The House of Favourite Newspapers

Swissport Yasisitiza Ushirikiano na ATCL

0
Mkurugenzi Mkuu wa Swissport Tanzania Mrisho Yassin, akizungumza na waandishi wa habari wakati wa wakiingia makubaliano ya kufanya kazi pamoja kati ya Swissport na Air Tanzania.
Mkurugenzi Mkuu wa Swissport Tanzania Mrisho Yassin (wa tatu kulia), pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Mipango Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) Kitula Yango ( wa tatu kushoto) wakikata keki wakati wakiingia makubaliano ya kufanya kazi pamoja.
Baadhi ya wafanyakazi wa Swissport Tanzania wakiwa katika hafla hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Swissport Tanzania Mrisho Yassin (katikati), akimsikiliza Kaimu Meneja wa kituo cha uwanja wa ndege , Barton Komba (kulia) wakati wakiingia makubaliano ya kufanya kazi pamoja kati ya Swissport na Air Tanzania, khafla iliyofanyika katika viwanja vya ndege terminal 3 , (kushoto) ni Mkurugenzi wa fedha Swissport Tanzania, Imani Mtafya
Mkuu wa Kitengo cha Mipango Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) Kitula Yango (katikati) akifafanua jambo.  (kushoto) Mkurugenzi Mkuu wa Swissport Tanzania, Mrisho Yassin na Mkurugenzi wa fedha Swissport Tanzania Imani Mtafya.

 

KAMPUNI ya kuhudumia mashirika ya ndege, abiria na mizigo katika viwanja vya ndege ya Swissport imesema kuwa kuanza sasa italisapoti Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) ili kuhakikisha linatoa huduma bora na nzuri kwa watanzania kwa lengo la kukuza na kuinua uchumi wa nchi.

 

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam na Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Mrisho Yassin wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkataba walioingia na ATCL wa kuhudumia ndege, abiria na mizigo ya Shirika hilo itakayokuwa inatua katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Mwalimu Nyerere na kiwanja cha ndege cha Kilimanjaro.

 

Yassin alisema Swissport kuanza kuhudumia ATCL ni fursa kubwa kwao hivyo watahakikisha wanalisapoti Shirika hilo kwa kujipanga kikamilifu kufanya kazi kwa bidii na kutoa huduma bora ili kuleta mabadiliko chanya.

 

Kazi hii tuliyopewa ni kubwa na kiukweli ATCL kwa sasa ni jina kubwa hivyo tunapaswa kuitendea haki fursa hii, wafanyakazi wenzangu tukiharibu kwa watu hawa itatubomoa na mimi kama kiongozi sipendi jambo hilo litokee ; alisema.
Hata hivyo alisema jumla ya watu 90 wamepata ajira katika kampuni hiyo baada ya kuingia mkataba huo kwa lengo la kuongeza nguvu na kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa watanzania.

 

Kiukweli kampuni tumejipanga kuhakikisha kwamba tunaweza kuwahudumia ATCL na kukidhi mahitaji yao kulingana na mkataba tuliyoingia, niendelee kuwahakikishia kwamba hatutawaangusha; alisema.

 

Naye Mkuu wa Kitengo cha Mipango ATCL, Kitula Yango alisema matarajio yao ni kwamba Swissport itafanya kazi kwa ufanisi mkubwa na weledi wa hali ya juu ili iweze kuendelea kuwahudumia kila wakati.

 

Alisema anatumaini kuwa kampuni hiyo itazingatia kila kilichokuwepo kwenye mkataba ikiwamo kutochelewesha ndege bila sababu ya msingi.

Leave A Reply