The House of Favourite Newspapers

Straika mpya Yanga afunguka atakavyomweka benchi Chirwa

MSHAMBULIAJI mpya wa Yanga, Yohana Nko­mola, amefunguka kuwa atahakikisha anapambana na washambuliaji wa timu hiyo ak­iwemo, Mzambia Obrey Chirwa ili kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza.

Mshambuliaji huyo amejiunga na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili akitokea katika Academy ya Cambiaso licha ya mapema mwaka huu kufanya majaribio kwenye timu ya vijana ya Etoile Du Sahel ya nchini Tunisia.

Nkomola amesema kuwa anatambua Yanga ni timu kubwa hivyo kujituma kwake ndiyo sehemu ya kuweza kufikia ndoto zake kwenye timu hiyo kwa kuhakikisha anapata nafasi kwenye kikosi cha kwanza kinachonolewa na kocha Mzambia, George Lwandamina.

“Kujiunga na Yanga kwangu ni hatua kubwa sana, siwezi kuichezea hii nafasi kwa sababu Yanga ni timu kubwa hapa nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki, sasa lazima nijitume ili kuweza kuonyesha thamani yangu kwao ili kuweza kutimiza ndoto zangu.

“Kitu kikubwa ambacho nakiona mbele yangu ni kuhakikisha najituma ili mwalimu aweze kunipa nafasi kwenye kikosi cha kwanza licha ya kwamba natambua kwamba kuna wachezaji wazuri na wenye uzoefu mkubwa zaidi yangu katika nafasi ya ushambuliaji ila nitapambana ikiwezekana nicheze wengine wasubirie,” alisema Nkomola ambaye ni mshambuliaji wa Kilimanjaro Stars katika michuano ya Chalenji inayoendelea nchini Kenya.

Ibrahim Mussa, Dar es Salaam

Comments are closed.