Snura: Mapenzi Nimeyaweka Pembeni, Hapa Kazi Tu

BAADA ya kuvunjika kwa uhusiano wake na mwanamuziki mwenzake, Minal Calypto uliosababisha apotee kabisa kwenye gemu, msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Snura Mushi ameibuka na kueleza kuwa kwa sasa ameamua kuweka mapenzi pembeni kwa kuwa yanampotezea muda.

 

Akizungumza katika mahojiano maalum na Showbiz, Snura alisema kutokana na kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi, alijikuta akipoteza muda mwingi na kushindwa kuendelea kufanya vizuri kwenye muziki ambapo kwa sasa ameamua kuachana na mapenzi kabisa.

 

Alisema kwa sasa yupo singo na anawalea watoto wake wawili aliojaaliwa na kufanya kazi yake ya muziki pamoja na biashara zake ndogondogo.

Snura amezungumza mengi, ungana naye katika maswali na majibu hapa chini;

Showbiz: Uko kimya sana kwenye muziki, nini tatizo?

Snura: Mambo tu yalikuwa mengi pia huwezi kutoa ngoma kila wakati, zitachuja.

Showbiz: Kuna tetesi kwamba umesahaulika kwenye muziki kwa sababu ya mapenzi, hili likoje?

Snura: Siyo kweli kwa sababu kwa sasa nilishaachana na mapenzi kabisa, niko nawalea wanangu na kuandaa ngoma kali. Mashabiki wakae tu mkao wa kula.

Showbiz: Baada ya kuachana na Minal, kwa sasa uko kwenye uhusiano wa kimapenzi na nani?

Snura: Kwa sasa sina mpenzi, niko singo. Nipo tu nawalea watoto wangu maana nimeamua kupumzika maana kwenye mapenzi hakuna faida yoyote.

Showbiz: Kuna tetesi kwamba aliyekuwa mpenzi wako, Minal alichukua nyota yako ndiyo maana usikiki tena kimuziki, hili likoje?

Snura: Achukue nyota yangu kupeleka wapi? Hilo siwezi kulizungumzia maana silifahamu kabisa.

Showbiz: Wasanii wengi wanapenda sana kiki ili kazi zao ziwe hot, unazungumziaje hilo?

Snura: Niwaambie tu kwamba kama kiki inafanikisha mambo yao wafanye tu kwa sababu kila mtu anatafuta mafanikio yake.

Showbiz: Kwa upande wako kwa nini hufanyi kiki ili muziki wako uwe juu?

Snura: Huwa sipendi tu mambo hayo, nitafanyia kazi hilo nikiona kiki zinalipa basi mwaka huu nitajaribu kufanya.

Showbiz: Tofauti na muziki, unajishughulisha na nini kingine?

Snura: Nafanya biashara ndogondogo tu.

Showbiz: Umejipangaje kimuziki kwa mwaka huu wa 2020?

Snura: Mashabiki zangu wakae tayari kupokea kazi nzuri na bora kutoka kwangu.

Showbiz: Una mpango wa kufanya kolabo na wasanii wa nje ya Bongo?

Snura: Bado sijafikiria, nina mpango wa kuendelea kufanya kolabo za hapahapa Bongo.

Showbiz: Vipi kwa sasa una meneja?

Snura: Sina meneja, kazi zangu nazisimamia mwenyewe.

Showbiz: Ni ngoma gani iliyokufanya ujulikane kwenye muziki?

Snura: Ngoma ya Majanga ambayo nilitoa 2013, ndiyo iliyonitambulisha kwenye ulimwengu wa muziki.

Showbiz: Wadada wengi wanakimbilia nje ya nchi kula bata, vipi wewe hujawahi kupata fursa hiyo?

Snura: Fursa nazipata sana tena sana ila mimi ukiona naenda nje ya nchi ujue naenda kwenye shoo, vinginevyo siendi hata mtu akiniita huwa nauliza kuna kazi? Kama hakuna kazi naenda kufanya nini sasa jamani.

Showbiz: Wewe ni mwanamke mrembo ambaye una sifa zote za kuitwa mwanamke, vipi usumbufu wa wanaume wakware ukoje?

Snura: Nilishawazoea, yaani kwangu naona kama si changamoto tena naona ni kitu cha kawaida sana maana huwezi kumzuia mtu asikutamani na akishakutamani si basi ukikubali ni wewe mwenyewe ila kwa upande wangu kwa kweli nawakwepa sana maana sitaki kuleta mtafaruku.

Showbiz: Neno lako la mwisho kwa mashabiki wako ni lipi?

Snura: Nawapenda sana mashabiki zangu, nawaomba waendelee kunisapoti kwa kazi zangu maana bila wao mimi siyo kitu.

Showbiz: Ahsante Snura kwa ushirikiano.

Snura: Karibu sana.

STORI: KHADIJA BAKARI

Toa comment