The House of Favourite Newspapers

Taifa Stars Imeandaliwa Vilivyo, Mtihani Ni Leo dhidi ya Uganda

0

TANGU siku ya kwanza ya kambi ya timu taifa hapa jijini Ismailia nchini Misri nimekuwa hapa nikishuhudia.

Timu ya taifa ambayo ni mara ya kwanza kocha mpya anaanza kazi lakini inakwenda katika mechi muhimu sana dhidi ya Uganda, leo.

Mechi ya kuwania kufuzu kuwania kucheza Afcon, itakuwa ni ngumu kwa kuwa katika miaka ya hivi karibuni, Tanzania dhidi ya Uganda haijawahi kuwa nyepesi.

Mechi mbili zilizopita, Uganda walishinda ugenini kwa Mkapa kwa bao 1-0 na Tanzania wakashinda kwa bao 1-0 katika mechi ya kirafiki, sasa ni mechi nyingine ya mashindano na Uganda chini ya Sredejovic Milutin ‘Micho’ waliwasili siku moja waliyowasili Taifa Stars.

Ismailia ni mji ulio umbali wa takribani saa mbili kutoka Jiji Cairo na Stars iko ugenini dhidi ya The Cranes ambao wamechagua Uwanja wa Suez Canal, uwanja mpya ulio katika mji huu kwa kuwa viwanja vya Uganda vimeshindwa kukidhi matakwa ya Caf.

Tayari nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta amesema: “Mechi yetu dhidi ya Uganda si nyepesi siku zote, tunajua itakuwa mechi ngumu lakini tutaungana pamoja kuhakikisha tunafanya vizuri. Tukiunganisha nguvu tunaamini ni jambo linalowezekana.”

Tayari wachezaji wa Stars wameambiwa lkuwa nafasi ya Tanzania kufuzu Afcon ni kumfunga Uganda hapa Misri na jijini Dar es Salaam siku chache zijazo. Sasa kazi kwao.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wamefanya kazi kubwa katika mambo yanayoihakikishia timu kujiandaa inavyotaka.

Licha ya kuajiri Kocha mpya, Adel Amrouache raia wa Ubelgiji lakini kuna makocha wa viungo, makipa, mifumo pamoja na mtaalamu wa video kwa ajili ya kulisaidia benchi la ufundi dhidi ya wapinzani lakini Stars pia.

Kambi ambayo wamefikia Taifa Stars ni moja ya kambi bora kabisa na historia ya kambi hii inaonyesha ndio sehemu timu kadhaa kubwa za Afrika wakiwemo Senegal chini ya Sadio Mane wamekuwa wakifikia hapa.

Eneo kubwa la hoteli hiyo, lenye viwanja viwili vya kisasa kwa ajili ya mazoezi, mabwawa bora ya kimazoezi kwa ajili ya timu za kuogelea, soka na michezo mingine.

Sehemu maalum ya kukimbilia nje ya uwanja lakini eneo kubwa linalowapa nafasi wachezaji kupumzika wanavyotaka baada ya mazoezi.

Achana na hivyo, hoteli hii ni mali ya jeshi na iko karibu na kambi ya jeshi katika Mfereji wa Suez. Hii maana yake ulinzi ni wa kutosha kupitiliza.

Kazi kubwa ni kwa wachezaji sasa, wao ndio wanatakiwa kupambana kwa kuwa maandalizi yao yapo vizuri na yameandaliwa sawasawa ikiwemo kuhakikisha wanalipwa stahiki zao zote hata kabla ya mechi.

Kocha Amrouche ameanza kazi hapa Misri lakini tayari kocha wa viungo kutoka Finland alianza kazi akiwa chini ya Kocha Msaidizi, Hemed Morocco ambaye aliongozana na kikosi hicho mwanzoni kabisa.

Ukiwaangalia wachezaji wanaonekana wana utayari, wako vizuri na mechi ya leo wanaitaka na kikubwa ni kuendelea kuwaombea wanachokihitaji kufanikiwe.

Uganda si timu nyepesi na wanapocheza na Tanzania hujiandaa hasa kwa kuwa matamanio yao ni kuwa wakubwa kuliko Tanzania ambayo inawazidi vitu vingi sana. Hivyo wanaamini katika mpira ni sehemu ya kuonyesha walichonacho dhidi ya nchi hiyo kubwa na tajiri kuliko wao.

Kama alivyosema Samatta, haitakuwa mechi nyepesi, maana yake lazima kuwe na mapambano ya uzalendo, nia ya ushindi na kama Stars utafanikiwa kushinda leo, basi itakuwa imeanza na mguu bora.

Na Saleh Ally, Ismailia

KISA KUTOCHEZA MUDA MREFU, KOCHA TAIFA STARS AMPA FEISAL MAZOEZI MAALUM ya PEKE YAKE MISRI...

Leave A Reply