The House of Favourite Newspapers

SPORTPESA CUP… ITAKUWA NA MAJIBU YA KISASI

Kikosi cha timu ya Yanga.

MABINGWA watetezi wa Tanzania Bara Simba, pamoja na Yanga, Singida United pamoja na JKU ndiyo wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Kombe la SportPesa Super Cup.

Michuano ya SportPesa Super Cup 2018, inaanza kuunguruma leo hadi Juni 10, mwaka huu katika Uwanja wa Afraha mjini Nakuru, Kenya inasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini Kenya.

 

Kuna kitu kimoja kinavutia kwamba kuna timu mbili zinashiriki michuano hiyo tayari ziko katika hatua ya Makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika. Hawa ni Yanga na Gor Mahia.

 

Timu hizo mbili ni sehemu ya lulu ya Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na inaonyesha si michuano lelemama kuwa na washiriki wenye uwezo mkubwa kama huo.

Kikosi cha timu ya Simba.

Wakati unaangalia hilo la ushindani wa kuwa na timu zinazoshiriki michuano mikubwa ya Caf lakini unaona kuna mabingwa wa Tanzania Bara kama walivyo mabingwa wa Kenya kwa kuwa timu zote mbili kongwe za Kenya, Gor Mahia na AFC Leopards, zinashiriki.

 

Lakini, kuna suala la ushindani kwa nchi kwa kuwa kuna jumla ya timu nane, hizo nne za Tanzania lakini nne za Kenya ambazo ni Gor Mahia, AFC Leopards, Kakamega Homeboys na Kariobangi Sharks.

 

Hapa linakuja suala la timu ipi au kutoka nchi ipi, Kenya au Tanzania itakuwa bingwa? Tanzania itaweza kulipa kisasi baada ya kunyanyaswa katika ardhi yake mashindano yaliyopita.

 

Mashindano hayo yalianzishwa Tanzania Juni, mwaka jana. Lakini fainali ikawa ni “Made in Kenya”, pia ikawa derby ya Nairobi ndani ya Dar es Salaam baada ya Gor Mahia na AFC Leopards kukutana.

Vikosi vya Simba na Yanga, havikuonyesha umakini na nia ya kufanya vema katika michuano hiyo ambayo hakika ina zawadi nono na ya juu ukilinganisha na michuano mingine inayochezwa kwa muda mfupi.

 

Pamoja na zawadi nono, bingwa wa msimu uliopita, Gor Mahia walipata nafasi ya kucheza dhidi ya Everton kutoka England iliyoongozwa na mchezaji nyota wa England, Wayne Rooney.

 

Tanzania inatakiwa kuonyesha hawakujua umuhimu wa michuano hii hapo awali. Safari wakiwa Kenya nao waonyeshe inawezekana ili kufanya vema na kuibuka na ubingwa.

 

Soka la Tanzania kwa sasa, kwa upande wa ligi ina ligi bora zaidi ya ile ya Kenya. Dharau ya kuona ni michuano isiyo na faida, ilisababisha timu za Tanzania kuonekana ziko ugenini licha ya kwamba zilikuwa nyumbani.

 

Lakini safari hii zina nafasi, hata kama kuna baadhi ya nyota wamebaki jijini Dar es Salaam au kurejea kwao nje ya Tanzania, lakini vikosi vilivyo kwa ajili ya mashindano hayo, ni bora kuliko vile vya msimu uliopita.

 

Mashindano haya sasa yameshika hatamu kwa ubora na wawakilishi wa Tanzania wana nafasi nzuri kuonyesha walikosea kwa kuwa hata Singida United watakuwa na wachezaji wapya lakini wataendelea kujenga kikosi chao kama ilivyo kwa JKU.

 

Yanga ambayo angalau mashindano yaliyopita ilipiga hatua kuliko Simba, itafungua mashindano hayo kwa kumenyana na Kakamega Homeboys ya Kenya.

 

Mchezo huo umepangwa kuanza saa 7:00 mchana, huku Gor Mahia ambayo nayo ni ya Kenya ikipambana na JKU ya Zanzibar kuanzia saa 9:15 alasiri. Mechi hizo zote zitachezwa Juni 3.

 

Simba ya Tanzania, wao watacheza kesho dhidi ya Kariobangi Sharks ya Kenya mchezo utakaopigwa majira ya saa 9:00 alasiri ambapo siku hiyo itachezwa mechi hiyo pekee.

Michuano hiyo itaendelea Juni 5, AFC Leopards itakutana na Wazee wa Alizeti, yaani Singida United ambao bado wana nafasi ya kufanya vizuri.

 

Kikubwa kabisa, waamuzi wanapaswa kuwa makini ili kuepuka kuvuruga burudani ambayo itakuwa na upinzani uliojaa kutaka kulipa kisasi.

 

Timu za Tanzania zingependa kukutana fainali, lakini zile za Kenya nazo zingependa kuendeleza ubabe dhidi ya jirani zao kwa kuendelea kufanya vizuri.

Utajiuliza, kweli hilo litawezekana Wakenya kuendelea kuifanya SportPesa Super Cup mali yao? Leo kazi inaanza na majibu yatapatikana.

RATIBA LIGI YA SPORTPESA

Jumanne, Juni 3, 2018

K akamega v Yanga

7:00 MCHANA

Gormahia v JKU

9:15 ALASIRI

Jumatatu, Juni 4, 2018

Kariobangi v Simba

9:00 USIKU

Jumanne, Juni 5, 2018

Leopads v Singida

9:00 ALASIRI

ZAWADI

Bingwa: Sh68mil.

Mshindi wa 2: Sh 22mil.

Mshindi wa 3: Sh17mil.

Comments are closed.