The House of Favourite Newspapers

Taarifa ya Kipigo cha Wema yazua Taharuki

0

DAR: Taarifa iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikidai kuwa msanii maarufu wa Bongo Muvi, Wema Isaac Sepetu amelazwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kutokana na kipigo, imezua taharuki miongoni mwa mashabiki wake.

 

Mapema wiki hii kwenye mitandao ya kijamii ilisambaa taarifa hiyo huku kundi la vijana likitajwa kumvamia staa huyo nyumbani kwake na kumshambulia kwa madai ya kuiba mume wa mtu.

 

Katika taarifa hiyo, mwanamke aitwaye Situmai Tambwe alitajwa kushikiliwa na jeshi la polisi na kukiri kuwatuma vijana hao kumpa kipigo Wema baada ya kunasa mawasiliano kati yake na mume wa mtuhumiwa.

Pole, hofu, huruma na manenomaneno kuwa mengi, mwandishi wetu alilazimika kufuatilia ukweli wa tukio hilo na kugundua jambo la ajabu.

 

Msingi wa tukio ulioenezwa kwenye mitandao ya kijamii ni kwamba, Stumai kupitia application fulani ambayo si vyema kuitaja kwa sababu Ijumaa limejiridhisha kuwa ni ya uongo, ndiyo aliyotumia kunasa mawasiliano ya Wema na mume wake.

Aidha, baada ya kile kilichodaiwa mtuhumiwa huyo alikodi vijana ambao walikwenda nyumbani kwa Wema na kumfanyia mbaya ambapo baadaye jeshi la polisi lilimtaiti Situmai na kukiri kosa.

 

Hata hivyo, mwandishi wetu alikosa doti za kuunganisha taarifa hiyo na Situmai kwa kuwa ni nadra mahojiano ya mtuhumiwa na vyombo vya usalama kupatikana vikieleza neno kwa neno kama ilivyokuwa imesambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

 

Kwa kuzingatia hilo, mwandishi wetu aliwasiliana kwa njia ya simu na meneja wa Wema aitwaye Neema Ndepanya ili kujua undani wa tukio hilo lililozua sintofahamu mitandaoni ambapo alisema:

“Hata mimi nimeiona hiyo (taarifa) lakini ni uzushi kwa sababu nimeongea na Wema mwenyewe yuko vizuri hana shida yoyote, huyo ni mtu aliyeamua kutengeneza habari kwa lengo la kujipatia kiki.”

 

Baada ya mwandishi wetu kutafakari majibu hayo, aliona ipo haja ya kumtafuta Wema ili kujua ni kwa nini Stumai amtumie yeye kupata kiki na si mwanamke mwingine yeyote.

“Hii si mara ya kwanza kufanyika kwa habari ya uongo dhidi yangu, nadhani umaarufu wangu ndiyo tatizo ndio maana wananitumia ili kupata kiki na kufanikisha malengo yao.

“Mimi ni mzima na hapa ninapoongea na wewe, niko bize jikoni kwangu, hizo taarifa naomba mashabiki zangu wazipuuze,” alisema Wema.

 

TAARIFA ZILIZOLETA TAHARUKI

“Mimi katika simu yangu nina application moja inaitwa (tunazuia jina) hii application ya …niliipata playstore nika download katika simu yangu.

“Kazi kubwa ya hiyo application ya… ukiwa nayo katika simu unaweza kufuatilia meseji za mtu yeyote baada ya kudownload hiyo application ya …nilichukua namba ya simu ya mume wangu na kuiunganisha na namba ya mume wangu katika hiyo application, ndipo nikawa nakamata meseji za mume wangu kupitia hiyo application pasipo mume wangu kujua.

 

“Ndipo nikanasa meseji za huyu msanii Wema Sepetu kupitia hiyo application. Anamtumia mes eji mume wangu, nilipofuatilia nikagundua huyu Wema ana mahusiano ya kimapenzi na mume wangu, ndipo nikachukua namba ya Wema Sepetu na kumpigia ili kumuonya aweze kuachana na mume wangu, lakini akawa ananijibu jeuri na matusi ndipo nikachukua maamuzi hayo,” haya ndiyo maelezo ya mtuhumiwa Situmai Tambwe na anashikiliwa na jeshi la polisi mpaka sasa!

 

Aidha, Ijumaa limefuatilia maelezo yao na kugundua kuwa ni ya uongo ambayo yanalenga kuwalaghai watu ili kuwaibia fedha; jamii inapaswa kuwa makini na utapeli huo.

 

Stori: IMELDA MTEMA, Ijumaa

Leave A Reply