TAHARUKI MAKABURINI DAR!

DAR ES SALAAM: Taharuki ya aina yake imeibuka hivi karibuni maeneo Kiwalani jijini Dar ambapo baadhi ya wananchi wamedai kuwa, katika zoezi la uhamishaji wa makaburi kupisha barabara, kaburi za ndugu zao zimefukuliwa bila wao kujua zimepelekwa wapi.  

 

Wakizungumza na Amani, wananchi hao wamedai kuwa wao hawakushirikishwa kwenye ufukuaji wa makaburi ya ndugu zao na kinachowauma ni kwamba hawajui maiti ziko wapi.

“Afadhali nyie waandishi mmefika ili mtusaidie katika hili, mimi naitwa mzee Juma Kubero, naishi mtaa wa Minazi Mirefu, hapa kwenye haya makaburi nimezika wajukuu zangu wawili na mtoto wa mdogo wangu anaitwa Ramadhani Maine, cha kushangaza ni kwamba hatujapewa taarifa yoyote kuhusu wao kubomoa haya makaburi na kuyahamishia sehemu nyingine.

 

“Nilipata taarifa tu kutoka kwa watu kuwa makaburi ya eneo hili yamefukufuliwa, ndiyo nikasema nifike hapa kujionea, ni kweli hata kaburi za ndugu zangu hao zimefukuliwa na kuhamishiwa kusikojulikana, sasa hii ni sawa jamani?” alihoji mzee huyo huku akionekana aliyechanganyikiwa.

 

Mwananchi mwingine aliyekumbwa na balaa hilo aliyejitambulisha kwa jina la Haji Ngonyani naye alisema kuwa haelewi mpango huo ulikuwaje lakini juzi alipita na kukuta makaburi ya watoto wake yanabomolewa. “Sielewi ishu nzima ikojeikoje maana juzi nilipita tu hapa baada ya kutoka kumzika mke wangu, nikakuta makaburi ya watoto wangu yanachimbuliwa na watu waliokuwa wamevalia maovaroli.

 

“Nikawauliza kwa nini wanafanya hivyo, yaani wanachimbua makaburi ya watoto wangu bila kunipa taarifa, wakasema wao walishatoa taarifa siku 30 zilizopita hivyo hawana muda wa kusubiri, pia wakaniambia kama sikuandikisha jina serikali ya mtaa basi siwezi kupata kitu chochote bali watapata wale walioandikisha tu. Huwezi amini hata walipoenda kuwazika watoto wangu sipajui, hivyo nawasubiri watakaporudi tena wakanionyeshe walipowaweka wanangu,” alisema Haji kwa uchungu.

 

Hata hivyo, Juma Bakari ambaye ni mkazi wa eneo hilo aliwataka wananchi watulie na kuiacha serikali ifanye kazi yake kwani kinachofanyika ni cha kimaendeleo.

“Mimi sina ndugu niliyezika hapa lakini naamini serikali inapoamua kufanya jambo kama hili la kimaendeleo, hatakiwi mtu yoyote kulipinga kwa sababu hii ni kwa faida yetu, mimi ni muislamu hivyo hata kama ningekuwa na ndugu niliyemzika hapa ningechukua hizo pesa na kwenda kutoa sadaka,” alisema Juma.

 

Akizungumza na Amani, mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo aliyefahamika kwa jina la Rajabu Abdallah alisema kuwa serikali ilishatoa taarifa kwa wananchi wa eneo hilo muda mrefu lakini cha kushangaza ni kwamba kuna wananchi ambao hawakufika ofisini kwake kujiandikisha majina yao na ndio hao ambao siku hiyo walikuwa wanalalamika.

 

“Tulianza kwa kutoa matangazo kwenye gazeti la serikali na redio ambapo yalitolewa kwa siku 30, mchakato wa pili tuliitisha kikao cha wafiwa na viongozi ambapo tulikubaliana kuwa wale ambao makaburi yao hayakujengewa walipwe fidia ya shilingi 200,000 na wale ambao walijengea walipwe fidia ya shilingi 45,0000. Basi tulikubaliana hivyo na zoezi likaanza ambapo juzi (Jumamosi iliyopita) tulichimbua makaburi 59, jana (Jumapili iliyopita) tukachimbua makaburi 61, jumla yakawa makaburi 120 ambapo maiti zilienda kuzikwa Kinyamwezi.

 

“Na pale pana makaburi zaidi ya 200 hivyo bado zoezi la kuchimbua makaburi linaendelea, sasa changamoto iliyopo ni kwamba kuna watu wamejitokeza wanadai hawakupata taarifa kwa hiyo wanahitaji kulipwa lakini sasa serikali ilishajipanga kuwalipa wale ambao walishatangulia kujiandikisha mwanzo, lakini haimaanishi kwamba na wao hawatalipwa hapana, niseme tu kwamba wananchi watulie na waamini serikali ipo na watapata haki yao,” alisema kiongozi huyo.

Stori: Memorise Richard, Amani

Toa comment