The House of Favourite Newspapers

Straika Mcongo anatua Simba SC

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Nkana FC ambaye amejiunga na Al Hilal ya Sudan, Idriss Mbombo raia wa DR Congo, ameingia kwenye rada za mabosi wa Simba na muda wowote kuanzia sasa mchakato wa kumsajili utaanza.

 

Mbombo ambaye msimu uliopita akiwa na Nkana alimaliza ligi akiwa na mabao 20, amesajiliwa na Al Hilal kuwa mbadala wa Mtanzania, Thomas Ulimwengu aliyeachana na timu hiyo miezi michache iliyopita.

 

Taarifa ambazo Championi imezipata kutoka hapa Zambia ambapo Simba imekuja kucheza na Nkana FC, ni kwamba mshambuliaji huyo amependekezwa na kiungo wa Simba, Claytous Chama raia wa Zambia.

 

Chama anamfahamu vizuri mshambuliaji huyo kutokana na msimu uliopita kucheza wote ligi ya Zambia. Chama alikuwa Power Dynamo kabla ya msimu huu hajatoa Simba.
Kwa mujibu wa mtoa habari wetu, mshambuliaji huyo atajiunga na Simba pindi timu hiyo ikifuzu makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika au mwishoni mwa msimu huu.

 

“Mbombo anaweza kusajiliwa na Simba kwa sababu Chama amesema ni mshambuliaji mzuri na anaweza kuwa msaada kwenye safu yetu ya ushambuliaji.
“Hivi sasa anacheza Al Hilal ya Sudan na msimu uliopita akiwa Nkana, alifunga mabao 20 na kushika nafasi ya pili kwa ufungaji.

 

“Tunasubiri tufuzu makundi ndiyo tumuongeze kikosini lakini hata hivyo tunaweza kumsajili mwisho wa msimu,” kilisema chanzo hapa Zambia.
Hata hivyo, baadhi ya mashabiki wa Nkana waliozungumza na Championi, wamesema kuwa Mbombo ni bonge la mshambuliaji na kama angekuwepo kwenye mechi dhidi ya Simba, basi wangeshinda mabao mengi.

 

Ikumbukwe kuwa, Nkana na Simba juzi zilicheza mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika Hatua ya Kwanza na Nkana kuibuka na ushindi wa mabao 2-1. Timu hizo zitarudiana Jumapili ijayo na mshindi wa jumla atafuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo. Viongozi wa Simba walipotafutwa jana kuzungumzia habari hii, simu zao za mkononi zilikuwa hazipatikani.

IBRAHIM MUSSA, Kitwe

ZAHERA: WASINGEKUWA MASHABIKI NINGESEPA YANGA, VIONGOZI WANAZINGUA – VIDEO

Comments are closed.