The House of Favourite Newspapers

SUMA JKT YASAINI MKATABA KULINDA MAJENGO NA VIFAA VYA TTCL NCHI NZIMA

Mkuu wa TTCL Corporation, Bw. Waziri Kindamba (kulia) akizungumza katika hafla ya kutiliana saini na kampuni ya SUMA JKT kuingia makubaliano ya kulinda Majengo, mali na Miundo mbinu ya kampuni ya TTCL Corporation. 

SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania – TTCL Corporation limeikabidhi kandarasi ya Ulinzi wa Majengo, mali na Miundo mbinu yake kwa SUMA JKT, Kampuni Tanzu ya Jeshi la kujenga Taifa kwa mkataba wa mwaka mmoja kuanzia Juni 01 2018.

Hafla ya utiaji saini Makubaliano hayo imefanyika leo katika Makao Makuu ya Shirika la Mawasiliano Tanzania- TTCL Corporation na kuhudhuriwa na Viongozi waandamizi wa taasisi hizo mbili na watendaji wa Idara mbali mbali.

Mkuu wa TTCL Corporation, Bw. Waziri Kindamba (kulia) pamoja na mwakilishi wa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa -JKT, Kanali Aristides Rutta (kushoto) wakisaini mkataba wa kampuni ya SUMA JKT kulinda Majengo, mali na Miundo mbinu ya kampuni ya TTCL Corporation.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Corporation Bw. Waziri Kindamba amesema, TTCL ina furaha kubwa kushirikiana na SUMA JKT katika jukumu hili nyeti la Ulinzi na Usalama wa Majengo, Mali na Miundo mbinu yake.

“Tuliwapa SUMA JKT kazi ya Ulinzi katika Makao Makuu ya Shirika letu na katika Kituo cha Kimataifa cha kutunzia Kumbukumbu(NIDC) kilichopo Kijitionyama Dar Es salaam. SUMA JKT wamefanya kazi yao kwa Weledi, nidhamu na ufanisi mkubwa, ndio maana leo tunayo furaha kuwakabidhi jukumu kubwa zaidi la kutulinda katika Ofisi zetu Nchi nzima.”

Mkuu wa TTCL Corporation, Bw. Waziri Kindamba (kulia) pamoja na mwakilishi wa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa -JKT, Kanali Aristides Rutta (kushoto) wakibadilishana nyaraka za mkataba. 

Bw. Kindamba amesema, TTCL Corporation ni Shirika jipya la Mawasiliano Tanzania ambalo limechukua nafasi ya iliyokuwa Kampuni ya Simu Tanzania TTCL LTD. Miongoni mwa majukumu mahsusi ya TTCL Corporation ni kuchochea kasi ya ukuaji wa Uchumi,  kusimamia maendeleo ya Sekta ya Mawasiliano kwa kuwaunganisha Wananchi wote, kusimamia ufanisi wa Miundombinu ya Kimkakati ya Mawasiliano kwa niaba ya Serikali,  kusaidia shughuli za Ulinzi na Usalama wa Nchi, Huduma za Jamii na ukuaji wa Sekta nyingine zote.

 

“Hii ni TTCL mpya ambayo imedhamiria kuwahudumia Wananchi kwa Viwango vya hali ya juu. Tutaweza kutimiza vyema wajibu huo tukiwa na uhakika katika ulinzi na usalama wa Watendaji wetu, mali zetu na Miundombinu yetu ambayo ni muhimu sana kwa Ulinzi na Usalama wa Nchi, amesema.”

Picha ya pamoja ya maofisa wa TTCL Corporation na SUMA JKT mara baada ya hafla hiyo iliyofanyika Makao Makuu ya TTCL Corporation jijini Dar es Salaam.

 

Akizungumza kwa Niaba ya Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa -JKT, Kanali Aristides Rutta amesema, licha ya Nidhamu na Ujuzi wa Kijeshi walio nao vijana wake, Kampuni hiyo inajivunia mafunzo na vifaa vya kisasa vya kufanyia kazi, rekodi iliyotukuka katika utekelezaji wa miradi ya Wananchi na nyenzo za Ulinzi na Usalama walizonazo.

“Tunalishukuru sana Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL kwa Imani kubwa waliyotupa, tunawakikishia utendaji uliotukuka kwa uzalendo wa hali ya juu wakati wote wa kutimiza majukumu yetu katika kandarasi hii.

SUMA JKT imepata umaarufu mkubwa Nchini hasa baada ya kutekeleza kwa mafanikio kandarasi mbali mbali katika Sekta za Ulinzi na Ujenzi wa Miundombinu katika maeneo mengi Nchini.

Comments are closed.