The House of Favourite Newspapers

Taifa Stars: Tupo Tayari Kuimaliza Uganda leo Saa 2:00 Usiku Uwanja wa Mkapa

0
Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars

KOCHA Msaidizi wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Hemmed Morocco, amesema watafanya kazi kubwa kwa ajili ya kupata ushindi dhidi ya Uganda.

Leo Jumanne, Taifa Stars ina kazi ya kusaka ushindi kwenye mchezo dhidi ya Uganda unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa, Dar, ukiwa ni wa kufuzu AFCON. Mechi inatarajiwa kuanza saa 2:00 usiku.

Mchezo uliopita ambao Uganda ilikuwa mwenyeji mechi ikichezwa Misri, Taifa Stars iliibuka na ushindi wa bao 0-1, mfungaji akiwa Simon Msuva.

Kocha Morocco alisema mchezo uliopita walionesha kiwango kikubwa jambo ambalo linahitajika, huku mpango mkubwa ikiwa ni kupata matokeo mazuri ya mwendelezo.

“Tupo nyumbani na tunapata nguvu kutoka kwa mchezaji wa 12 ambao ni mashabiki, kikubwa ambacho tunahitaji ni kupata ushindi na tunaamini inawezekana.

“Tutabadili aina ya kikosi kutokana na aina ya wachezaji ambao tupo nao na tuna kazi kubwa kwa kuwa Uganda ni timu ngumu, lakini nasi pia tupo vizuri. Kuongezeka Kwa Shomari Kapombe na Mohamed Hussein kuna kitu kitaongezeka,” alisema Morocco.

Simon Msuva, nyota wa Taifa Stars ambaye alifunga katika mchezo dhidi ya Uganda ugenini, alisema wachezaji watapambana kupata ushindi kwenye mchezo huo.

“Tuna kazi kubwa ya kufanya na kila mmoja anatambua kazi iliyopo katika kusaka ushindi, tutashirikiana katika kupata matokeo mazuri na kwa uwezo wa Mungu nitafunga tena,” alisema Msuva.

Kocha Mkuu wa Uganda, Milutin Sredojević ‘Micho’ alisema mchezo huo ni muhimu kupata matokeo mazuri baada ya kupoteza mchezo uliopita.

“Tulipoteza mchezo uliopita na sasa tunahitaji ushindi kwenye mchezo huu ambao ni muhimu, tunawaheshimu wapinzani, lakini tupo tayari kupata matokeo chanya,” alisema Micho.

Nahodha wa Uganda, Emmanuel Okwi, alisema kila kitu kipo sawa wanatarajia kupata ushindi katika mchezo huo mgumu.

“Mchezo wetu dhidi ya Tanzania utakuwa mgumu, lakini tunatarajia kupindua meza, wao walishinda nyumbani kwetu nasi tutapambana kupata matokeo katika mchezo wetu wa kesho (leo),” alisema Okwi.

JAMBO LA NCHI

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo, amesema kuwa kuna tiketi 43,000 ambazo zimenunuliwa na wanaendelea kupokea ahadi kutoka kwa wadau mbalimbali.

“Tunataka kuujaza uwanja kwa pamoja ili kufanikiwa kukata tiketi ya kufuzu AFCON, tunaamini kazi itafanyika na mashabiki wajitokeze kwa wingi.

“Mo Dewji ametoa tiketi 5000, Azim Dewji ametoa tiketi 1000 kwa wafanyakazi wake pamoja na Kampuni ya Africaries wadhamini wa Simba wametoa tiketi 1000 na kufanya jumla ya tiketi 8,000, Munir Said Mjumbe wa Kamati ya Yanga aliahidi kutoa tiketi 150, Hussein Masanza Ofisa Habari wa Singida Big Stars alitoa tiketi 100,” alisema Ndimbo.

WAANDISHI: LUNYAMADZO MLYUKA, HAPPINESS LAURENT NA OMARY MICHUZI

#EXCLUSIVE: ”KWENYE USAJILI TUMEPIGWA” – MO DEWJI AFUNGUKA SABABU ya KUKWAMA NUSU FAINALI | PART 3

Leave A Reply