The House of Favourite Newspapers

Sumaye Aanika Mazito Serikali Kumnyang’anya Mashamba Yake

0
Frederick Sumaye.

Waziri  Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye amevunja ukimya na kusema  kwamba watawala wanaendesha nchi  kwa visasi ndiyo maana tangu ahame Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) amezidi kuandamwa  ikiwamo kunyang’anywa mashamba anayoyamiliki kihalali.

 
Sumaye ambaye kwa sasa ni  Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani  Chadema, amesema tangu ajiunge na upinzani amekuwa akikumbana na vikwazo vingi, ikiwamo kudhauliwa pamoja na  kuporwa mashamba yake kwa kisingizio kwamba ameshindwa kuyaendeleza.
 
Amemtuhumu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kwamba anajua ukweli kuhusu mashamba yake lakini hataki kuusema kwa kuwa ametumwa na mkubwa wake.
 
Ametaja mashamba aliyoporwa kuwa ni lile la Mvomero mkoani Morogoro na lililopo Mabwepande katika wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, ambayo yote serikali imefuta hati za umiliki wake.
 
Amesema shamba la Mvomero linamilikiwa na mke wake Ester Sumaye ambalo lina ukubwa wa hekari 326, na kwamba huko alikuwa anafuga ng’ombe zaidi ya 200, kondoo 300, ghala la kuhifadhia chakula, trekta na nyumba mbili za kudumu.
 
Sumaye akizungumza na waandishi wa habari leo katika  ofisi za makao makuu kanda ya Pwani  (Chadema), amesema mgogoro huo ulianza mara baada tu ya yeye kuhamia upinzani.
 
Amesema muda wote aliokuwa ndani ya CCM,  hakuwahi kuwa na mgogoro wowote na serikali wala kusumbuliwa kuhusu mali zake yakiwamo mashamba.
 
“Mara baada tu ya mimi kuhama wapo viongozi waliodiriki kusema huyu Sumaye dawa yake ni kumfilisi kwa kumnyang’anya mashamba, kama moja ya kunikomoa tu, hivyo ni dhahiri kuwa ni uadui kati ya serikali na mimi kwa sababu ya kuhamia upinzani.” amesema Sumaye.
 
“Mashamba hayo wanadai wameamua kuninyang’anywa kwa kuwa siyalipii kodi na kutoendelezwa hivyo yanatakiwa kuchukuliwa na kuwagawia wananchi kitu ambacho si weli kwani shughuli za kilimo katika mashamba hayo zilikuwa zikiendelea kama kawaida.”
 
Sumaye amemtaka, Lukuvi kutumia nafasi yake vizuri kwani kwa kuendeleza uadui wa kisiasa hakuwezi kulisaidia taifa badala yake kutazidi kukandamiza demokrasia hapa nchini.
 
Sumaye ameionya serikali ya awamu ya tano na kuitaka iache  kulipa visasi kwa wapinzani na kuwatahadharisha  watawala kwamba dhambi itawatafuna kwani wapo viongozi wengine wa CCM wana mali nyingi na mahoteli makubwa kuliko shamba lake lakini hawaguswi.

VIDEO: KAMA ILIKUPITA HII ICHEKI

Leave A Reply