The House of Favourite Newspapers

Tambwe Naye Mbioni Kuikacha Yanga

0

Sekeseke la usajili wa wachezaji wa Kimataifa unamuhusu pia Amissi Tambwe.

SIKU chache baada ya uongozi wa Yanga kutangaza rasmi kuachana na Mnyarwanda, Haruna Niyonzima baada ya kushindwa kufi kia makubaliano naye ya kuongeza mkataba, mshambuliaji wa timu hiyo, Mrundi, Amissi Tambwe naye inawezekana akafuata nyayo za mwenzake huyo.

Hivi sasa hofu kubwa ya kumpoteza mshambuliaji huyo kama ilivyojitokeza kwa Niyonzima imetanda ndani ya klabu hiyo baada ya kuwepo kwa taarifa kuwa kuna klabu moja hapa nchini imemtengea dola 30,000 (Sh milioni 70) ili aweze kujiunga nayo.

Kutokana na hali hiyo, uongozi wa Yanga umemuita mara moja Tambwe kwa ajili ya kufanya naye mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya na leo Ijumaa anatajia kutua nchini akitokea kwao Burundi alikokuwa kwa ajili ya mapumziko baada ya kumalizika kwa michuano ya ligi kuu.

Akizungumza na Championi, mmoja wa viongozi wa Kamati ya Usajili ya Yanga, ambaye aliomba kutotajwa jina lake gazetini alisema kuwa baada ya kushindwa kumbakiza Niyonzima klabuni, pia taarifa walizozipata ni kuwa Tambwe anawindwa na moja ya timu za hapa nchini ambayo ipo vizuri kiuchumi, imebidi wamuite haraka iwezekanavyo kwa ajili ya kufanya naye mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya kwa sababu bado wanamuhitaji sana.

Alipotafutwa Tambwe na kuulizwa kuhusiana na suala hilo alisema: “Ni kweli kabisa uongozi umeniita na kesho (leo) Mungu akipenda nitakuwa Dar es Salaam kwa ajili ya mazungumzo.

“Hata hivyo, mpaka sasa sijui watanipa kiasi gani cha fedha lakini ngoja niwasikilize kwanza baada ya hapo nitajua nini cha kufanya kwa sababu nina ofa kama tatu hivi, lakini kwa vile Yanga ndiyo niliyokuwa naitumikia basi imebidi niwape nafasi ya kuzungumza nao kwanza kabla ya kufanya maamuzi mengine,” alisema Tambwe.

Sweetbert Lukonge

Stamina, Darassa Kulipeleka Jiji Dar Live Sikukuu ya Idd Mosi

Leave A Reply