Taasisi ya Wananchi Wazalendo Tanzania Yatoa Elimu kwa Kutumia Michezo
TAASISI ya Wananchi Wazalendo Tanzania (TWWT) imetoa elimu ya uzalendo kwa kutumia michezo katika tamasha lililofanyika Uwanja wa Kituo cha Wilaya ya Kipolisi ya Chanika jijini Dar.
Tamasha hilo lililokusanya maelfu ya wahudhuriaji lilianza na maandamano ya wananchi waliokuwa wakiimba nyimbo za kizalendo na kupambwa na burudani mbalimbali ikiwemo vigoma, matarumbeta na kumaliziwa na fainali ya mpira wa miguu kati ya timu ya Polisi Chanika na vijana wa Chanika Combine.
Katika fainali hiyo iliyokusanya maelfu ya watazamaji timu ya Chanika Combine inayoundwa na vijana wa maeneo hayo ndiyo walioibuka na kombe hilo sambamba na jezi mpya. Kabla ya mechi hiyo kulikuwa na maneno ya uhamasishaji uzalendo wa taifa la Tanzania yaliongozwa mgeni rasmi ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wananchi Wazalendo Tanzania (TWWT), Dkt. Ezekiel Kyogo ambaye pia ni Mkuu wa Upelelezi OC-CID wa Wilaya ya Kipolisi ya Kariakoo.
Katika tamasha hilo wananchi kwanza walifundishwa umuhimu wa kuipenda na kuijenga nchi yao kuaswa kutokubali kuisaliti kwa namna yeyote ile. Dkt. Kyogo amesema unakuta kuna mtu mwingine kwa kukosa uzalendo anasambaza mitandaoni picha au video zinazodhalilisha taifa.
Wananchi hao pia walielimishwa juu ya kuacha uharifu na madhara ya matumizi ya dawa za kulevya na aina nyingine za vilevi haramu vinavyokatazwa na serikali ambavyo vimeshaharibu sana nguvu kazi ya taifa. Akizungumza kwenye umati huo Dkt. Kyogo alisema;
“Ndugu wananchi naomba tumuunge mkono Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ambaye anaupinga mwingi kwa kuleta maendeleo ya kazi na kudumisha amani na utulivu.
“Tusipokuwa wazalendo ni ngumu kuendelea kuwa na amani hivyo basi tukiwa wazalendo na nchi yetu tumuunge mkono Rais wetu Mama Samia Suluhu, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camilius Wambura, RPC wetu wa Kanda Maalum wa Dar es Salaam Murilo Jumanne na RPC wa mkoa wa Kipolisi wa Ilala tulipo hivi sasa, Kamishna Msaidizi, Debora Magilingimba”. Alimaliza kusema Dkt. Kyogo. HABARI/PICHA: NA RICHARD BUKOS NA ISSA MNALLY /GPL