The House of Favourite Newspapers

StarTimes waadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa namna hii

Mmoja wa wafanyakazi wa Star Media Group, Joan Usiri (kulia) akimkabidhi misaada mbalimbali Katibu Mtendaji wa Kituo cha Kulea Watoto Yatima na Wasio na Makazi Maalum (Chakuwama), Hassan Hamis wakati wafanyakazi hao walipotembelea kituo hicho leo Ijumaa katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.
Wakiwa katika picha ya pamoja.
Wafanyakazi wa Star Media Group.
Msimamizi wa kituo akizungumza jambo.

 

BAADHI ya wafanyakazi wa Kampuni ya Star Media Group inayomiliki King’amuzi cha StarTimes, leo wameadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa kutembelea Kituo cha Kulea Watoto Yatima na Wasio na Makazi Maalum (Chakuwama) kilichopo Sinza jijini Dar.

 

Wakiwa kituoni hapo, wafanyakazi hao walikabidhi misaada mbalimbali ikiwemo mchele, sabuni, magodoro na juisi.

 

Akizungumza wakati wa kukabidhi misaada hiyo, mmoja wa wafanyakazi hao, Joan Usiri, alisema wameamua kufanya hivyo ikiwa ni sehemu ya kuwakumbuka watoto hao ambao wamepoteza mapenzi ya wazazi wao wakiwa na umri mdogo.

 

“Sisi kama wafanyakazi wa Star Media, tumeona leo katika Siku ya Wanawake Duniani tuwakumbuke watoto kama hawa ambao wanahitaji mapenzi ya wazazi wao, lakini wameyakosa wakiwa na umri mdogo sana.

 

“Tumewaletea magodoro, sabuni, juisi na vitu vingine mbalimbali. Tutaendelea kufanya hivi katika kugusa mioyo ya jamii inayotuzunguka,” alisema.

 

Naye Katibu Mtendaji wa (Chakuwama), Hassan Hamis, aliwapongeza wafanyakazi hao kwa kitendo hicho huku akiwataka wengine kuiga mfano huo kwa kuwakumbuka watoto wanaoishi kwenye mazingira kama hayo.

 

Kwa mujibu wa katibu huyo, kituo hicho kilichoanzishwa mwaka 1998, hivi sasa kina watoto 68 kuanzia umri wa miaka miwili mpaka 18 na wapo ambapo wanasoma shule mbalimbali ikiwemo za serikali na za watu binafsi.

 

Comments are closed.