The House of Favourite Newspapers

Asha Baraka: Muziki wa Dansi Umekosa Promo

0

MWANAMKE mpambanaji ambaye mpaka sasa anaupigania muziki wa dansi Bongo ni Asha Baraka. Kutokana na jitihada zake UWAZI limezungumza naye kwa kina kuhusu mwelekeo wa muziki wa dansi nchini.

 

Uwazi: Tunahitaji kujua historia yako katika muziki.

Asha Baraka: Nilianza kuingia kwenye muziki kwa kuwa nilikuwa napenda, nilianza mwaka 1992 nikiwa na bendi ya City Sound. Nilikuwa meneja na akina Nyoshi Eli Sadaat.

 

Uwazi: Nini kilikufanya upende kuongoza muziki?

Asha Baraka: Ni hali ya kupenda muziki tu kutoka moyoni ndio ambayo ilinifanya nipende kuongoza wenzangu, kwenye muziki nikaona nianzishe bendi.

 

Uwazi: Katika uongozi wa Twanga pepeta, inasemekana ni bendi ya familia. Kuna ukweli kuhusu hilo?

Asha Baraka: Kulikuwa na bendi inaitwa Mk Group, hiyo ilikuwa ya familia nikiwa mimi, Omary Baraka na Baraka Musilwa. Baadaye nao wakabadilisha upepo, ikabidi mimi nianzishe Afrikan Star na baadaye nikabadilisha jina na kwa sasa hivi inaitwa Twanga pepeta ambayo hivi sasa inamilikiwa na kampuni ya Twanga pepeta Entertaiment.

 

Uwazi: Twanga pepeta ipo chini ya kampuni ya African Stars Entertainment Asset, ambayo mkurugenzi ni wewe. Je, kuna wakurugenzi wengine zaidi yako?

Asha Baraka: Kwa sasa mimi si mkurugenzi, tumebadilisha kila kitu na Mkurugenzi kwa sasa ni Luwiza Mbutu na kiongozi wa bendi ni Kalala Junior.

 

Uwazi: Twanga ilizalisha waimbaji mahiri kama Banza Stone, Ally Choki, Msafiri Diof, Mwijuma Muumin, Chalz Baba, Khalid Chokoraa, Fagason na kadhalika. Nini siri ya kuzalisha waimbaji wazuri katika bendi yako?

 

Asha Baraka: Unajua kipindi kile kila msanii alikuwa akija kwa wakati wake, alianza Banza Stone baadaye akaondoka na akaja Ally Choki na nyimbo ya jirani, wakina Jesca Charles, akaja na fainali uzeeni na baadaye Banza akarudi kutoka uholanzi ambako alitaka kuzamia, akaona arudi tu Tanzania ndipo akatunga wimbo wa mtu pesa akimaanisha hata uwe na pesa za aina gani huwezi kununua uhai kwa hiyo ule wimbo aliutengeneza kwa kufundisha maisha halisi ya binadamu akiwa na pesa nyingi anasahau kuwa kuna umauti. Ni wimbo ambao ulikuwa ukifundisha sana.

 

Uwazi: Unadhani ni kwa nini muziki wa dansi unafifia ukilinganisha na Bongo fleva?

Asha Baraka: Muziki wa Dansi haujafifia, bali ni kuupromot tu ndio kinachotakiwa kama unavyopromotiwa muziki wa Bongo Fleva.

 

Uwazi: Uliwahi kuwa na bendi ya chipolopolo, kwa nini ilikufa?

Asha Baraka: Ile bendi niliianzisha kwa sababu mimi napenda sana mpira, sasa kutokana na kipindi kile kuna timu ya mpira ya Zambia walikuwa wanasafiri wakapata ajali wakafariki wote, alibakia mmoja tu ambaye hakusafiri. Kwa kuwa tukio lile lilihuzunisha Afrika na Dunia nzima, nikaona kuwaenzi na kuanzisha bendi hiyo na pia kwa kuwa baba yetu wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa ana mahusiano mazuri na nchi nyingine za Afrika ikiwemo Afrika Kusini pamoja na Zambia, nikaona nianzishe lakini ndio hivyo ikafa. Nikaona nibaki na twanga pepeta.

 

Uwazi: Nini maoni yako kuhusu muziki wa dansi?

Asha Baraka: Maoni yangu ni kwamba muziki wa dansi bado upo na una wapenzi wao na sasa huwa tunafanya matamasha makubwa ambayo yanabeba watu mbalimbali na pia tunashirikiana na wanamuziki wengine na hivi sasa tunaelekea Kigoma kwa ajili ya kumsapoti Diamond kwa hiyo ukiona hivyo ujue kuwa Dansi bado ipo hai na Watanzania waendelee kuisapoti tu.

 

Uwazi: Vipi kuhusu bendi ya Tamtam ambayo ilikuwa chini ya Mwijuma Muumini, ilikuwaje mpaka ikafa?

Asha Baraka: Muumini alikuwa Tamtam, hii ilianzishwa baada ya yeye kuja kutoka Nairobi. Alipofika akataka kuingia Twanga, sasa kwa kuwa kule kulikuwa kumejaa tukaanzisha Tamtam ambayo alikuwa akiisimamia, lakini baadaye alikwenda Mchinga Sound na kwa kuwa tulikuwa na bendi nyingine ile bendi ikafa na baadaye alirudi tena Twanga pepeta.

 

Uwazi: Ni mafanikio yapi ambayo Twanga pepeta imeyapata mpaka sasa?

Asha Baraka: Mafanikio ni makubwa kwa sababu mpaka sasa ina miaka ishirini, vijana wamepata ajira, tumepata umaarufu, tumejulikana na tunapata mambo mengine tofauti kwenye kampeni na mambo mengi mbalimbali. Kwa hiyo, twanga imetupa mafanikio makubwa sana.

Makala: Neema Adrian

Kwa kuwa jambo hili linatakiwa lifanyike kesho, hatuwezi kukata rufaa, tunaamini mahakama ilikuwa na uwezo wa kuamua,” amesema Wakili Jebra.
Leave A Reply