The House of Favourite Newspapers

TANASHA AMTENGANISHA DIAMOND, MAMA’KE

DAR ES SALAAM: Ama kweli mapenzi yana nguvu zaidi ya greda! Hatimaye mchumba wa staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Tanasha Donna Oketch amefanikiwa kumtenganisha jamaa huyo na mama yake mzazi, Sanura Kassim ‘Bi Sandra’, Gazeti la Amani lina exclusive.  

 

Habari kutoka ndani ya familia ya Diamond au Mondi zilieleza kuwa, staa huyo mkubwa Afrika Mashariki ameondoka nyumbani kwa mama yake, Madale-Tegeta na kwenda kuishi na Tanasha kwenye jumba jipya la kifahari alilolapangisha lililopo maeneo ya Mbezi-Beach kwenye Ufukwe wa Bahari ya Hindi jijini Dar kwa shinikizo la mwanamke huyo.

 

MONDI HAJAWAHI…

Gazeti la Amani linafahamu kwamba, Mondi hajawahi kuishi mbali na mama yake na mara kadhaa amekuwa akieleza kuwa popote atakapokwenda kuishi, ataambatana na mama yake huyo kutokana na maisha ya mateso waliyopitia pamoja. Waliishi wote tangu wakiwa Tandale kisha walihamia Sinza-Mori kabla ya Mondi kumjengea mama yake huyo ule mjengo wa Madale- Tegeta ambako walikwenda kuishi wote.

TANASHA AVUNJA REKODI

Lakini sasa inadaiwa kuwa, Tanasha ambaye ni mtangazaji wa redio wa nchini Kenya amevunja rekodi ya wapenzi wote wa Mondi waliopita wakiwemo Wema Isaac Sepetu, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’, Hamisa Mobeto na wengine baada ya kufanikiwa kumbandua jamaa huyo mikononi mwa mama yake.

 

Chanzo hicho cha ndani ya familia ya Mondi kilieleza kwamba, hivi karibuni Tanasha alikaribishwa kwenye mjengo huo wa Mbezi- Beach na kuelezwa hapo ndipo nyumbani kwake.

“Unajua ni kweli kwamba Nasibu (Mondi) amekuwa hataki kuishi mbali na mama yake, lakini baada ya kuwa na Tanasha, anaonekana kukubali yaishe hivyo ameamua kuhamia kwenye mjengo wa kifahari aliopangisha maeneo ya Mbezi-Beach.

 

“Awali nyumba hiyo ilisemekana kuwa Mondi aliipangisha kwa ajili ya kutengenezea tamthiliya na familia yake, lakini sasa mambo yamebadilika kwa sababu ndiyo nyumba anayoishi na Tanasha. “Unajua hata sisi tulishangaa ni tamthiliya gani hiyo inayorekodiwa kwa gharama kubwa kiasi hicho? Maana ule mjengo siyo wa kitoto na ndani yake kuna fenicha za gharama kubwa.“Ukiacha fenicha, pia Nasibu ameikarabati nyumba kwa gharama kubwa, watu wakijua ni kwa ajili ya tamthiliya kumbe ana lake jambo.

“Nahisi jamaa alikuwa hayupo huru kuishi na mwanamke nyumbani kwa mama yake. Hata kama wapenzi wake waliopita walikuwa hawamwambii, lakini inawezekana ilichangia kuvunjika kwa uhusiano wao na bro (Mondi). “Nadhani Tanasha aliliona hilo na inawezekana ameshausoma mchezo hivyo hataki yamkute yaliyowafika wengine waliokuwa wanabanana pale Madale,” kilihitimisha chanzo hicho.

 

Ili kupata undani wa ishu hiyo juu ya Diamond kuhamia kwenye mjengo huo wa ghorofa moja na kumwacha mama yake, Amani lilimtafuta Bi Sandra au mama Dangote, lakini lilimkosa. Badala yake lilimpata Esma Khan ‘Esma Platnumz’ ambaye ni dada wa Mondi.

 

ESMA AFUNGUKA

Esma, katika mazungumzo yake na Amani, alisema kuwa ni kweli wao kama familia walimpokea Tanasha kwenye mjengo huo na baada ya hapo walimwacha. “Ni kweli tulimpokea mkwe wetu kwenye mjengo mpya wa Nasibu (Mondi), lakini baada ya hapo mama yetu (mama D) atarudi zake Madale na kuwaacha na nyumba yao.

“Sisi kama familia, hatuna shida na kaka yetu (Mondi) na tupo tayari kumpokea yeyote ambaye atatutambulisha na hatuwezi kuwa na kipingamizi,” alisema Esma ambaye alipoulizwa kama huo utakuwa mwanzo wa Mondi kutengana na mama yake alisema wao wanakubaliana na uamuzi wa Mondi. “Nimeshakuambia sisi hatuna kipingamizi na uamuzi wake,” alimalizia Esma.

HUYU HAPA FELA

Kuhusu mjengo huo mpya wenye gharama kubwa kudaiwa kutumika kwa ajili ya kutengeneza tamthiliya ya familia ya Mondi na siyo makazi ya jamaa huyo na Tanasha, Gazeti la Amani lilimtafuta mmoja wa mameneja wa staa huyo, Hamis Taletale ‘Babu Tale’ bila mafanikio.

Alipotafutwa Said Fela ‘Mkubwa’ ambaye naye ni mmoja wa mameneja wa Mondi alifunguka ukweli juu ya mjengo huo kwamba hapo ndipo makazi mapya ya mwanamuziki huyo na kukanusha suala la nyumba hiyo kutumika kwa ajili ya kutengeneza tamthiliya.

Stori: Neema Adrian na Shamuma Awadhi, Amani

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Comments are closed.