim Kimanza ambaye ni rais mteule wa mitume na manabii.” Chanzo kilisema.

UGOMVI ULIANZIA HUKU

Kupitia kwenye group la WhatsApp, Mtume Nyaga na Mtume Bashando walipeana maneno makali ya matusi ambapo sauti zao zilinaswa na gazeti hili na kutaja ambayo hayaandikiki gazetini, lakini mwandishi wetu alitaka kujua kulikoni.

Baada ya kupata ushahidi wa sauti hizo za kutukanana, Uwazi lilimsaka Mtume Bashando ambaye alikiri kuwepo kwa mgogoro huo na kwamba ni kweli kuwa walitoleana maneno hayo machafu.

Akieleza kwa undani, Bashando alisema awali Mtume Nyaga aliunda Group la WhatsApp na kuwaunga watumishi walioko karibu naye na kuanza kujiita yeye ndiye rais wa mitume na manabii Tanzania, jambo ambalo alidai kuwa si la kweli. “Kwa kutumia nafasi hiyo aliyojipachika mwenyewe, aliweza kwenda sehemu mbalimbali na kusema ndiye rais. Hivyo, watu wakiwemo watumishi wenzetu wa Mungu, walimuamini.

“Cha kushangaza alikwenda kwa Askofu Mkuu Kakobe (Zachary wa kanisa la Full Gospel Bible Fellowship) na kumueleza kuwa yeye ndiye rais wa mitume na manabii na kumwambia kuwa kuna baadhi ya wachungaji wanatumia uchawi kwenye huduma zao.

“Kauli hiyo imemfanya Askofu Kakobe kuanza kuwasema wachungaji wenzake hasa mitume na manabii kuwa wanatumia nguvu za giza kufanya miujiza.

“Kutokana na maneno hayo ya uongo kwa Askofu Kakobe, wazee ilibidi wamuite Nyaga na kumvua uongozi aliojipachika na kutengeneza uongozi mpya halali. “Wazee walimteua Maboya (Dustan) kuwa mlezi wa mitume na manabii nchini kwa sababu Nyaga mbali na kupoteza sifa nyingine kwamba yeye si raia wa Tanzania, yeye ni Mkenya,” alisema Bashando.

MSINGI WA MVUTANO NI NINI?

Uchunguzi unaonesha kuwa msingi wa mvutano kati ya wachungaji hasa wa makanisa ya kiroho ni huduma zao za maombezi huku nyuma yake ikiwa ni kugombea waumini.

Baadhi ya makanisa yamekuwa yakitumia huduma za maombezi na uponyaji kuvutia waumini kwa kutumia vitu yakiwemo mafuta ya upako, jambo ambalo limewafanya wachungaji wengine wasiotumia staili hiyo ya maombi kuibuka na kusema kuwa aina hiyo ya maombezi imejaa nguvu za giza.

Mara kadhaa katika mahubiri yake, Askofu Kakobe amekuwa akiwaasa waumini wake kuwa makini na maombezi hayo kwa madai kuwa yanakiuka misingi ya imani aliyoacha Nabii Yesu. “Wanangu, siku za mwisho wataibuka manabii wa uongo, jihadharini nao, Wakristo tumeachiwa jina moja tu linaloweza kutuponya nalo ni jina la Yesu, siyo mafuta ya upako, bangili, maji, keki wala chumvi,” alisema Kakobe katika moja ya mahubiri yake kanisani mwake.

Hata hivyo, hivi karibuni Askofu Josephat Gwajima ambaye ni swahiba wa Askofu Kakobe, aliibuka na kusema kuwa maombezi kwa njia ya mafuta ya upako si haramu kwa kuwa yalitumika hata zama za wanafunzi wa Yesu. Kauli hiyo ilikuja baada ya kuzuka kwa sintofahamu kuhusu watu 20 kufariki dunia walipokuwa wakigombea kukanyaga mafuta kwenye ibada ya maombezi iliyofanywa na Nabii Mwamposa mjini Moshi hivi karibuni.

MADAI MENGINE MAFUTA YA UPAKO

Kumekuwa na madai mengi kuwa mafuta yanayoitwa ya upako wanayotumia baadhi ya mitume na manabii kutibu watu, yanachanganywa na vitu vinavyoaminika kuwa na nguvu za kichawi. Madai hayo yamekuwa yakipuuzwa na baadhi ya wachungaji wanaotoa huduma hiyo na kuyaita kuwa yanatokana na wivu wa mafanikio ya kiroho.

“Hakuna uchawi wala nini, wanaosema ni uchawi wameishiwa nguvu za Kimungu na wanaona waumini wao wanawakimbia, kwa hiyo ili kujilinda wasibaki peke yao kwenye makanisa, wameamua kuyavika mafuta hayo mambo ya uongo.

“Kuna wivu wa huduma, siwezi kuzungumza sana kwa sababu tukio (la watu kufa kwenye mahubiri) bado linachunguzwa,” alisema Mchungaji Mwamposa katika mahubiri yake ya Jumapili iliyopita kwenye Viwanja vya Tanganyika Packers jijini Dar es Salaam.

Leave A Reply